MVUA
zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma,zimesababisha kuharibika kwa miundombinu ya barabara katika mtaa
wa Kipika kata ya Matarawe wilayani humo na hivyo kutishia kukata
mawasiliano kati ya mtaa huo na maeneo mengine ya mji wa Mbinga.
Kutokana
na uharibifu uliotokea,baadhi ya wakazi wa mji wa Mbinga wameiomba
Serikali kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani makandarasi
na wahandisi wa wakala wa barabara vijijini na mijini Tanzania (TARURA)
kwa kushindwa kusimamia majukumu yao ikiwemo ujenzi wa mradi huo chini
ya kiwango.
Walisema,
ni kawaida baadhi ya barabara katika mji wa Mbinga kuharibika ndani ya
muda mfupi tangu zinapojengwa na hali hiyo inatokana na wahandisi
kushindwa kutumia taaluma zao wakati wa kutekeleza miradi ya Barabara
katika wilaya hiyo.
Wamesema,
kupeana kazi za ujenzi wa miradi ya barabara kwa misingi ya urafiki na
kujuana kwa kiasi kikubwa kumechangia miradi mingi ya barabara katika
mji huo kujengwa chini ya kiwango na hivyo kushindwa kuleta tija.
Aidha,wameiomba
taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mikataba
inayoingiwa kati ya Tarura na Makandarasi ili kufahamu juu ya uwezo wa
wakandarasi wanaopewa kazi katika Mji wa Mbinga.
Wakiongea
kwa nyakati tofauti,wakazi hao Antonia Komba,Daud Shija na Suzana
Ndomba wamesema, baadhi ya miradi inayojengwa haimalizi kero za
wananchi licha ya kutekelezwa kwa fedha nyingi za walipa kodi wa nchi
hii.
Antonia
Komba mkazi wa mtaa huo, alitolea mfano ujenzi wa mifereji iliyojengwa
katika barabara ya Kipika mtaa wa Kipika imedumu kwa miezi saba tu
tangu ilipojengwa na sasa imeharibika kutokana na kusombwa na maji ya
mvua na hivyo kushindwa kumaliza kero ya muda mrefu ya wananchi wa
kata ya Matarawe.
Alisema,
mifereji hiyo badala ya kuleta faraja kwa wananchi imeonekana sio
salama hasa kwa watoto wadogo wanaopita maeneo hayo wakati mvua
zinaponyesha ambapo maji kutoka maeneo ya milimani yanapita kwa wingi.
Mkazi
mwingine Daud Shija amesikitishwa kuona mifereji iliyojengwa kwa fedha
nyingi imeanza kuharibika kabla ya mvua hazijawa kubwa na hivyo kuwa
na hofu kuhusu uwezo wa mkandarasi aliyejenga mifereji hiyo.
Shija
ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la TAG Mbinga, ameiomba Serikali kupitia
taasisi na idara zake kupima na kujiridhisha juu ya uwezo wa
wakandarasi wanaoomba kazi za ujenzi ili kuepusha matumizi mabaya ya
fedha za Serikali.
“kwa
kweli nilipoona mifereji inajengwa katika eneo hili nilifurahi na
kuipongeza sana Serikali kwa hatua hii,lakini furaha yangu imepotea
ghafla baada ya kuona mifereji yote imeharibika kwa muda mfupi tangu
ilipojengwa, mimi kama Mtanzania naishauri Serikali lazima iwe makini
na waandisi wake na wakandarasi”alisema Mchungaji Shija.
Ditram
Shabani alisema, uwezo mdogo wa makandarasi ndiyo sababu ya mifereji
hiyo kuharibika kwa muda mfupi, tofauti na matarajio ya wakazi wa mtaa
huo kwani ni kama hakufanya kazi yoyote katika eneo hilo ambalo ni
kiungo muhimu kwa wakazi wa kata ya Matarawe na maeneo mengine ya Mji wa
Mbinga.
Suzana
Ndomba alisema, ‘’kila mvua inaponyesha maji yanayopita katika eneo
hilo yanakuwa na kasi kubwa hali inayo hatarisha maisha ya watoto wadogo
na hivyo wanalazimika kuwafungia ndani kama hatua ya kuwaepusha
kusombwa na maji.
Meneja
wa wakala wa Barabara(Tarura)Mji wa Mbinga Ismail Mafita hakupatikana
kutolea ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kwa kuwa yuko nje ya wilaya
ya Mbinga na hata alipotafutwa kwa njia ya simu alikataa kujibu
chochote badala yake alituma ujumbe mfupi (sms) yuko Hospitali.
Hata
hivyo,Kaimu Meneja wa Tarura Amos Agustine alikiri kuharibika kwa
mifereji iliyojengwa katika eneo hilo,ambapo alisema hali hiyo imetokana
na athari za mvua zinazo endelea kunyesha kwa wingi katika wilaya ya
Mbinga.
Amos
ameitaja kampuni iliyojenga mifereji ni Stumack Engineering Co Ltd ya
Dar es salaam huku akitaja gharama za mradi huo ni shilingi Milioni
33.6.
Kwa
mujibu wake,kazi ya ujenzi wa mradi huo ilianza mwaka 2018 na
kukamilika mwaka 2019 ambapo muda wa uangalizi umemalizika tangu tarehe
17 Novemba mwaka huu na mkandarasi ameshakabidhi mradi kwa Tarura.
Aidha
alieleza,mpango uliopo kwa sasa ni kumpata mkandarasi mwingine ambaye
atajenga upya mifereji hiyo, hata hivyo alisisitiza kuwa, suluhisho la
kudumu ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika eneo hilo
sambamba na kuimarishwa kwa mifereji.
Alisema,
eneo hilo ni kati ya maeneo mengi katika Mji wa Mbinga ambapo barabara
zake zimeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa
wingi katika mji wa Mbinga.
Mkandarasi
wa mradi huo aliyefahamika kwa jina moja la Mwafyenga alipotafutwa kwa
njia ya simu alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sababu yuko
Hospitalini amelazwa.

Mitaro iliyojengwa katika Mtaa wa Kipika kata ya Matarawe na Wakala wa Barabara mjini na vijijini(Tarura) Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma ikiwa imeharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika wilaya hiyo,hata hivyo kuharibika kwa Mitaro hiyo kumetajwa na baadhi ya wakazi wa Mbinga kunatokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango na kukosa usimamizi makini wa Tarura ambapo imeanza kuharibika katika kipindi cha miezi sita tu tangu mkandarasi akabidhi kazi hiyo.
Mhandisi wa wakala wa Barabara mjni na vijijini(Tarura)Mji wa Mbinga Amos Agustine akieleza jambo juu ya kuharibika kwa mifereji iliyojengwa katika mtaa wa Kipika kata ya Matarawe Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,

Mitaro iliyojengwa katika Mtaa wa Kipika kata ya Matarawe na Wakala wa Barabara mjini na vijijini(Tarura) Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma ikiwa imeharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika wilaya hiyo,hata hivyo kuharibika kwa Mitaro hiyo kumetajwa na baadhi ya wakazi wa Mbinga kunatokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango na kukosa usimamizi makini wa Tarura ambapo imeanza kuharibika katika kipindi cha miezi sita tu tangu mkandarasi akabidhi kazi hiyo.

Mhandisi wa wakala wa Barabara mjni na vijijini(Tarura)Mji wa Mbinga Amos Agustine akieleza jambo juu ya kuharibika kwa mifereji iliyojengwa katika mtaa wa Kipika kata ya Matarawe Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...