Baadhi ya wananchi wakiendelea na kazi ya kushusha mifuko ya saruji kutoka kwenye gari katika bandari ya Kasanga mkoani Rukwa ili ipakizwe kwenye meli ya mizigo kueleka nchini Burundi.
Shehena ya mifuko ya saruji kutoka kiwanda cha Mbeya Cement ikipakiwa katika meli ya Rwegura ya nchini Burundi iliyokuwa katika bandari ya Kasanga mkoani Rukwa.
Mmoja wa madereva anayesafirisha mifuko ya saruhi kutoka mkoani Mbeya hadi Bandari ya Kasanga akizungumza na waandishi habari ambapo ameipongeza Serikali kwa kuijenga kwa lami barabara inayokwenda bandarini hapo kutokea Sumbawanga.
Dereva wa Kampuni ya Triple S ambaye anajihusisha na kusafirisha mizigo akitoa shukrani kwa Rais Dk.John Magufuli kwa kufanikisha ujenzi wa barabara ya lami kutoka Sumbawanga hadi bandari ya Kasanga.
Malori yakiwa yameegeshwa katika barabara inayoelekea bandari ya Kasanga baada ya kushusha mizigo katika bandari hiyo.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Rukwa

HATUA ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli kujenga kwa kiwango cha lami babarabara ya kutoka Sumbawanga hadi Bandari ya Kasanga, imesababisha madereva wanaoendesha magari ya mizigo kwenda katika bandari hiyo kuipongeza Serikali kwa kuijenga barabara hiyo na sasa inapitika vizuri.

Wamesema kwa muda mrefu wameteseka kutokana na ubovu wa barabara hiyo ambayo ilisababisha wawe wanatumia muda mwingi barabarani huku wakikkabiliwa na changamoto za kila aina lakini sasa mambo safi.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya madereva wa malori wanaosafirisha mizigo na hasa saruji kutoka mkoani Mbeya hadi Bandari ya Kasanga wamesema Serikali imefanya kazi nzuri kwa kuamua kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani awali kutoka Mbeya hadi Kasanga walikuwa wanatumia kati ya siku 8 hasi siku 13 lakini hivi sasa baada ya miundombinu ya barabara kuboreshwa wanatumia siku moja tu.

Dereva Yusuph Robert anayefanya kazi ya kusafirisha mizigo kupitia magari ya Kampuni ya AFM Hash amesema siku za nyuma hali ya usafiri ilikuwa mbaya lakini kujengwa kwa barabara ya lami na hasa kutoka Sumbawanga hadi Kasanga kumesaidia kufanya eneo hilo kufika kwa urahisi kwani wanatumia kati ya saa moja na nusu hadi saa mbili lakini zamani walikuwa wanatumia kati ya saa tano hadi nane.

"Zamani tulikuwa tunatoka Mbeya hadi Kasanga tunatumia hadi siku 14 kwani barabara ilikuwa mbaya na tulikuwa tunakwama njiani lakini Serikali ilipoamua kuboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga kwa kiwango cha lami wanatumia siku moja tu , hivyo hata poshoo ambazo tunapewa angalau tunaziona, zamani zilikuwa zinakwisha njiani,"amesema.

Amesema kuimarishwa kwa barabara kwa kujengwa kwa lami na upanuzi wa eneo la bandari ya Kasanga kumefanya hada idadi ya magari kuongezeka na kwa siku moja magari zaidi ya 20 yanashusha mzigo wakati zamani kwa siku zilikuwa zinashusha gari tatu au nne tu.

Kwa upande wake dereva wa Kampuni ya Triple S anayefasafirisha saruji kutoka Kiwanda cha Mbeya Cement hadi Bandari ya Kasanga Ambrose Nsokwe amesema kuimarishwa kwa barabara hiyo kumerahisisha kazi yao ya kusafirisha mizigo na sio karaha tena kwani sasa ni raha tupu.

Amesema kwa sasa baada ya kukamilika kwa barabara, wanatamani Serikali ilete meli kubwa ya mizigo na abiria katika bandari ya Kasanga hasa kwa kuzingatia miundombinu ya bandari hiyo nayo inaboreshwa na kuwa ya kisasa."Tunatamani sasa Serikali ilete meli ambayo itabeba abiria na mizigo, hata sisi madereva tutaongeza kipato kwani tutakuwa tunakuja na mizigo na kisha tunarudi na mizigo, tofauti na sasa tunaleta tu lakini hatuna tunachoondoka nacho."

"Kwa kweli tunamshukuru Rais Magufuli , kazi ambayo anaifanya katika nchi yetu tunaona, kwa mfano hii barabara imetusumbua muda mrefu na hatukutarajia kama itakamilika kwa haraka hivi , lakini kupitia yeye leo hii tunapita kwa raha mustarehe kabisa, lakini kutoka Mbeya hadi bandari ya Kasanga mkoani Rukwa ,"amesema.

Wakati dereva Elias Sadala wa Kampuni ya Triple S amesema kuwa hali ya barabara imeleta matumaini mapya kwao na matarajio yao shughuli za bandari zitaongezeka na Serikali kuingiza mapato."Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu na iendelee na moyo huo huo."

Awali akizungumzia barabara inayotoka Sumbawanga kwenda Kasanga, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama amesema Serikali imeona umuhimu wa bandari hiyo na hivyo kuamua kujenga barabara kwa kiwango cha lami ili kuondoa adha iliyokuwepo awali, hivyo kwa sasa barabara inapita vizuri.

"Kwa kipeee TPA tunaishukuru Serikali yetu kwa kuwezesha kuboresha barabara inayokuja bandarini ambayo ilikuwa haijakamilika lakini sasa imeshawekewa lami kutoka Sumbawanga hadi hapa.Tunatarajia mwishoni mwa Desemba au mapema Januari mwakani itakuwa imekamilika kwa asilimia 100,"amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...