Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa
Wilaya ya Sengerema Dkt. Emmanuel Kipole wakiimba wimbo wa Taifa wakati
wa Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Kanda ya Ziwa-Mwanza.
Kulia kwake ni Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof.
Hozen Mayaya na kushoto kwa mkuu wa wilaya ni Kamishna Msaidizi wa
Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Pius Mponzi.

Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini Kanda ya Ziwa wakiwa katika sherehe ya
Mahafali ya 33 yaliyofanyika kwa mara ya saba katika Kituo cha Mafunzo
Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.

Kamishna Msaidizi wa Bajeti Wizara
ya Fedha na Mipango Bw. Pius Mponzi akihutubia wahitimu na wageni
mbalimbali waliohudhuria katika sherehe za Mahafali ya 33 ya Chuo cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini Kanda ya Ziwa, tawi la Mwanza.

Mkuu wa wilaya ya Sengerema Dkt.
Emmanuel Kipole ambaye ni Mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri wa Fedha na
Mipango, akihutubia wahitimu wakati wa Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini cha Kanda ya Ziwa kilichoko Jijini Mwanza

Mkuu wa wilaya ya Sengerema na
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini cha Kanda ya Ziwa, Kituo cha Mwanza yaliyofanyika kwa mara ya
saba katika Kituo hicho, Dkt. Emmanuel Kipole, akimtunuku mmoja wa
wahitimu katika sherehe zilizofanyika jijini Mwanza.

Meza Kuu
ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Sengerema Dkt. Emmanuel Kipole wakiwa
katika picha ya pamoja na wahitimu wa kada mbalimbali wakati wa Mahafali
ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika kwa mara
ya saba katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Mwanza)
……………………
Na Saidina Msangi na Ramadhani Kisimba, WFM, Mwanza
WAZIRI wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekiagiza Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini kuanzisha viwanda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili
kuchochea maendeleo ya vijana na wananchi kwa ujumla.
Maagizo hayo
yametolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza,
Dkt. Emanuel Kipole Dkt. Kipole, aliyemwakilisha kuwa Mgeni Rasmi katika
Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kituo cha
Kanda ya Ziwa, kilichoko mkoani Mwanza.
‘’ Nimefurahishwa
kwa juhudi za Chuo za kuonesha mfano kwa kuanzisha Kiwanda cha Kukamua
Alizeti katika Kijiji cha Pahi, Kata ya Pahi, Wilaya ya Kondoa mkoani
Dodoma na ni matumaini yangu kuwa Chuo kitaendelea kukisimamia kwa
ufanisi kiwanda hiki ili kiweze kuchochea maendeleo kwa vijana na
wananchi wanaozunguka eneo la mradi huo’’ alisema Dkt. Kipole.
Alitoa wito
kwa Chuo hicho kuongeza juhudi za kuanzisha viwanda vingine katika Mikoa
ya Kanda ya Ziwa hususani katika Wilaya za Magu na Bariadi ambako Chuo
kina viwanja kwa ajili ya kujenga miundombinu yake ya kudumu’’
aliongeza Dkt. Kipole
Aidha Dkt.
Kipole alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia
madarakani ilidhamiria na imeendelea na dhamira yake ya kuboresha
mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi zote za elimu hapa
nchini ili kutoa fursa kwa wananchi wengi, hususan wanyonge kupata
elimu bora.
“Ili kufikia
azma hii, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuondoa
ada na michango kwa elimu ya msingi na sekondari na kuongeza ruzuku za
kuendeshea shule za msingi na sekondari zote za umma hapa nchini, ambapo
kwa sasa Serikali inatoa kiasi cha shilingi bilioni 24 kwa mwezi kwa
shule zote za Serikali nchini’ aliongeza Dkt. Kipole
Kwa upande
wake Kamishna Msaidizi wa Idara ya Bajeti ya Serikali kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw.Pius Mponzi ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu
Wizara hiyo, Bw. Doto James, alisema mafunzo yanayotolewa na Chuo cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini yana umuhimu mkubwa kwa nchi hasa
ikizingatiwa kwamba watalaamu wa mipango wanahitajika ili wasaidie
kupanga masuala ya maendeleo katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya
vijiji hadi Taifa.
Awali Mkuu wa
chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Hozen
Mayaya, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa maelekezo, ushauri
na miongozo mbalimbali wanayoitoa kwa Chuo chake ambayo ndiyo imekuwa
chachu ya mafanikio ya Chuo hicho.
Profesa
Mayaya aliwataka wazazi na walezi kuitumia fursa iliyotolewa na Serikali
ya kutoa elimu bure katika ngazi za shule ya msingi na sekondari
kuwaandaa vijana ili wapate elimu ya juu itakayowasaidia kuongeza
maarifa na kujikwamua katika umasikini
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...