SERIKALI
haitaingilia Vyama vya Ushirika nchini vinavyofuata sheria na taratibu
katika uendeshaji wake, isipokuwa pale panapojitokeza ukiukwaji wa
Misingi ya Ushirika na panapokuwa na ubadhilifu wa mali za Wanaushirika
unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo.
Angalizo
hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania
(TCDC), Dkt. Titus Kamani pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey
Mwanri, Alhamis, Desemba 19, 2019 mjini Tabora, walipokuwa wakiongea
kwenye Kikao cha Wadau wa Ushirika mkoa wa Tabora kilichofanyika katika
ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
“Serikali
haiwezi kuingilia Vyama vya Ushirika vinavyofuata sheria na taratibu
katika uendeshaji wake isipokuwa panapojitokeza ukiukwaji wa Misingi ya
Ushirika na panapokuwa na ubadhilifu na wizi wa mali za Wanaushirika
unaofanywa na baadhi ya viongozi, hatutanyamaza, tutachukua hatua,”
amesema Dkt. Kamani.
Dkt.
Kamani amewahimiza Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuwa waaminifu na
waadilifu katika kusimamia mali za wanaushirika walizokabidhiwa na
wanachama wenzao kuzisimamia kwa niaba yao na kuweza kupata faida ya
pamoja itayowawezesha kuboresha maisha yao.
Aidha,
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Aggrey Mwanri, amesema Serikali mkoani
humo haitasita kuwachulia hatua kali za kisheria viongozi wa vyama vya
ushirika wanaokiuka sheria na taratibu za uendeshaji wa vyama ushirika
kwa kisingizio kuwa ushirika ni mali yao na Serikali haiwezi
kuwaingilia.
“Ushirika
siyo kichaka cha baadhi ya watu kuiba; hatutaruhusu, tutawakamata
wakati wanaiba, hatutasubiri na tutawatia ndani. Wapo viongozi wa
ushirika wazuri tu, anaweza kuwa Mwenyekiti au Katibu Meneja, hao
watakuwa marafiki wa Serikali na hawatasumbuliwa,” amesema Mkuu wa Mkoa
wa Tabora.
Akizungumza
katika Kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora
ambaye ni pia ni Mwanaushirika, Hassan Wakasuvi, amewataka viongozi wa
vyama vya ushirika katika maeneo yanayolima zao la Tumbaku wasimamie
masharti wanayojiwekea ili kuondokana na adha inayojitokeza wakati msimu
wa kuuza Tumbaku.
.
“Viongozi
wa vyama vya ushirika simamieni masharti mnayojiwekea, ili kuinua
thamani ya zao la Tumbaku na kuondokana na bei za aina mbili, ikiwemo
bei ya makinikia ambayo inakuwa ni ya kinyonyaji kwa wakulima,” amesema
Wakasuvi.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu, akizungumza katika Kikao hicho, amewataka Wanaushirika kote
nchini kuchangamkia Bima ya Afya inayotolewa mahsusi kwa wanachama wa
Vyama vya Ushirika – Ushika Afya.
“Viongozi
wa Vyama vya Ushirika wahimizeni Wanachama wenu kujiunga na Bima ya
Afya inayotolewa kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika – Ushika Afya, kwa
kuwa ni muhimu kwa afya na maendeleo ya familia zao; na inatolewa kwa
gharama nafuu ya Shilingi 76,800/ (mtu mzima) na Shilingi 50,400/
(mtoto) kwa mwaka,” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza kwenye Kikao cha Wadau wa Ushirika mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri akizingumza kwenye Kikao cha Wadau wa Ushirika mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani akizungumza kwenye Kikao cha Wadau wa Ushirika mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...