KESHO KUTOA UAMUZI WA KUFUTA AU KUTOFUTA DHAMANA
Na Karama Kenyunko, Globu ya Jami.
MAHAKAMA
ya ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Novemba 20, mwaka 2019 inatarajia
kutoa uamuzi wa kufuta au kutofuta dhamana ya wabunge wanne wa Chadema
baada ya kukiuka masharti ya dhamana.
Wabunge
hao ni Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini
Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini Ester
Bulaya ambao wamefika mahakamani hapo leo wakitokea katika kituo cha
polisi Osterbay jijini Dar es Salaam baada ya kujisalimisha kutokana na
amri ya Mahakama ya kuamuru wakamatwe.
Hatua
hiyo ya Mahakama imekuja bàada ya washtakiwa hao wote wanne kutoa
sababu zao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba zilizowafanya
kushindwa kufika mahakamani hapo Novemba 15, saa tatu asubuhi kama
Mahakama ilivyokuwa imepanga.
Wakitoa
sababu kwa nini wasifutiwe dhamana, washtakiwa Heche, Msigwa na Mdee
waliieleza Mahakama kuwa siku hiyo ya kesi walifika mahakamani hapo kwa
kuchelewa kutokana na sababu mbali mbali.
Mshtakiwa
Msigwa na Heche walidai kuwa walipata ajali wakiwa njiani kufika
mahakamani hapo huku Mdee yeye alidai aliugua ghafla akiwa njiani na
kumlazimu kupitia Hospitali kitendo kilichopelekea wote kufika
mahakamani kwa kuchelewa.
Kwa
upande wake, mshtakiwa Ester Bulaya alidai kuwa hakufika mahakamani
siku hiyo kwa kuwa alifiwa na mama yake Mdogo hivyo alikwenda Singida
kwa ajili ya Maziko.
"Wakati
kesi inaendelea siku ya mwisho nilijaribu kunyoosha mkono lakini
haukuniona Hakimu, mimi ni Mjumbe wa kamati ya Bunge ambapo baada ya
kesi, nilikimbia kwenda Dodoma alhamisi kwenye kikao ambacho kiliisha
saa moja na nusu usiku niliondoka saa mbili na nusu usiku na kuingia Dar
es Salaam saa mbili asubuhi. Kwenye akili yangu nilijua kesi ni saa nne
na nusu hivyo sikuwa na wasiwasi kama nitachelewa lakini wakati nikiwa
njiani kuja mahakamani nikiwa na Heche, tulipata ajali", amesema Msigwa.
"Mheshimiwa ninaheshimu Mahakama na siwezi kuidharau mahakama wala wewe binafsi,
Naomba Mahakama isinifutie dhamana yangu," alisema Msigwa.
Kwa
upande wake Mdee ameiomba Mahakama isimfutie dhamana yake kwani
anaiheshimu sana mahakamai ila siku hiyo wakati anakuja mahakamani
aliugua ghafla akapitia Hosp lakini kwa kihofia kuchelewa alimpigia
mdhamini wake ambae nae alifika kwa kuchelewa.
"Mimi
ninakaa karibu kilometa 1600 kutoka hapa, hapa mjini sina familia wala
mke, ila tangia kianza kwa kesi hii sijawahi kuchelewa mahakamani wala
kuonywa, ila siku ya kesi tukiwa njianj na Msigwa, gari iligongwa,
ikabidi tutafute pa kuiweka na kisha tukachukua boda boda lakini
tulipofika mahakamani tukakutana na wenzetu ndio wanatoka" amesema
Heche.
Wakati Bulaya
amesema, hawezi kuidharau mahakama, ila alifikwa na msiba wa mama yake
mdogo huko Singida, hivyo aliwataarifu wadhamini wake ili siku ya kesi
wafike, lakini nao walipofika walikuwa wamechelewa na kukuta kesi
imeahirishwa.
Hata hivyo
upande wa mashtaka kupitia wakili wa Serikali Salimu Msemo akiwasilisha
hoja ya kutaka washtakiwa wafutiwe dhamana amedai, ni muhimu suala muda
wa kuwepo mahakamani kuzingatiwa na ni dhahiri kuwa washtakiwa
hawakuwepo mahakamani wakati kesi hiyo inaahirishwa.
Hivyo
ninaiomba mahakama iwafutie dhamana washtakiwa hao wanne na
kuwachukulia hatia stahiki wadhamini wao.Akijibu hoja hizo, Wakili wa
utetezi Peter Kibatala amedai, hakuna sababu za kimazingira wala
kisheria za kufuta dhamana, uamuzi wa kutoa dhamana ni mwepesi zaidi
kuliko uamuzi wa kuifuta.
Hakuna
ubishi kwamba wakati wa kesi hii washtakiwa walikuwa na rekodi bzuri ya
kuhudhuria mahakamani na kwamba washtakiwa walitoa maelezo siku hiyo
walikuja mahakamani.
Ni
kweli kwamba kawaida kesi za jinai zinaanza saa tatu asubuhi lakini
tangu waanze shauri hili awajawahi kuanza muda huo bali wamekuwa
wakianza saa 4:30 asubuhi na kuendelea na kuongeza kuwa kuchelewa
mahakamani sio na kutofika.
Mahakama
sio mashine kwakuwa zipo sababu za kibinadamu na ndio maana kuna
mahakimu au majaji wanaofanya maamuzi na kutafsiri sheria.
Wabunge
watatu wa CHADEMA wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu kutoa amri ya wabunge wa 4 wa chama hicho wakamatwe
kwa kukiuka masharti ya dhamana.
Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo ni, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe,
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu bara na
Mbunge wa kibamba John Mnyika, katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent
Mashinji na Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko.
Katika
Kesi hiyo Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula
njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.
Pia,
wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa makosa
yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es
Salaam. Hata hivyo watuhumiwa hao wanne wamepelekwa mahabusu hadi kesho
uamuzi utakapotolewa.
Hata
hivyo, pia Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameshindwa kufika
mahakamani kwa sababu anaumwa na amelazwa katika Hospitali ya Aghakhan
chumba 507. Taarifa ya kuumwa kwa Mbowe, imetolewa mahakamani hapo na
Mdhamini wake, Grayson Selestine.






Naomba serikali iweze kuwalipa fidia wakazi wa Kifuru na Kibaga fidia kutokana na ujenzi wa umeme mkubwa utakatumika na reli ya kisasa ya SGR kwani mpaka sasa tingatinga liko site likiendelea kuchimba mitaro ya kusimika nguzo za umeme huo licha ya wananchi kutolipwa fidia.
ReplyDeleteNaomba serikali iingilie kati suala hili maana ni mwaka sasa tangu tathmini ifanywe