Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli
Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akizungumza katika Mkutano wake na
Waandishi wa Habari(hawapo pichani) kuhusu Mafanikio ya Shirika hilo
kwenye miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano huo ulifanyika
katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam leo
Disemba 12, 2019.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli
Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akifafanua jambo katika Mkutano wake
na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mafanikio ya Shirika hilo
kwenye miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano huo ulifanyika
katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam leo
Disemba 12, 2019.Picha na Idara ya Habari-MAELEZO
………………
Eric Msuya,MAELEZO
Shirika la Reli Tanzania (TRC)
limefanya mageuzi makubwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa wakati
akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu
mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Kadogosa alisema kuwa pamoja na
mageuzi yanayoendelea katika sekta mbalimbali hapa nchini, Serikali ya
Awamu ya Tano imefanikiwa kufufua miundombinu ya reli katika maeneo
mbalimbali ikiwemo njia ya treni ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi
Kilimanjaro ambayo kwa sasa inasafiri mara tano kwa wiki.
“Kutokana na maombi ya wananchi
wengi tumeamua kwamba kuanzia Desemba 16 mwaka huu safari ya treni
kutoka Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro itakuwa ni mara tano kwa wiki”
alisema Kadogosa.
Kadogosa alieleza kuwa TRC
imefanikiwa kuongeza idadi ya mizigo ambapo zaidi ya tani 1,456,537
zimeweza kusafirishwa katika reli ya kati (Dar es Salaam, Mwanza na
Kigoma) na kwa upande wa abiria treni za mikoani wameongezeka kutoka
411,172 mwaka 2014/15 hadi 578,439 mwaka 2018/19.
Sambamba na hilo, TRC imeweza
kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 17.4 mwaka 2014/15 hadi bilioni
30 mwaka 2018/19 kwa treni za mizigo, kutoka bilioni 8.3 hadi bilioni
10.7 kwa treni za abiria wa mikoani na kutoka milioni 316.6 hadi bilioni
1.96 kwa treni za mjini.
Aidha TRC inajivunia mageuzi
makubwa yanayofanywa na Serikali katika sekta ya reli kwa kutekeleza
mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR)
wenye gharama ya shilingi trilioni 7.5
“Mradi wa SGR katika mindombinu ya
reli hapa nchini ni mradi mkubwa sana ambao utamwezesha mfanyabiashara
au abiria wa kawaida kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi mwanza kwa saa 9
na treni hii itakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 160 kwa
saa hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi hapa Tanzania” alieleza Kadogosa.
Alisema kuwa mpaka sasa ujenzi wa
reli hiyo ya kisasa (SGR) yenye mtandao usiopungua kilometa 2,561
umefikia asilimia 70 ambapo reli hiyo itaunganisha mikoa ya Dar es
Salaam, Mwanza, Kigoma na Katavi pamoja na nchi zisizokuwa na bandari
(Rwanda, Burundi na DRC Congo).
Pia Kadogosa aliongeza kuwa TRC
inatekeleza mradi wa uboreshaji wa reli ya kati- TIRP wenye lengo la
kuongeza ubora na uimara wa njia ya reli kutoka Dar hadi Isaka ili
kuweza kubeba mizigo kufikia tani 18.5 na mwendokasi wa kilometa 70 kwa
saa.
Mradi huo wa TIRP umezalisha ajira
kwa vijana wa kitanzania zaidi ya 1,600 pamoja na kuwanufaisha
wafanyabiashara mbalimbali na watoa huduma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...