*Asema wanaomiliki bandari zao binafsi nao lazima watambuliwe kisheria
Na Said Mwishehe, Michuzi Globu -Mwanza
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema pamoja na mikakati inayoendelea kuimarisha sekta ya bandari, moja ya changamoto iliyopo ni wingi wa utitiri wa bandari bubu ambapo kwa sasa zimefikia 601 huku akitaja hatua za kuhakikisha bandari hizo zote zinakuwa sio bubu tena kwa kuchkua hatua kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza TPA imeiona changamoto hiyo, hivyo imedhamiria kuwa muda sio mrefu lazima ziwe zimepatiwa majibu yake ili nazo zianze kuingiza mapato kwa Serikali kutokana na huduma zinazoendelea kwenye bandari hizo kokote ziliko iwe katika maziwa makuu au bahari ya Hindi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Mwanza , Mhandisi Kakoko ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio lukuki yaliyopatikana ndani ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli.
Ambapo amesema licha kuwa na mafanikio makubwa ambayo wanajivunia, bado ni wajibu wao kuendelea kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto ikiwemo hiyo ya uwepo wa bandari bubu.
"Awali kulikuwa na bandari bubu 437 lakini baada ya muda kidogo tukabaini zimeongezeka tena hadi kufikia bandari bubu 601.Hivyo mkakati wetu ni kuhakikisha hakuna bandari bubu hata moja ndani ya nchi yetu, na huo ububu hautakuwepo bali ziwe na ndimi ya kutoa fedha.
"Kuwa na bandari bubu ni ngumu kujua kitu gani kinasafirishwa kupitia bandari hizo , hivyo kiusalama nayo sio jambo nzuri, lazima tufahamu kila kinachoingia na kutoka ndani ya bahari zetu.Tutaweka utaratibu maalumu wa kuzitambua bandari zote bubu na kimsingi tayari tunazifahamu na muda mchache ujao zote zitakuwa zinatambuliwa na TPA.
Amesisitiza katika kuhakikisha bandari bubu zote zinatambuliwa na TPA, pia watatumia utaratibu wa kushirikisha viongozi wa maeneo husika ambao nao watakuwa sehemu ya wadau muhimu,"amesema Mhandisi Kakoko.
Amesema kuwa kama uwepo wa bandari bubu unatokana na gharama kubwa katika bandari zilizopo, hilo ni jambo ambalo linazungumzika kwani TPA haipo kwa ajili ya kutaka faida kubwa zaidi ya kutoa huduma kwa gharama nafuu.
"Ukweli tumejipanga kuzidhibiti zote, kama kuna sababu ya kuwepo kwa bandari hizo tutata kufahamu na kutafuta jibu la pamoja.Kama kwenye bandari zetu gharama ni kubwa, ni jambo ambalo linazungumzika, tuko tayari kupunguza na hatimaye sote tuwe tunatumia bandari zinazotambuliwa na TPA.
"Tunatambua pia kuna baadhi ya watu binafsi wanamiliki bandari zao na kuendelea na shughuli za utoaji wa huduma kwa wananchi.Nako tumeanza mazungumzo na baadhi yao ili hatimaye nao tujue wanachokifanya na huduma ambazo wanazitoa na hapo tutapa kodi yetu na hivyo Serikali kuingiza fedha.Hatuna nia mbaya na wanaomiliki bandari lakini lazima tuwatambue na tuepeane maelekezo ya nini ambacho tunataka kuona kinaendelea kwenye bandari hizo,"amesema Mhandisi Kakoko.
Kuhusu mikakati iliyopo katika kuboresha miundombinu katika bandari za maziwa makuu zikiwemo bandari za Ziwa Victoria, Mhandisi Kakoko amesema TPA kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Kampuni ya Huduma za Meli na TRC wameendelea na mkakati wa kuboresha bandari hizo.
"Katika Ziwa Victoria mikoa yote ambayo ziwa hili limepita, kuna bandari na zile ambazo zilikuwa zimeanza kulega lega na kuchoka kimiundombinu,sasa matengenezo yanafanyika , Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi kujenga miundombinu ya bandari hizo na hakika mambo yanakwenda vizuri,"amesema Mhandisi Kakoko.
Hata hivyo amesema kwa kutambua umuhimu wa bandari kama kichocheo muhimu cha maendeleo ya wananchi wa kanda ya Ziwa, TPA imeweka mkakati wa kuhakikisha kila mkoa uliopo kwenye ziwa hilo au kila wilaya kunakuwa na bandari.
"Kila Mkoa utakuwa ba bandari kubwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi, na hivyo hivyo kwa kila wilaya nako kutakuwa na bandari na huo ni mkakati ambao tutaunza awamu ya pili ya malengo yetu."
Akizungumzia bandari ambazo kwa kanda ya Ziwa ni maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo ,ameitaja bandari ya Kemondo, Bandari ya Mwanza Kaskazini na Bandari ya Musoma ambazo hizo zilikuwa na mfumo wa reli ambazo zinakwenda moja kwa moja kwenye meli kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji mzigo, hivyo mojawapo ya kazi inayoendelea sasa ni kufufua miundombinu katika bandari hizo na kazi inakwenda vizuri.
Amesema kwa kutumia usafiri wa meli na reli, gharama za usafirishaji ziko chini ikilinganishwa na kusafirisha mizigo kwa njia usafiri wa malori hasa kwa kuzingatia kusafirisha kwa barabara inapofika kuanzia kilometa 500 gharama inakuwa kubwa lakini wa kutumia reli na baadae meli unasafirisha mzigo mkubwa lakini kwa gharama nafuu.
Wakati huo huo, Mhandisi Kakoko amesema kauli ya Rais ya kutaka kurudishwa kwa Shirika la Meli ya Taifa, wao wameipokea kwa mikono miwili na ilikuwa ni kilio chao cha muda mrefu, hatimaye kimesikika kwani wanaamini shirika hilo litakaporejea idadi ya meli zitaongezeka na wao bandari wanachotamani kuona ni uwepo wa meli nyingi nchini.
Ametoa mfano nchi ya Ethiopia ndio yenye meli nyingi kwa kuwa na meli 96 lakini hawana ukanda wa bahari, wakati Tanzania yenye kilometa zaidi ya 1, 440 za bahari kuna meli 14 tu na kati ya hizo nne ndio zinatoa huduma.Hivyo lazima kuwepo na meli za kutosha na hasa kwa kutambua Tanzania inaweza kutumia eneo la maji tu kujiendesha kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini Mhandisi Deusdedit Kakoko akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mambo ambayo mamlaka hiyo inajivunia katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli
wananchi wakiendelea na shughuli zao katika Bandari ya Musoma mkoani Mara ambapo kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ni kwamba bandari hiyo ni miongoni mwa bandari zilizopo katika Ziwa Victoria ambazo zipo katika mkakati wa kuboreshwa kiundombinu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...