Tanzania ni moja kati ya nchi nyingi ulimwenguni zilizoridhia kutekeleza Ajenda 2030 inayohusu Malengo ya Maendeleo Endelevu hususan lengo Namba 4 linalohusu elimu. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu (2016/17-2020/21), Tanzania pamoja na mambo mengine inatekeleza lengo Namba 4 ambalo linalenga kutoa fursa ya elimumsingi jumuishi, kwa usawa na yenye ubora kwa wote na bila malipo ili kuwajengea wanafunzi maarifa, ujuzi na kuwaandaa na masomo ya juu.
Ili kutekeleza hili, Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ilipoingia madarakani mwaka 2015, ilitangaza rasmi dhamira yake ya kutoa elimumsingi bila malipo kuanzia darasa la awali hadi sekondari kuanzia mwaka 2016. Tayari, Serikali inatumia mabilioni ya fedha kila mwezi kughaharamia elimumsingi nchini. Kwa dhati kabisa tunampongeza Rais wetu mpendwa pamoja na watendaji wote wa Wizara husika.
Moja ya mafanikio ya kujivunia yaliyotokana na utekelezaji wa elimumsingi bila malipo ni kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wa elimumsingi nchini. Hata hivyo, ongezeko hili limekuja na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa miundombinu ya madarasa, walimu, msongamano wa wanafunzi mdarasani, upungufu wa vitabu n.k. Tunatambua juhudi kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya TAMISEMI hasa katika suala la ujenzi wa miundombinu ya madarasa, kuajiri walimu zaidi, kusambaza vitabu vya kiada na ziada mashuleni n.k Hayo pia ni mambo ya msingi sana na hayana budi kupongezwa kwa dhati kabisa.
Ni dhahiri kuwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimumsingi bila malipo itaendelea kuongezeka na kuwa kubwa zaidi mwaka hadi mwaka. Sambamba na hili, mamlaka husika zitaendelea kuwajibika kuhakikisha kuwa walengwa wanaendelea kupata fursa ya elimumsingi katika mazingira bora na salama. Swali linalogonga vichwa vya wadau wengi wa elimu ni, Je kasi ya ongezeko la wanafunzi kwa upande mmoja litawiana na ongezeko la ujenzi wa miundombinu ya madarasa, ajira za walimu, usambazaji wa vitabu mashuleni n.k kwa upande mwingine?, iwapo hatukuweza kuwa na uwiano wa wanafunzi 45 kwa mwalimu mmoja au kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja wakati wa elimumsingi iliyokuwa inatoza ada, je tutaweza kufikia uwiano huo katika mazingira ya elimumsingi bila malipo?
Utoaji wa elimu kwa njia tulizozoea pekeyake hautaweza kumaliza changamoto ya upungufu wa madarasa, walimu, vitabu n.k. Nashawishika kushauri kuwa ni wakati sasa wa kuanza kutekeleza elimu mtandao (m-Elimu) kimkakati zaidi katika kutoa elimu katika ngazi zote kwa lengo la kutatua changamoto na kutoa fursa ya elimu kwa wanafunzi wengi zaidi. Elimu mtandao ni matumizi ya miundombinu mbalimbali ya TEHAMA kwa lengo la kufikisha fursa ya elimu kwa wanafunzi wengi zaidi pamoja na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza unyumbufu katika kutoa elimu. Tafiti zinaonyesha kuwa elimu mtandao ikiandaliwa kimkakati na kutekelezwa kwa umakini, kwa viwango vilivyowekwa inauwezo mkubwa wa kuchangia katika kutatua nyingi ya changamoto za kielimu nchini ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu na hata upungufu wa vitabu.
Naomba nitaje sababu tatu zilizonisukuma nishauri hivi; kwanza, uwepo wa utashi wa kisiasa. Suala la elimu mtandao (TEHAMA) lipo bayana katika sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, Sera ya TEHAMA ya elimumsingi 2003 na Sera ya TEHAMA ya Taifa 2007. Aidha, umuhimu wa elimu mtandao pia umesisitizwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Sambamba na hili, mwongozo wa awali wa kuhakikisha ubora wa elimu mtandao ulioandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na SIDA na GESCI mwaka 2011upo.
Sababu nyingine ni uwekezaji mkubwa uliofanyika na unaoendelea kufanyika katika suala la miundombinu ya TEHAMA hususan katika baadhi ya shule za sekondari. Siku za karibuni tumeshuhudia shule ya sekondari Mzumbe na Kilakala za Morogoro wakikabidhiwa kompyuta zenye rejea nyingi na zilizounganishwa na internet. Tumeshuhudia shule nyingi sana zikiwekewa miundombinu ya namna hii japo bado uhitaji ni mkubwa. Pia, kadiri ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015, kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule zote za sekondari na vyuo vikuu katika mkongo wa Taifa wa mawasiliano ili kuwezesha elimu mtandao nchini ni moja ya maeneo ya kipaumbele.
Aidha, licha ya mafunzo ya TEHAMA katika vyuo vya ualimu, idadi kubwa ya walimu hasa sekondari wamepata mafunzo kazini kuhusu namna ya kufundisha kwa kutumia TEHAMA yakiwemo yale yaliyofanyika DIT, Dar es Salaam miezi michache iliyopita.
Takwimu zinaonyesha kuwa kuna watanzania wengi wakiwemo wanafunzi wa ngazi ya elimumsingi wanamiliki na wanatumia TEHAMA na hivyo kuna ongezeko kubwa la matumizi ya mtandao (internet), mitandao (socialmedia) pamoja na TEHAMA za mikononi (mobile devices) kama simu za kiganjani, ipad, laptop n.k miongoni. Aidha, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), watanzania wa vijijini sasa wana mawasiliano ya simu za viganjani na lengo ni kufikisha huduma hii kwa watanzania wote katika vijiji vyote.
Ni wakati sasa tuanze kutumia miundombinu hii iliyopo na ile itakayowekwa kutekeleza mipango mikubwa ya kitaifa ya elimu mtandao badala ya miradi isiyoendelevu kutatua changamoto za kielimu pamoja na kufikisha fursa ya elimu kwa wanafunzi wengi zaidi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na malengo ya elimu kwa wote (education for all) ifikapo 2030.
Ipo mifano mingi ya kutekeleza elimu mtandao lakini nitajikita katika hii mitatu. Kwanza, tuanze kutumia video conferencing. Ili kutatua changamoto ya ongezeko la wanafunzi na upungufu wa walimu mashuleni, elimu mtandao kama video conferencing inaweza kutumika kuendesha vipindi mbalimbali vilivyoandaliwa na walimu mahiri na wenye uzoefu kwa kuzingatia mitaala ya elimu kwa ngazi husika. Sio lazima wanafunzi wote wawe shuleni, badala yake wanaweza kuhudhuria masomo katika vituo maalumu vitakavyoandaliwa na kuwekwa miundombinu ya video conferencing katika ngazi ya mikoa na wilaya kwa kuanzia lakini baadaye vinaweza kuwekwa hadi ngazi ya kata. Aidha, baadhi ya walimu wenye ujuzi wa TEHAMA na wataalamu wa TEHAMA wachache wanaweza kuwa katika kila kituo kwa ajili ya uratibu, kuwasaidia wanafunzi kufuatilia masomo yako na kutoa huduma za ushauri na kiufundi.
Pili, kutoa masomo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ya kuendesha mafunzo (lessons / course management systems). Elimu mtandao kwa kutumia mifumo hii inaweza kutumika maalumu kwa kutoa fursa ya elimu kwa wanafunzi ambao wanaweza kufuatilia masomo kwa kutumia miundombinu ya TEHAMA kama kompyuta na internet walizonazo majumbani badala ya kila mwanafunzi kuja darasani. Kupitia mfumo huu, kunakuwa na ratiba itakayoonyesha ni mara ngapi kwa wiki mwalimu atafundisha moja kwa moja (live online lessons) au mwanafunzi atajifunza kwa wakati wake akiwa popote pamoja na taratibu nyingine kama zinavyofanyika katika darasa halisi. Kwa namna hii, mwalimu mmoja atafundisha somo lake kwa wanafunzi wote nchi nzima na hivyo kupunguza uhitaji wa mwalimu wa somo hilo kwa kila shule.
Tatu, kuanzisha shule mtandao (online / virtual schools) za serikali na za wawekezaji binafsi ambapo Wizara ya TAMISEMi itaratibu itatakiwa kuwa imeandaa kanzidata itakayoonyesha mwanafunzi yupi anapenda kusoma elimumsingi kwa utaratibu upi na kuwapanga hivyo. Wale ambao watapenda elimu mtanda watasoma hivyo na wale wa elimu tuliyoizoea (conventional education) nao watasoma hivyo. Kupitia shule za namna hii, vipindi vilivyorekodiwa (recorded lessons) pamoja na vitabu kadiri ya mitaala husika vitapatikana hapo.
Hii itasaidia wanafunzi wengi zaidi kupata fursa ya elimu bila kulazimika kufika shuleni au kuingia darasani. Shule mtandao zitaondoa changamoto za msongamano wa wanafunzi mashuleni na pia kupunguza tatizo la walimu na vitabu. Sambamba na hili, upo umuhimu wa kuanzisha “shule mtandao zinazotembea” (mobile online schools), “madarasa mtandao yanayotembea” (mobile online classrooms) na fursa nyingine za aina hiyo ili kufikisha fursa ya elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika jamii.
Hata hivyo, ili kuhakikisha elimu mtandao inatekelezwa kwa ubora, ufanishi na kwa tija, mambo yafuatayo ni muhimu yakazingatiwa; mosi, kupitia upya Sheria ya Elimu Na. 25 ya mwaka 1978 ambayo ipo kimya kuhusu elimu mtandao ili iendane na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Sera ya TEHAMA ya Elimumsingi 2003 na Sera ya TEHAMA ya Taifa 2007.
Kwa mfano ni muhimu Sheria ya Elimu ifafanue maana ya elimu mtandao kwa mazingira na maadili ya Tanzania, iweke wazi vigezo vya kusajili huduma za video conferencing, shule mtandao, shule mtandao zinazotembea, madarasa mtandao yanayotembea na taratibu za uendeshaji huduma hizo iwapo watu binafsi watajitokeza kuwekeza katika huduma hizo.
Pili, ni wakati sasa wa kuboresha mwongozo ulioandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na SIDA na GESCI mwaka 2011 kuhusu elimu mtandao ili uendane na mahitaji ya sasa na viwango vya kimataifa. Mwongozo utakuwa ni rejea kuhusu viwango vya ubora vya kuzingatia wakati wa kusajiri elimu mtandao (National Standards for Online Education) pamoja na utaratibu mzima wa kufuatwa.
Tatu, ukusanyaji wa taarifa za wanafunzi kabla ya kuanza masomo hauna budi uhusishe taarifa kuhusu utaratibu ambao mwanafunzi atapenda kutumia katika masomo yake.
Iwapo mwanafunzi atapenda kusoma kwa utaratibu tuliouzoea wa kwenda shuleni na kuingia darasani, au kupitia elimu mtandao nyumani au kwenye vituo nitakavyoandaliwa na Serikali katika ngazi ya mikoa na wilaya kwakuanzia. Hii itasaidia katika kufanya maamuzi kuhusu nani atapata elimu kwa kwa utaratibu upi na wapi.
NNe, juhudi za kuboresha miundombinu ya TEHAMA hazina budi kuendelea pamoja na kuboresha zaidi utoaji wa mafunzo kwa walimu vyuoni juu ya namna ya kufundisha kwa kutumia TEHAMA sambamba na mafunzo kazini.
Mwsho, ni imani yangu kuwa elimu mtandao inawezekana na wakati wa kuthubutu. Hakika tunahitaji kuanza sasa kutekeleza mipango mikubwa ya kitaifa ya elimu mtandao kwa kutumia miundombinu ya TEHAMA iliyopo na itakayowekwa. Kwa maoni yangu, ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na Malengo ya Elimu kwa Wote, Tanzania haina budi kuanza kutumia elimu mtandao kama moja ya juhudi za kukabiliana na changamoto za ongezeko la wanafunzi nchini ambalo litakuwa kubwa zaidi huko miaka ya mbeleni.
Makala hii imeandikwa na Dr. Kassimu Nihuka
Mhadhiri Mwandamizi,
Sayansi na Teknolojia za Elimu
+255 658 323 218



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...