Na Said Mwishehe, Michuzi Globu -Mwanzania

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) umeamua kutaja mambo matano muhimu ambayo kwa sasa wanajivunia nayo katika utendaji wao wa kazi katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani.

Akizungumza jijini Mwanza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema jambo la kwanza ambalo wanajivunia nalo ni kukua kwa uwezo wa bandari zilizopo Bahari Kuu na Maziwa Makuu yote nchini.

“Katika kupima uwezo wa bandari ni pamoja na kuangalia tani za shehena ambazo tunazihudumia ukilinganisha na wengine au ukijilinganisha na kipindi kilichopita.

"Hili swali la nini tunajivunia, kwanza tunamshukuru Rais Dk.John Magufuli ambaye kwa nia yake ya dhati amedhamiria kufufua na kuimarisha bandari kama sehemu muhimu kwa uchumi wa nchi. Ni swali la kawaida katika misingi ya menejimenti , sababu unajivunia nini maana yake ni matokeo ya kufanikisha utekelezaji kwa kile ulichopanga.

"Kama ukilima shamba unatarajia kuvuna na utakuwa na malengo ya magunia kiasi gani au tani ngapi kwa heka, sasa ukizipata zile ndiyo unasema najivunia kwa kupata kile nilichoanga au zaidi,"amesema.
Amesema TPA imekuwa ikishirikiana na taasisi nyingine ili kufufua meli na miudombinu ya bandari nchini na kazi hiyo imekuwa ikifanyika kwa mafaniko makubwa.

“Kwetu sisi tukiona kuna meli nyingi tunapata usingizi lakini meli zikikosekana hata usingizi hauji kabisa na unaamka usiku kuanza kuuliza kwa mameneja , maana yake kila mahali kukiwa hivyo, Bandari ya Dar es Salaam imeongeza meli.

"Tunazihasebu meli kwa wingi wake na ukubwa wake kwa maana ya uwezo, unaiangalia Tanga, Mtwara, meli zinavyoongezeka, ndivyo usingizi unavyopatikana, meli zikipungua ndivyo unaihirisha kulala na kuangalia unazitafutaje, hivyo tunajivunia ongezeko la meli,"amesema Mhandisi Kakoko.

Ameongeza kuwa wakati wanaanza kazi kwa maana ya menejiment na bodi mwaka 2016 , meli zilikuwa chache sana na hiyo ilianza mwaka 2014/2015.Ndio ambacho mzigo wa shehena ilipungua, hivyo hicho ni kipimo cha kwanza.

“Nchi zote tulishusha mzigo na ndio kipindi tulipingwa na hao mnaosema wanasambaza propaganda kuwa Bandari ya Dar es Salaam imechoka na haina tofauti na bibi kizee ambaye hata akipaka wanja hauwezi kutoka.

"Ni kipindi ambacho wengi wenu mlipiga picha magofu ya bandari ambayo yalikuwa yamebomolewa kwa ajili ya kujenga miundombinu,"amesema Mhandisi Kakoko na kuongeza hivyo wanajivunia hatua waliyofikia na mpango uliopo ni kuongeza shehena ambapo haipungui tani milioni moja kwa mwaka.

Na kwamba awali walikuwa wanahudumia tani milioni 14.7 kwa mwaka lakini kutokana na kuimarishwa kwa huduma bandarini wakafanikiwa kufikia tani milioni 17.8 na sasa wanazungumzia tani milioni 18.1.

Pia anasema wanajivunia kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kwani kwa sasa mapato yamepanda ikilinganisha na huko nyuma ambapo kwenye upande wa shehena walikuwa na ongezeko la asilimia 6 hadi 7 na sasa wamekwenda asilimia tisa hadi 11 mwaka.

“Kwenye fedha tunakipimo hicho hicho, tumekuwa na fedha ingawa sina tamkwimu hapa,lakini tulikuwa tunakusanya Sh.bilioni 300 na imekuwa ikipanda mwezi hadi mwezi. Tulitoka Sh.bilioni 300, tukaenda Shilingi bilioni 320, baadae Sh.bilioni 360,"amesema.

Ameongeza kuwa hivyo wamekuwa na ongezeko kati ya Sh. bilioni 10 kila mwaka hadi Sh.bilioni 20 na kusisitiza kuwa wakati menejmenti na bodi walipokuwa wanaingia walikuwa wanafikisha Sh. bilioni 608 , lakini sasa wamepanda na kufikia Sh.bilioni 940 na mkakati wao ni kufikia makusanyo ya Sh.trilioni 1.4.

Wakati jambo jingine ambalo wanajivunia kayika kupindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwa na uwezo wa kutoa gawio la Sh. bilioni 480 na kwamba hivi sasa wamekuwa wakipata inayozidi Sh.bilioni 240.

“Hivyo kigezo cha pili ni mapato kwa njia ya fedha ambayo unaweza kuyaona yana uwiano na shehena tunayoihudumia , tunataka kujihakikishia kuendelea , tumejilinganisha na wenzetu market share yetu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 26 wakati bandari ziko nyingi tu tena kubwa ,unaweza kusema ziko bandari kama sita au saba. Tukiziunga bandari zote hizo sisi bado tunaongoza kwa asilimia hizo.

“Kwa hiyo ni zaidi ya robo kwa mfano sasa hivi kuna tani zaidi ya milioni 60 hadi milioni 70 ambazo ziko kwenye bara hili (Afrika)ambazo zinaingia na kutoka , sisi kama tunahiyo basi tuna Market Share kubwa. Tunamshukuru Rais, kwani tunapozungumzia viwanda vya ndani kwetu ni faida
“Miradi inayoendelea nchini kwetu inatuinua sana , kwa mfano mradi wa reli kuna vyuma ambavyo vinaingia nchini, na kupitia vyuma hivyo na mitambo mingine tunapata fedha, hata mradi wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere nako tutapata fedha kupitia mradi huo kwani malighafi za ujenzi zitapita kwenye bandari yetu,” alisema.

Pia Mhandisi Kakoko amesema wanajivunia vigezo vya uzalishaji , kwa maana ya muda unaotumika katika kutoa huduma kuanzia malori yanapoingia , yanavyopakia shehena, muda gani wa kupakua na kupakia mizigo ya shehena.

"Muda gani meli inakaa kwenye gati. Tangu unapofunga kamba ya kwanza , unaanza kuhudumia meli hadi inapofungua kamba ya mwisho inapoanza kuondoka , kwasababu meli kwa kawaida inafungwa na kamba nne au tano
“Sasa tunaanza kuhesabu tangu ilipofungwa kamba ya kwanza maana ile ni huduma , ukichelewa kufunga kamba ni kupoteza muda, kama muda kupakia na kushusha shehena inahesabiwa.

"Hivyo kufungua kamba ya mwisho na meli kuanza kutembea ile ni muhimu sana , inatakiwa muda uwe mdogo hata kama mzigo ni mkubwa, kwani inapima uwezo wako wa kutoa huduma, hivyo katika eneo hilo tumefanikiwa,” amesema.

Wakati huo huo amesema uhusiano mzuri kati yao na wadau wengine ni jambo muhimu kwao na hilo wanajivunia nalo sana kwa sasa."Mahusiano mazuri na wadau wengine kwetu ni muhimu na hayawezi hayapimiki kwa tani,"amesema.

Alisema suala la uhusiano mwema kwa jamii kupitia biashara hurudisha wateja, kwani hakuna mteja anayekubali kuleta vitu vyake mahali penye kelele au katika eneo ambalo muda wowote inaweza kutokea vita na mzigo ukapotea.

Pia amesema amani iliyopo nchini ni jambo la aseti ambayo watalaamu hawajaweza kubainisha thamani ya amani ni shilingi trilioni ngapi lakini hiyo kwa Tanzania imekuwa fursa nyingi ya bandari zake kuwa sehemu salama ukilinganisha na nchi nyingine
 Ukarabati wa MV. Victoria ukiendelea katika Ziwa  Victoria ukiwa ni mkakati wa kuimarisha huduma ya usafiri wa meli katika ziwa hilo
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini Mhandisi Deusdedit Kakoko akifafanua jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Mwanza

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...