Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema inajipanga kujenga vituo vya kuchakata Dhahabu jijini Dodoma na mkoani Geita kwa ajili ya kusafisha madini hayo lengo likiwa ni kuongezea thamani rasilimali hizo.

Akizungumza katika mkutano wa majadiliano ya rasimali katika wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) jijini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Madini Stanislaus Nyongo amesema Dhahabu inayopatikana hivi sasa nchini ni asilimia 80 hivyo  wanahitaji isafishwe kufikia asilimia 99.9 ili Benki Kuu (BOT) iweze kupata fedha kutokana na dhahabu hiyo.

Amesema wamejipanga kuanza kusafisha dhahabu hapa nchini ili kuongeza thamani yake hali iatayosaidia kuongeza pato la taifa na kuhifadhi fedha Benki kuu kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya baadaye.

Mbali na fedha kupelekwa BOT, pia wakianza zoezi hilo watakuwa na uwezo wa kuanza kuuza kwa gramu tofauti tofauti kwa wadau na kuzidi kuongeza pato la taifa kutokana na dhahabu itakayochakatwa.

Mhe Nyongo amesema lengo la mipango mikakati hiyo ni kutaka kuongeza asilimia ya pato litokanalo na madini ambalo awali ilikuwa asilimia 3.5 lakini hivi sasa limefikia asilimia tano kutokana na usimamizi mzuri wa serikali ya awamu ya tano.

" Mbali na mpango huo wa kutaka kuanza kuchakata dhahabu pia tumeanzisha tume ya madini ambayo inaundwa na watu kutoka sekta tofauti ambayo inahusika kutoa leseni za wachimbaji wadogo,  lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kutaka kuondoa ukiritimba iliokuwa ukileta kelele nyingi kwa wachimbaji wadogo," Amesema Naibu Waziri Nyongo.

Amesema mabadiliko hayo ya utoaji leseni hizo yameonyesha matunda mazuri kwa wachimbaji pamoja taifa kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusiana na suala uwajibakaji wa makampuni kwa jamii (CSR) alisema mabadiliko ya sheria hiyo wachimbaji wamekubaliana nayo hali ambayo itasaidia sekta ya madini kuwanuisha watanzania wote.

“Tanzania ni nchi ya tatu kwa uchimbaji wa madini ya dhahabu usimamizi wa rasilimali hizi utaleta faida kubwa,kwa sababu tumesogea hadi asilimia tano kutoka tatu na kuongeza pato la Nchi yetu, hivyo niwaombe Azaki kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano haya," Amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amesema serikali inasisitiza katika matumizi ya gesi kwa wananchi ili kupunguza uharibifu wa mazingira ndani ya nchi.

Dk. Kalemani amesema ni vema wananchi hivi sasa wakajenga mazoea ya kutumia gesi lengo ni kupunguza ukataji wa miti hovyo ambayo inachangia kuharibu mazingira.

“ Mathalani wakazi wa Dar wanatumia takribani magunia 500 ya mkaa kila siku kwa ajili ya kupikia huu ni uharibifu mkubwa wa mazingira nchini, tunapaswa tuanze kutoa elimu na kuudhibiti kabla madhara hayajawa makubwa zaidi, " Amesema Dk Kalemani

Waziri Kalemani amezitaka Asasi za kiraia zilizopo nchini kutoa taarifa sahihi na zitoke kwa wakati ili wananchi waweze kujua nini kinaendelea ikiwemo kupata takwimu sahihi.

Wiki ya maadhimisho ya Asasi za Kiraia nchini inaendelea jijini Dodoma ambapo leo washiriki waligawanywa kwenye makundi mbalimbali kujadili mada zilizokua zikitolewa ikiwemo Sheria, Rasimali na Uongozi ambapo viongozi mbalimbali wa kiserikali na wabunge wamehudhuria.
Waziri wa Nishati, Mhe Medard Kalemani (katikati) na Naibu Waziri wa Madini, Mhe Stanislaus Nyongo (wa Pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Wiki ya Azaki jijini Dodoma leo.
 Waziri wa Nishati, Mhe Medard Kalemani akizungumza na washiriki mbalimbali kwenye mkutano wa majadiliano kuhusu Rasimali wa wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) unaondelea jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Madini, Mhe Stanislaus Nyongo akizungumza kwenye mkutano wa majadiliano ya Rasimali katika wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) unaondelea jijini Dodoma leo.
 Mmoja wa Washiriki wa mdahalo huo wa rasimali kutoka mkoani Geita akiuliza swali kwa Naibu Waziri wa Madini, Mhe Stanislaus Nyongo ambaye alizungumzia suala la kufungua vituo viwili vya kuchakata Dhahabu jijini Dodoma na mkoani Geita.
 Baadhi ya viongozi wa kiserikali na Wabunge ambao wamejitokeza leo kwenye siku ya tatu ya maadhimisho ya wiki ya Azaki jijini Dodoma wakifuatilia majadiliano kuhusu Rasimali kutoka kwa Waziri wa Nishati, Mhe Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Madini, Mhe Stanislaus Nyongo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...