. Haki Rasilimali yapongezwa kwa kuwakutanisha wadau na wananchi wanaozungukwa na shughuli za uziduaji

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi jukwaa la tisa la sekta ya uziduaji liliofanyika jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo kutoka Mikoa yote nchini  na visiwani Zanzibar ambapo wote kwa pamoja wamejadili namna ya kukuza, kushiriki na kuendeleza sekta hiyo ya uziduaji  ambayo huangaza zaidi katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia.

Akizungumza katika warsha hiyo Waziri Kalemani amesema kuwa sekta hiyo inahitaji uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu na hiyo ni pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa wadau ambazo zitawasaidia kushiriki zaidi katika sekta hiyo ya uziduaji pamoja na wananchi wa maeneo husika ya rasilimali kunufaika na miradi hiyo chechemuzi inayopatikana katika mazingira yao.

Amesema matarajio katika sekta hiyo ni makubwa hivyo wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi hawana budi kutumia fursa hiyo ila lazima wazingatie sheria, kanuni, taratibu na miongozo kwa kuweka wazi mikataba yao.

Amesema kuwa wawekezaji lazima wahakikishe wananchi katika maeneo husika wanaona matokeo ya miradi hiyo inayowazunguka huku akiipongeza taasisi ya Haki Rasilimali kwa kuendelea kufanya vyema katika kuwashirikisha wadau kwa kutoa taarifa na kuhabarishana kuhusiana na sekta ya uziduaji.

Vilevile amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta hiyo ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi Trilioni 5.64 zimewekezwa katika viwanda vya mbolea na kemikali za petroli na shilingi Trilioni 1.1 zimewekezwa katika gesi za magari ambazo zitakuwa mbadala wa mafuta ya Petroli na Disel na kufikia sasa zaidi ya magari 320 yameunganishwa na mfumo huo.

Kalemani amewashauri Haki Rasilimali kuendelea kutoa taarifa sahihi kwa wadau hao na kusema kuwa wameonesha mfano kwa kuwashirikisha wadau kutoka kote nchini pamoja na watu wenye mahitaji maalamu na Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa madini Stanslaus Nyongo amesema kuwa, sekta ya uziduaji imeendelea kukua hasa baada ya maduka maalumu ya madini 28 kujengwa kote nchini jambo lililorahisisha ufanyaji wa biashara pamoja na kuziba mianya ya utoroshaji madini na uuzaji wa madini kwa njia za panya.

Nyongo amesema kuwa tangu kujengwa kwa masoko hayo ambayo huwakutanisha wauzaji na wanunuzi kasi ya ukusaji wa mapato umepanda zaidi ambapo katika soko la Geita makusanyo yamepanda kutoka shilingi milioni 280 hadi 500 na kufikia shilingi bilioni 2 kwa mwezi huku soko la Chunya upatikanaji wa madini umepanda kutoka kilo 20 hadi kufikia kilo150 kwa mwezi.

Awali akitoa salamu kutoka Haki Rasilimali Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi  hiyo Racheal Chagonja amesema kuwa uhusiano wao na wadau katika sekta ya uziduaji unajibu hoja ya kauli mbiu  ya  jukwaa na wiki ya Azaki kwa mwaka huu ambayo imebeba  kauli mbiu ya Ubia kwa Maendeleo, Ushirikiano kama Nguzo ya Maendeleo Nchini Tanzania.

Chagonja amesema kuwa ikiwa ni mara ya tisa tangu waanze kufanya jukwaa hilo, malengo ya kuwakutanisha wadau hao kwa msimu huu ni pamoja na kupashana habari na uelewa wa sekta ya uziduaji, kuchagiza na kuongeza nguvu thabiti ya utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo ihusuyo sekta hiyo.

Amesema kuwa ushirikiano baina ya wadau ndani na nje ya nchi ndio siri ya mafanikio katika sekta ya uziduaji na hiyo ni pamoja na kushauri na kushawishi sekta sera na sheria bora, ukusanyaji na usimamizi mzuri wa mapato yatokanayo na sekta na kukuza sauti za wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za sekta ya uziduaji na kudumisha ushirikiano na ubia kwa maendeleo endelevu nchini.

Jukwaa hilo lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo wabunge, mawaziri,  wanasiasa na wadau wa sekta ya uziduaji umeenda sambamba na kujadili mada mbalimbali zikiwemo Duru za Kisiasa na Uzalendo wa Rasilimali,Ushirikishwaji wa Wazawa na Ufaidi wa Wananchi kwenye Sekta ya Uziduaji nchini na Bajeti na Matumizi ya Mapato ya Sekta ya Uziduaji.
Waziri wa Nishati, Mhe Medard Kalemani akizungumza na washiriki mbalimbali kwenye mkutano wa majadiliano kuhusu Rasimali wa wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) unaondelea jijini Dodoma. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...