Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( Kulia) na Naibu Waziri wa Nishati
wa Namibia, Kornelia Shilunga( kushoto), wakiwa katika picha ya
pamoja na ujumbe kutoka Namibia na Watendaji wakuu wa Wizara ya
Nishati baada ya majadiliano ya pamoja kuhusu Kituo cha Nishati Jadidifu
na matumizi bora ya Nishati cha nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SACREEE)
katika Ofisi ya Wizara ya Nishati Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akiongoza majadiliano ya
pamoja na Ujumbe kutoka Namibia na Watendaji wakuu wa
Wizara ya Nishati kuhusu Kituo cha Nishati Jadidifu na matumizi
bora ya Nishati cha nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SACREEE) katika Ofisi
ya Wizara ya Nishati Dodoma.
Na Zuena Msuya, Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Naibu Waziri wa Nishati wa
Namibia, Kornelia Shilunga pamoja na ujumbe wake, wamekutana na
kujadili kwa pamoja kuhusu Kituo cha Nishati Jadidifu na matumizi bora ya
Nishati cha nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SACREEE).
Mgalu alikutana na ujumbe huo, Desemba 2, 2019, uliofika katika Ofisi za
Wizara zilizopo jijini Dodoma, kwa lengo la kuisisitiza Tanzania kuweka
saini katika mkataba wa makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa na Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika( SADC) juu ya
kuanzishwa kwa SACREEE.
Katika mazungumzo hayo, Mgalu aliueleza ujumbe huo kuwa mpaka sasa
Tanzania bado haijasaini Mkataba wa Makubaliano ya pamoja ya
utekelezaji wa kituo hicho hadi pale uamuzi wa kuanzishwa kwa kituo hicho
utakapoidhinishwa na Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika( SADC).
Aidha, Mgalu alisema baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria juu ya
uanzishwaji wa SACREEE, Tanzania iko tayari kusaini mkataba kwa ajili
kuwezesha kituo hicho ambacho Makao yake Makuu yako nchini Namibia.
Halikadhalika, Mgalu alisema kuwa Tanzania na Namibia ni nchi
wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC), ni
dhahiri Kwamba nchi hizo zitakuwa zikishirikiana kwa namna moja ama
nyingine katika masuala mengine mbalimbali kupitia umoja huo.
Sambamba na hilo alisema nchi hizo pia zinaweza kushirikiana kwa
kuuziana umeme kupitia njia ya kusafirisha umeme wa kV400 inayojengwa
kwa ajili ya kuunganisha gridi za Tanzania na Zambia(TAZA) kwakuwa nchi
hizo ni wanachama wa Mtandao wa Southern Africa Power Pool
(SAPP)ambao uko chini ya SADC.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Namibia, Shilunga aliishauri kwamba
Tanzania isaini mkatba huo ili SARCEEE isonge mbele kwa manufaa nchi
wanachama pia alisema Namibia inaendelea kuhamasisha nchi zilizobaki
zisaini mkataba huo.
Tayari nchi 8 kati ya 16 zimekwisha kusaini Mkataba wa makubaliano ya
pamoja ya nchi wanachama wa Jumuiaya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
ya kuanzishwa kwa SACREEE ambayo ilizinduliwa mjini Windhoek nchini
Namibia, Oktoba, 2018 na kuhudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi
wanachama wa SADC na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa na Kikanda
zinazohusika na sekta ya nishati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...