Benki ya Exim Tanzania imeendelea kuwa kinara kwenye Tuzo za Mwajiri Bora (EYA) za mwaka 2019 baada ya kutwaa Tuzo ya mshindi wa jumla ya Mwajili Bora kutoka ndani ya nchini ya mwaka 2019 zilizoandaliwa na kutolewa na Chama cha Waajili Tanzania (ATE) katikati ya wiki hii.
Mbali na tuzo hiyo ilishuhudiwa pia benki hiyo ikiibuka kinara kwenye Tuzo ya mshindi wa jumla ya Ushirikishaji mzuri wa wafanyakazi ya mwaka 2019 sambamba na kutangazwa kuwa miongoni mwa waajili kumi bora hapa nchini kati ya waajili 800 walioshiriki kuwania tuzo hiyo.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam ikipambwa na uwepo wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Mkuu wa Idara wa Rasimali watu wa benki hiyo Bw Frederick Kanga alisema tuzo hiyo ni kiashiria tosha mbele ya jamii kuhusiana na namna ambavyo benki hiyo imewekeza kwenye rasilimali watu, hatua ambayo ina umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo ya benki hiyo.
“Tuzo zote hizo tatu ni heshima kubwa kwetu na ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu ambao tumekuwa tukiufanya kwa rasilimali watu kwenye taasisi yetu katika kuwasaidia waweze kutoa mchango wao kiutendaji katika ubora tunaoutarajia na ikibidi zaidi ya matarajio’’ alibainisha Bw Kanga.
Aliongeza kuwa moja ya vipaumbele vya benki hiyo ni pamoja na kuwaandaa watendaji wake kwa kuwaongezea ujuzi unaowawezesha kuwa mbele ya wakati katika utendaji wao ili kuleta matokeo bora na yenye ubunifu mpya kwa wateja.
“Lengo ni kuifanya taasisi yetu iwe sehemu ambayo mfanyakazi anakuwa bora zaidi, mwenye mabadiliko na mwenye utofauti,’’ alisisitiza.
Katika tuzo za hizo kwa mwaka huu zaidi ya waajili 800 kote nchini walishiriki kuwania tuzo mbalimbali ikilinganishwa na idadi ya waajili 150 tu walioshiriki mwaka jana.
Kwa mujibu wa Bw Kanga benki hiyo imedhamilia kuandaa wafanyakazi wenye ushirikiano katika kuunda timu imara ya pamoja kwa kuandaa mazingira ambayo wafanyakazi hao watajihisi kuwa wanathaminiwa, wanashirikishwa sambamba na kupewa fursa ya kukua na kujiendeleza kitaaluma.
Mkuu wa Idara wa Rasimali watu wa benki ya Exim Tanzania, Bw Frederick Kanga (wa pili kushoto) pamoja na wafanyakazi wengine wa benki hiyo wakifurahia baada ya kutwaa Tuzo ya mshindi wa jumla ya Mwajili Bora kutoka ndani ya nchini ya mwaka 2019 pamoja na Tuzo ya mshindi wa jumla ya Ushirikishaji mzuri wa wafanyakazi ya mwaka 2019 zilizoandaliwa na kutolewa na Chama cha Waajili Tanzania (ATE) jijini Dar es Salaam katikati ya wiki hii.

Muonekano wa Tuzo Ushirikishaji mzuri wa wafanyakazi ya mwaka 2019 ambayo ilikabidhiwa kwa Benki ya Exim Tanzania wakati wa hafla hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...