Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka wazazi wote na walezi Mkoani Mara walioozesha watoto wadogo wakiwemo wanafunzi kurudisha ng’ombe walizopokea kama mahari vingenevyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na watafungwa jela.
“baba wa Tanzania hauko juu ya sheria ukimpiga mkeo ni kosa la jinai ukimuozesha mwanao kabla ya umri ni kosa utashughulikiwa tu, lazima tufunge watu sasa hata kama wazazi wamekubaliana tutawagonga kwa mujibu wa sheria”amesema
Sirro ametoa agizo hilo Wilayani Bunda Mkoani mara wakati wa uzinduzi wa madawati ya jinsia Mkoani humo ambapo akiwa Bunda ametoa agizo kwa wazazi wote na walezi kuhakikisha wanawarudisha watoto wote waliowaozesha na warudishe mahari kama wanataka mali wazitafute kwa kufanyakazi na siyo kufanya watoto wa kike mtaji.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi ameendeleza kauli mbiu yake ya polisi kutumia nguvu ya kadri kwa wanaume wote nchini wanaopiga wake zao ili kukomesha vitendo vya ukatili ambavyo amesema Mkoa wa Mara unaongoza kwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Bahati mbaya sana mimi ni IGP na natokea Mkoa huu sasa kuanzia sasa huu ukatili haukubaliki madawati haya ya jinsia yatafanyakazi saa ishirini na nne mwana mama ukipigwa muda wowote wewe nenda kituoni utapata huduma na huyo aliyekupiga atapata huduma anayostahili”ameongeza Sirro
Aidha amewaomba viongozi wa madhehebu ya dini wafanye kazi ya doria ya kiroho kwa waumini wao ili waachane na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wawilaya ya Bunda Bi Lidya Bupilipili akimkaribisha IGP wilayani hapa ameeleza kuwa mbali na ukatili kwa watoto lakini kuna changamoto ya wanafunzi wa kike kutumia uzazi wa mpango wakati bado wanasoma.
Amesema wazazi wamewekeza kwenye mambo ambayo hayana tija badala ya kuwekeza kwenye elimu ndiyo maana mmomonyoko wa maadili ni mkubwa.
“Sijawahi kushuhudia katika kesi nnazopokea ofisini kwangu baba amekatwa mapanga lakini kila siku ni wanawake tu na jambo la kusikitisha kuna baadhi ya viongozi wa vijiji hawalichukulii kwa uzito ukatili huu”amesema mkuu wa wilaya
Mkurugenzi wa jukwaa la Utu wa Mtoto CDF bw Koshuma Mtengeti amewataka wana Mara kuacha vitendo vya unyanyapaa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na wasiogope kwenda kutoa ushahidi wanapohitajika.
Ameongeza kuwa kamati za ulinzi na usalama zinapaswa kuhakikisha sheria zinasimamiwa kikamilifu kuanzia ngazi ya chini.
Mwakilishi Mkaazi Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA) Jacqueline Mahon amesema madawati hayo yameanzishwa ili kuwarahisishia wahanga wa ukatili kupata haki zao.
“mtoto wa mwenzio ni wako, mlinde mwanamke wa yeyote ni mama yako muheshimu, mlinde, msichana yeyote ni sawa na binti yako au dada yako mlinde,muwezeshe atomize ndoto zake.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akikata utepe wakati wa uzinduzi wa jengo la ofisi ya dawati la jinsia wilayani Bunda Mkoani Mara, kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Bunda Lidya Bupilipili na kulia kwake ni mkurugenzi mtendaji wa jukwa la utu wa mtoto Koshuma Mtengeti na Mwakilishi Mkaazi Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA) bi Jacqueline Mahon
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...