Mkurugenzi Mtendaji wa Banki ya
Maendeleo ya Kilimo (TADB) Japhet Justine akizungumza katika Mkutano
wake na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) kuhusu Mafanikio ya Benki
hiyo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano huo
ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam
leo Disemba 12, 2019.
Mkurugenzi Mtendaji wa Banki ya
Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine akifafanua jambo katika
Mkutano wake na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mafanikio ya
Benki hiyo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano
huo ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es
Salaam leo Disemba 12, 2019.
Picha na Idara ya Habari-MAELEZO
………………..
Na Mwandishi Wetu- MAELEZO
Serikali ya Awamu ya Tano Chini,
Rais Dkt. John Magufuli imejikita katika kuwawezesha wakulima kwani
ilitoa zaidi ya Billioni 300 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania,
(TADB) katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake.
Akielezea mafanikio ya Benki hiyo
katika kipindi cha miaka minne ya Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB
Japhet Justine alisema kuwa Rais Dkt. Magufuli alitoa pesa hiyo, kwa
ajili ya kusaidia sekta hiyo katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa
mikopo kwa Wakulima.
‘’Katika kipindi cha miaka minne
cha utawala wa Rais Dkt. Magufuli alituwezesha kutupa mtaji wa zaidi ya
Sh. Billioni 300, ambapo mpaka Novemba mwaka huu, tumefanikiwa kutoa
kiasi cha Sh. Billioni 148 kwa ajili ya mikopo kwa wakulima’’, alisema
Bw. Justine
Justine alisema wakati wanaanzisha
Benki hiyo mwaka 2016 Rais Magufuli aliwapa Billioni 60 kama mtaji,
lakini waliweza kuizungusha pesa hiyo kwa kutoa mikopo katika vyama
mbalimbali vya wakulima ambapo walifanikiwa kurudisha Sh. Billioni 68
kwa muda mfupi.
Aidh Mkurugenzi huyo alisema, pesa
hiyo ilijikita zaidi katika mpango wa pili wa Maendeleo ya Kilimo,
matumizi bora ya Ardhi na Maji, ambapo mpango huo ulifanikiwa na
kutimiza malengo yaliyotarajiwa.
‘’Pesa hiyo ililenga zaidi katika
mnyororo wa thamani wa mazao , ambapo Sh. Billioni 10 tulipeleka katika
Mifugo, Billioni 1 ilienda ufugaji wa Samaki, Millioni 700 ilienda
kwenye Kuku na Billioni 37 zilienda katika Mazao mbali mbali ya
biashara’’, alisema Japhet.
Mkurugenzi huyo alisema, kutokana
na mpango huo watu Millioni 1.6 wamefanikiwa kutokana na huduma zao
hivyo katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Magufuli Benki
hiyo pamoja na wadau wake wamepata mafanikio makubwa.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema,
mbali na kutoa mikopo kwa wakulima lakini wamekuwa wakiwasaidia
kutafuta masoko hivyo inawarahisishia kuwa na uhakika wa masoko ya
mazao yao.
Mkurugenzi huyo alisema katika
kuimarisha kilimo na kumpa mkulima nyenzo bora, Benki hiyo imekuwa
ikitoa matrekta pamoja na mashine za kuvunia mpunga kwa wakulima.Aidha Mkurugenzi huyo alisema,
mbali na pesa hizo, Benki hiyo ilitoa pesa nyingine kiasi Sh. Billioni
35 mkopo kwa Viwanda 13 vya kuchakata mazao ya Kilimo.
Japhet alitaja baadhi ya viwanda
vilijengwa kutokana na mkopo huo ni pamoja na kiwanda cha Alizeti
kilichopo Kahama, kiwanda cha kuchakata mafuta kilichopo Manyoni na
kiwanda cha kusindika Chikichi kichopo Kigoma.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema TADB
baada ya miaka minne ya mafanikio, inatarajia kuweka nguvu zaidi na
kuyaongezea thamani mazao ya Pamba na Mkonge kwani yalikuwa yakiingiza
pesa nyingi miaka ya nyuma hapa nchini.
‘’Kwakweli TADB tuna nia ya dhati
ya kurudisha thamani ya zao la Pamba na Mkonge, enzi za Mwalimu
Nyerere, mazao haya yalikuwa yakiingiza pesa nyingi hapa nchini, lakini
kadiri miaka ilivyosonga na mazao yalikuwa yakishuka’’, alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Benki
hiyo, inataka kufanya mapinduzi makubwa katika mazao hayo kwani
wanatarajia kufufua viwanda vya kutengenezea nguo, kiwanda cha
kutengeneza magunia.
Japhet amewataka Watanzania waache
kuwaza kilimo cha zamani na badala yake wajiingize kwenye kilimo cha
kisasa, kwani sekta hiyo hivi sasa ni biashara kubwa ambayo inawatoa
watu wengi.
Mkurugenzi huyo alisema, licha ya
kuwa benki hiyo kuwa na mafaniko hayo katika kipindi cha miaka minne,
lakini bado kuna changamoto ya masoko, hivyo wanatarajia kushirikiana na
taasisi zilizo katika mnyororo wa thamani ndani ya Afrika Mashariki na
nchi zilizo kusini mwa Afrika (SADC) katika kutafuta masomo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...