Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mikono na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akishuhudiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Yakub Mohamed baada ya
kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Uwanja wa Maadhimisho ya Taifa eneo la Chamwino jijini Dodoma leo Jumatatu Novemba 25, 2019
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa shilingi Bilioni 10
kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la
Kikombo Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli
ametoa fedha hizo leo tarehe 25 Novemba, 2019 baada ya kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa mradi huo na ameagiza milima yote inayozunguka eneo la Makao Makuu ya
Ulinzi wa Taifa lenye ukubwa wa ekari 5,567 imilikiwe na JWTZ kwa ajili ya
shughuli za ulinzi.
Kuhusu madai ya
fidia, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin
Kunambi kuwalipa fidia ya shilingi Bilioni 3 na Milioni 339 wananchi 1,500 wa
Kata ya Kikombo ambao ardhi yao imechukuliwa na JWTZ kwa ajili ya Makao Makuu
ya Ulinzi wa Taifa, kuanzia tarehe 01 Desemba, 2019.
Pamoja na agizo
hilo, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi wa Kikombo kujiepusha na
matapeli wanaowahamasisha kudai fidia wasiyostahili kwa mujibu wa sheria ama
kudai ardhi isiyo yao.
Mhe. Rais Magufuli
pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kujenga kwa kiwango cha
lami kilometa 18 za barabara inayounganisha Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa na
barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli amekubali ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory
Mabeyo aliyeomba Serikali ibebeba jukumu la kulipa deni la takribani shilingi
Trilioni 1 ambalo JWTZ inadaiwa baada ya kujengewa nyumba 6,064 za makazi ya
Askari katika maeneo mbalimbali nchini, badala ya Askari kukatwa posho zao ili
kupata fedha za kulipia deni hilo kama ilivyowekwa katika mkataba wa ujenzi.
“Nakuhakikishia hakuna
kukatwa Askari yeyote, hilo deni litabebwa na Serikali, kabla sijaja hapa
nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu, na nafikiri kesho au
keshokutwa wataanza kulipia hilo deni ambalo limeanza kuiva, tutaanza kulipa
Dola za Marekani zaidi ya Milioni 25 (sawa na shilingi Bilioni 56 na Milioni
948). Mkataba ni kweli ulikosewa, nafikiri ilikuwa ni mwaka 2012/13 lakini
siwezi kukubali makosa ya namna hiyo yakafanyika katika kipindi changu”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli amewapongeza Maafisa na Askari wa JWTZ kwa kazi nzuri ya kulinda
mipaka ya nchi na kushiriki katika operesheni za kulinda amani katika Mataifa
mbalimbali, majukumu ambayo yamelijengea heshima jeshi hilo na Tanzania.
Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
maelekezo yake ya kujengwa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la
Kikombo ambayo yanajengwa na jeshi lenyewe.
Mapema kabla ya
kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi
la ujenzi wa uwanja wa maadhimisho ya kitaifa katika eneo la Chamwino.
Ujenzi wa uwanja
huo utakamilika Januari 2020 ukiwa na uwezo wa kuchukua watu 5,000 kwa gharama
ya shilingi Bilioni 2, na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa ukumbi wa
mikutano, jengo la watu mashuhuri na jengo la kupumzikia watu.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
25 Novemba,
2019
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...