Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha,  Jijini Dodoma.
 
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. 
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akimkabidhi nakala za vitabu Kaimu 
Kamishna Msaaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya 
Fedha na Mipango Bi. Dionisia Mjema,  baada ya uzinduzi wa Mpango wa 
Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha, 
Jijini Dodoma.
 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. 
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa 
Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo 
za Fedha, kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Benki Kuu (BoT), Kanda ya Kati
 Bw. Richard Wambali, Kaimu
 Kamishna Msaaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya 
Fedha naMipango Bi. Dionisia Mjema, , kutoka kulia ni Mkurugenzi wa 
Uendeshaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT) Bi. Irene Mlola 
na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa TAMISEMI Bw. John Cheyo.
 
Mkurugenzi wa Benki Kuu (BoT), Kanda ya Kati, Bw. Richard Wambali, akizungumza
 jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu 
Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha,  Jijini Dodoma.
 
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. 
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) na wadau wengine wakiangalia 
makala kabla ya uzinduzi wa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria
 na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha, Jijini Dodoma.
 
Baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo 
na  Wawakilishi wa  Wakuu wa Idara na Vitengo wakisikiliza hotuba ya 
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo 
pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu
 Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha jijini Dodoma

Waziri wa Fedha 
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwa katika picha ya 
pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali baada ya kuwakabidhi nakala 
za vitabu alivyozindua kuhusu Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, 
Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha jijini Dodoma.(Picha na Josephine Majura – WFM Dodoma).
………………
Na. Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha 
na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) 
kusimamia Sekta Ndogo ya Fedha kikamilifu ili kukomesha michezo michafu 
inayofanywa na  baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha nchini na 
kusababisha  upotevu wa mali za wananchi.
Ametoa maagizo 
hayo, wakati akizindua Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na 
Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha, uliowakutanisha wadau mbalimbali 
zikiwemo Wizara, Idara, Taasisi na watoa huduma za fedha.
 Alisema kuwa 
kuna taasisi za huduma ndogo za fedha ambazo zinatoa mikopo kwa masharti
 magumu ikiwa ni pamoja na viwango vikubwa vya riba na  tozo ambazo 
huanzia asilimia 3 mpaka asilimia 20 kwa mwezi ambayo ni sawa na 
asilimia 36 mpaka 240 kwa mwaka na pia kukosekana kwa uwazi na masharti 
ya mikataba ya mikopo.
 ‘’Naiagiza Benki
 Kuu ya Tanzania ifuatilie kwa makini mwenendo wa utoaji wa huduma ndogo
 za fedha kupitia mitandao (Digital Microfinance Services) na pia elimu 
kwa umma ya huduma hiyo ya fedha iwe endelevu na itolewe nchi nzima”, 
alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango 
alisema kuwa kwa muda mrefu takribani wananchi milioni 15.4 sawa na 
asilimia 55.3 ya nguvu kazi ya Taifa walikua wanatumia huduma ndogo za 
fedha bila kuwepo kwa Sheria ya kutambua na kulinda haki zao.
Aidha alisema 
kutokuwepo kwa sheria inayosimamia huduma hizo za kifedha kulisababisha 
kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba ya mikopo kwa kutopatikana 
kwa takwimu sahihi za uendeshaji za watoa huduma hizo.
Dkt. Mpango  
alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali ilitunga 
Sheria ya huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake 
zilizotungwa mwaka 2019, ambazo lengo lake ni kuhakikisha watumiaji wa 
huduma hizo wanalindwa kikamilifu.
‘’Sheria hii 
inatambua madaraja manne ya taasisi zinazotoa huduma za fedha ambapo 
Daraja la Kwanza ni zile zinazopokea amana, daraja la pili ni taasisi 
zisizopokea amana, daraja la tatu linahusu vyama vya Ushirika wa Akiba 
na Mikopo (SACCOS) na daraja la nne ni vikundi vya kijamii vya huduma 
ndogo za fedha”, aliongeza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake 
Mkurugenzi wa BoT tawi la Kanda ya Kati, Bw. Richard Wambali, ambaye 
alimwakilisha Gavana wa Benki hiyo Prof. Florens Luoga, amewataka watoa 
huduma ndogo za fedha kuisoma na kuielewa sheria na kanuni zake ili 
wazitekeleze kwa ufanisi.
Pia amewataka 
wadau hao kutumia muda wa miezi 12 iliyotolewa na Sheria kuweka mifumo 
na taratibu za biashara kuendana na matakwa ya Sheria na Kanuni ili 
ifikapo Oktoba 31, 2020, muda mbao umeainishwa kisheria kuwa ni mwisho 
wa kutekeleza masharti hayo wawe wamepata leseni hizo kutoka BoT au kwa 
mamlaka zilizokasimishwa majukumu hayo.
Aidha amewataka 
kuzingatia mazingira na fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa Sheria
 na Kanuni kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi ambao 
hawajafikiwa na sekta rasmi ya fedha.
Naye Mkurugenzi 
wa Uendeshaji wa Mfuko wa kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT), Bi. Irene 
Mlola, alisema kuwa Mfuko huo utaendelea kushirikiana kwa karibu na 
Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwa anaamini nafasi ya  huduma za 
kifedha katika kumkomboa mwananchi kwenye hali ya uchumi na kumsaidia 
kimaendeleo katika kupunguza umasikini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...