Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na baadhi ya wavuvi katika soko la
samaki manispaa ya Mtwara (hawapo pichani) wakati wa kuhitimisha ziara
yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mtwara

Baadhi ya wavuvi katika soko la
samaki la Manispaa ya Mtwara wakimsikiliza Naibu waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akijibu hoja mbalimbali wakati akihitimisha
ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mtwara.

Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega akijibu hoja mbalimbali za wavuvi katika soko la
samaki la Manispaa ya Mtwara wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya
siku mbili Mkoani Mtwara
………………..
Serikali imesema
itaendelea kufanya marekebisho ya tozo, kanuni na sheria mbalimbali za
uvuvi nchini ili wadau wa uvuvi waweze kufanya shughuli zao kwa tija
zaidi na kuwataka maafisa uvuvi kuendelea kusimamia sheria zilizopo
pamoja na wavuvi kutii sheria hizo.
Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo jana (13.12.2019)
Mkoani Mtwara wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili
mkoani humo kwa kujionea shughuli mbalimbali za uvuvi na kuzungumza na
wavuvi katika baadhi ya vijiji vya Halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya
Mtwara ambapo amesema ziara yake imelenga kukusanya maoni kutoka kwa
wadau hao.
Akizungumza na
wadau wa uvuvi katika soko la samaki la Manispaa ya Mtwara, Mhe. Ulega
amewataka maafisa uvuvi nchini kuwa na mahusiano mazuri na wavuvi pamoja
na kuwasaidia wavuvi kutafsiri sheria mbalimbali ili wajiepushe na
matumizi ya zana za uvuvi zisizotakiwa kisheria ambazo zinaweza
kuwasababishia kutiwa hatiani kwa kukiuka sheria za nchi.
Aidha Mhe. Ulega
amewataka maafisa uvuvi nchini kutojihusha na vitendo vya rushwa na
kuwataka wavuvi wanaokutwa na hatia ya kujihusisha na kufanya shughuli
zao kinyume na sheria ikiwemo uvuvi haramu kulipa faini wanayotozwa kwa
kutumia utaratibu wa serikali uliowekwa.
Nao baadhi ya
wavuvi wa soko la samaki la Manispaa ya Mtwara waliopata nafasi ya
kuuliza maswali na kutoa maoni yao kwa Naibu Waziri Ulega wameiomba
serikali ya awamu ya tano kuwaboreshea zaidi mazingira ya kufanya
shughuli zao kwa kuondoa kero mbalimbali wanazokabiliana nazo ili waweze
kufanya shughuli zao ziwe na tija zaidi kwa kujiongezea mapato na
kulipa kodi ya serikali.
Wakati wa
kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mtwara Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametembelea pia Kijiji cha
Msanga Mkuu kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na
kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho wanaojihusha na shughuli za uvuvi
na kuwataka kufanya kazi kwa kufuata sheria huku akiwataka pia maafisa
uvuvi wakishirikiana na vyombo vya dola kutotumia nguvu kwa mtuhumiwa wa
matumizi ya zana za uvuvi zisizotakiwa kisheria ambaye anatii sheria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...