Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imewataka wakuu wa Shule nchini kuwahimiza na kuwajenga wanafunzi kwenye shule zao kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mashindano ya Insha yanayoshirikisha wanafunzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na ile ya kusini mwa Afrika SADC.
Walimu hao wametakiwa kutilia mkazo ushiriki wa wanafunzi hao kwani unachangia kuwajenga kitaaluma, kuwaongezea uwezo wa kufikiri lakini pia kuwapatia kipato kutokana na zawadi zinazotolewa.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe William Ole Nasha wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti washindi wa kitaifa wa shindano la uandishi wa insha kwa Jumuiya SADC na EAC, tukio lililoenda sambamba na ugawaji wa zawadi kwa washindi hao.
" Ili tupate washindi wengi katika mashindano haya ni lazima wakuu wa shule za Sekondari wahakikishe wanawahamasisha wanafunzi wengi kushiriki katika mashindano haya kwa sababu yanawaongezea fursa washiriki na kuwasaidia kujiamini Sana.
"Mashindano haya yanasaidia kuwajengea wanafunzi wetu uwezo wa uandishi, udadisi na kuwa wepesi kufanya tafiti pia mashindano haya yanasaidia kuwajengea uzalendo pindi wanapokuwa wanawakilisha Taifa" Amesema Ole Nasha.
Amewataka wanafunzi walioshiriki na kushinda kuwa mabalozi wazuri kwa kuhamasisha wenzao nao kuhakikisha wanashiriki mashindano hayo ili kuwa na wawakilishi wengi zaidi katika mashindano hayo na kuwapongeza kwa kushiriki na hatimaye kuibuka washindi wa mashindano hayo.
Amesema mashindano hayo yalianzishwa ikiwa ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Jumuiya ya SADC na EAC kujenga uelewa kwa wanafunzi juu kazi na mipango ya Jumuiya hizo kwa wanafunzi kushiriki katika mashindano hayo ya kuandika insha yenye maada zinazoshabihiana na Jumuiya hizo.
Kwa upande wake mratibu wa tukio hilo la uandishi wa insha Sylvia Chinguwile, amesema mada zinazoshindaniwa huzingatia makubaliano ya wakuu wa Nchi na baadaye Nchi wanachama kuwajibika kutangaza na kubainisha vigezo vya washiriki.
Amesema baada ya kupita katika michakato huo huwasilishwa wizarani na kuteuliwa insha bora katika ngazi ya shule na kusahihishwa na jopo la wataalamu na zile za EAC husimamiwa na balaza la mitihani, na insha tatu bora za SADC hupelekwa Botswana ili kuidhinishwa na mataifa Nchi wanachama, wakati insha tano bora huwasilishwa Arusha Makao makuu ya Jumuiya kushindanishwa na Mataifa mengine.
Amesema kwa upande wa EAC mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza ni Vanessa Lema, kutoka Longido Sekondari kidato Cha sita, wakati wa pili ni Thomas Kalisti, Kibasila Sekondari Dar as saalam kidato Cha Tatu, huku kwa ujumla wake Wakiwa 13.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Elimu nchini Augusta Lupokela ameipongeza wizara ya elimu kwa kuweza kuwasimamia mwanzo hadi mwisho wa mashindano hayo amesema kupitia mashindano hayo wameweza kujipambanua kuwa bado elimu yetu ipo katika Hali nzuri ukilinganisha wanavyoiongelea watu wengine.
Nae mwanafunzi ambaye alifanya vizuri katika uandishi wa Insha kwa mada zote Julieth Mpuya, kutoka Kilangalanga Sekondari kidato Cha kwanza, amesema kilichompelekea kufanya vizuri ni ujasiri, kujituma na kufuatilia mada na kuamini kuwa anaweza na hatimaye kufanya vizuri.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe William Ole Nasha akimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mashindano ya Insha kwa Nchi wanachama wa Jumuiya za SADC na EAC leo jijini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe William Ole Nasha
akizungumza na walimu, wazazi na wanafunzi katika hafla ya utoaji tuzo
za Insha jijini Dodoma leo.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe William Ole Nasha
akizungumza na Walimu, Wanafunzi na Wazazi katika hafla ya utoaji tuzo
kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mashindano ya Insha kwa Nchi
wanachama wa SADC na EAC. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe William Ole Nasha akiwa
katika picha ya pamoja na maofisa kutoka Jumuiya za SADC, EAC na Wizara
pamoja na wanafunzi walioshinda kwenye mashindano ya Insha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...