Serikali ya Awamu ya Tano imeuwezesha mkoa wa Mara kujenga Hospitali 4 za Wilaya, Vituo vya Afya 13 kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima amesema mkoa huo umepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma mbalimbali za jamii ikiwemo sekta ya afya kutokana na kutekelezwa kwa ujenzi wa miundombinu ya sekta hiyo kwa ufanisi.

“Mradi wa Hospitali ya Kanda ya Mwalimu Nyerere unaendelea vizuri na utawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa ikiwemo za mifupa na nyingine hali itakayoondoa adha ya wananchi kusafiri hadi Hospitali ya Bugando kufuata huduma hizo” Alisisitiza Malima.

Akifafanua amesema kuwa mkoa huo umepata mafanikio makubwa katika sekta nyingine kama vile elimu kwa kujenga miundombinu ya kisasa yakiwemo madarasa na maabara hali iliyochangia kukua kwa kiwango cha elimu katika mkoa huo ikilinganishwa na miaka iliyotangulia kabla ya uwekezaji huo.

Kwa upande wa sekta ya madini amesema kuwa kuwepo kwa sheria nzuri na taratibu zilizowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano, mkoa huo umezalisha kilo 130 za dhahabu kufikia Septemba mwaka huu hali inayochangia kukuza sekta ya madini na uchumi kwa ujumla.

Akizungumzia mikakati yake ya kukuza kilimo na uvuvi, Mhe. Malima amesema kuwa dhamira ya mkoa huo ni kuona sekta hizo zinatoa mchango stahiki katika uchumi kutokana na hatua zilizochukuliwa katika kokomesha uvuvi haramu katika mkoa huo.

Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa wamejipanga kukuza sekta ya utalii katika mkoa huo ili kuongeza pato la mkoa huo hatua itakayowasaidia kuwainua wananchi kiuchumi na Taifa kwa ujumla.

Kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...