Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza wakati alipofunga semina ya Viongozi wa Dola katika
Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini kwenye ukumbi wa St. Gaspar
jijini Dodoma, Januari 26, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiagana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi baada
ya kufunga semina ya Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa
Rasilimali Madini kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari 26,
2019. Kulia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko , Wa tatu kulia ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Madini, Stanslaus Nyongo na wapili kushoto ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
Baadhi ya washiriki wa semina ya
Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini
wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofunga semina hiyo
kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari 26, 2019.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina ya Viongozi
wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini baada ya
kuifunga semina hiyo kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari
26, 2019. Waliokaa kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Madini,
Profesa. Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.
Bilinith Mahenge na kulia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Stanslaus
Nyongo.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………….
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe
vinawalinda wafanyabiashara wa madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata
sheria na kujiepuka kamata kamata zisizo na tija.
“Katika
kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa
wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila
sababu za msingi. Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea
suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo
kufuata taratibu.”
Ametoa agizo
hilo leo (Jamapili, Januari 26, 2020) wakati akifunga semina ya ushiriki
wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika usimamizi na udhibiti wa
rasilimali madini katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.
Waziri Mkuu
amesema kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatakiwa vitumie Sheria,
Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha
usimamizi wa sekta ya madini.
Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kuviagiza vyombo vya Dola kusimamia na kudhibiti
utoroshwaji wa madini na kuhakikisha kuwa masoko yote ya madini nchini
yanalindwa.
“Nyote
mtakubaliana nami kwamba kila taasisi ina utaalamu na wataalamu wake.
Kwa hivyo, hatunabudi kufanya kazi kwa kuheshimu na kutambua utaalamu
ama taaluma za wengine tunaoshirikiana nao.”
“Sasa ni vema
tukaondoa tofauti zetu na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuimarisha
udhibiti na usimamizi wa rasilimali madini. Aidha, tutambue kuwa kuna
nyakati hatuhitaji kutumia nguvu nyingi bali ushauri tuu ili kutatua
changamoto husika.”
Waziri Mkuu
ameelekeza kwamba kuanzia sasa wadau wote wanaopatikana na madini
wapewe utaratibu wa kuelekea sokoni kuuza madini hayo badala ya
kuwakamata wakiwa wanaenda sokoni.
Waziri Mkuu
amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ina ofisi mikoa yote ya
Tanzania Bara, hivyo hakuna sehemu ambayo wanaweza kusema walikosa
msaada wa kitaalamu. “Ni wajibu wetu sote kama watumishi wa umma kujenga
mazingira rafiki ya kazi, kuaminiana na kufanya kazi kwa ushirikiano.”
Wakati huo
huo,Waziri Mkuu amesema kuazia sasa suala la migodi kutegemea bidhaa
mbalimbali kutoka nje ya nchi lifikie ukomo kwa kuhakikisha kuwa, kila
huduma inayohitajika migodini, inapatikana nchini.
Waziri Mkuu
amesema nchi inawajibu wa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa
madini kwa maana ya kutoa huduma kwa ubora stahiki na kwa wakati
muafaka.
Amesema sekta
ya madini inazalisha ajira ila kuna changamoto ya ubora wa ajira,
mishahara na stahiki katika kazi zinazofanana na suala la unyanyasaji wa
wafanyakazi. Waziri Mkuu
amesema masuala mengi hapo yanaweza kuonekana haraka kwenye maeneo yao
ya kazi, hivyo ni vyema wakawa na taarifa hizo kwa wakati na kuwasilisha
kwa wahusika ili mambo yawekwe sawa na kuipeleka sekta mbele.
Akizungumzia
kuhusu suala la unyanyasaji wa wafanyakazi wazalendo amesema si suala la
kufumbiwa macho kama ilivyo suala la usalama wa watenda kazi katika
migodi.
Kadhalika,
suala la udhibiti wa wageni kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na
Watanzania wenzetu pia ni jukumu letu na hivyo ni wajibu wetu kusimamia
mikataba tuliyoingia na wawekezaji hususani eneo la urithishaji wa
madaraka na ujuzi kwa wazawa. Kwa upande wa
Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Waziri Mkuu amewaagiza watafute
suluhu ya changamoto ya usalama wa wafanyakazi kipindi wakiwa kazini na
baada ya kumaliza muda wa kazi kwa hiari au kwa kustaafu au kumaliza
mkataba. “Tumepokea malalamiko mengi sana katika eneo hilo.”
“Hivyo, ni
wajibu wetu kushirikisha wadau wote wanaohusika na masuala ya ajira,
bima za wafanyakazi, afya za wafanyakazi na usimamizi wa stahiki za
wafanyakazi kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto hii ili isiendelee
kukomaa.”
Vilevile,
Waziri Mkuu ameagiza suala la utunzaji wa mazingira liwekewe mkazo wa
kipekee maana nje ya mazuri yote yaletwayo na Sekta ya Madini, uharibifu
wa mazingira unaweza kugharimu maisha ya binadamu, wanyama na mimea.
Waziri Mkuu
amesema “mazingira yetu ndio uhai wetu sisi na vizazi vijavyo, hivyo ni
wajibu wetu kama Wizara kuhakikisha wawekezaji wetu ni watu wema kwa
mazingira yetu.”
Pia, Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kwa uthubutu mkubwa alioufanya ambao umeleta mageuzi makubwa
katika Sekta ya madini.“Hili
linadhihirishwa na kitendo cha utiaji saini makubaliano ya uanzishwaji
wa Kampuni ya Twiga Minerals uliofanywa juzi Jijini Dar es Salaam tarehe
24 Januari 2020 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria Mpya ya Madini
ya mwaka 2017.”
Awali, Waziri
wa Madini Doto Biteko alisema lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa wa
pamoja kwenye masuala ya usimamizi wa sekta ya madini nchini.
Alisema suala
la kudhibiti utoroshwaji wa madini linafanyika kwa kushirikiana kati
Wizara ya Madini na vyombo vya Ulinzi na Usalama na kwamba wanaendelea
kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza.
Waziri Biteko
ametumia fursa hiyo kutuma salamu kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na
utengenezaji na uuzaji wa madini bandia pamoja na wanaotaka kuuza
madini nje ya mfumo kuwa zama zao zimekwisha.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...