Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii
WANAFUNZI wa Tanzania ambao wanasoma kwenye vyuo mbalimbali vilivyopo nchini China wameshauriwa na Balozi wa Tanzania nchini humo Mbelwa Kairuki kuhakikisha wanafuata sheria na maagizo yaliyotolewa na Serikali ili kujiepusha kupata virusi vya ugonjwa wa Corona ambao umesababisha vifo vya watu kadhaa hadi sasa.
WANAFUNZI wa Tanzania ambao wanasoma kwenye vyuo mbalimbali vilivyopo nchini China wameshauriwa na Balozi wa Tanzania nchini humo Mbelwa Kairuki kuhakikisha wanafuata sheria na maagizo yaliyotolewa na Serikali ili kujiepusha kupata virusi vya ugonjwa wa Corona ambao umesababisha vifo vya watu kadhaa hadi sasa.
Balozi Kairuki ametoa ushauri huo leo Februari 10 mwaka 2020 wakati akitoa ufafanuzi wa video inayosambaa mtandaoni ambayo inaonesha Watanzania ambao wako China wakiendelea na masomo katika vyuo mbalimbali wakiomba warejeshwe nchini Tanzania.
"Ni kweli nimeona ujumbe wa vijana wetu wakitaka kurejeshwa nchini, ifahamike ugonjwa Corona upo katika nchi yote ya China lakini upo zaidi katika Jimbo la Hubei na hasa Mji wa Wuhan ambako ndio vijana wametuma ujumbe wa kutaka waondolewe.
"Na katika hatua za kukabiliana na ugonjwa huu Serikali ya China ilichukua hatua ya kuweka Karantee kwa maana watu wote katika jimbo hilo, wanatakiwa kukaa ndani , hakuna anayeruhusiwa kutoka nje ya jimbo au ndani ya mji huo.Kila aliyekuwa ndani anatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuepuka msongamano na pale ambapo unataka kutoka nje lazima uvae mask,"amesema Balozi Mbelwa.
Amefafanua kuwa kutoka na kuwepo kwa ugonjwa huo, hakuna usafiri wa treni inayokwenda kule, hakua basi, hakuna ndege na wala hakuna aina nyingine yoyote ya kufika huko na hali hiyo imesababisha wanafunzi hao wa Tanzania kuwa kwenye msongo wa mawazo.
"Wenzetu wa Serikali ya China wamekuwa wakirejea rai yao kwamba usalama wa watu utazingatiwa kwa watu kukaa ndani, sasa kukaa ndani muda mrefu sote tunaelewa lazima utakuwa na mawazo na hii ndio inayopelekea vijana wetu kutaka waondolewe.Hata hivyo kwa sasa kuna zuio la watu kutoka na wanafunzi nimezungumza nao mwenyewe na hata mwishoni mwa wiki iliyopita nilikuwa na vikao na viongozi wao kupitia njia ya simu kwani hata mimi hapa nilipo siruhusiwi kusogea hata nje ya geti, hivyo mazingira waliyonayo ninaelewa lakini mwisho wa siku lazima tufuate masharti kwa ajili ya usalama.
"Nawapongeza kwa kufuata masharti na ndio maana wako salama, lakini kwa mkusanyiko ambao wameufanya kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe wao wamevunja masharti, maana virusi vya ugonjwa huo ni hatari.Hivyo kukusanyika kwao ni makosa na wanahatarisha maisha yao,"amesisitiza.
Balozi Kairuki amesema kuwa ujumbe wao walishaupeleka na uafanyiwa kazi na mambo hayo hatatakiwi kufanywa kwa mihemko bali kwa kufuata tararatibu ili wawe salama.
"Muhimu zaidi tunajifunza kutoka kwa mataifa mengine, Japan walikuwa na watu wao na katika zoezi la kuwaondoa wanafunzi wao watano walipata maambukizi ya Corona na wakati wanarudi wengine watano nao wakapata ugonjwa huo, na sasa idadi ya wagonjwa wa Corona Japan imeongezeka na kufikia 20, hatutaki kurudia makosa ambayo Japan imefanya.
"Maana yake tutaupeleka ugonjwa nchini kwetu na ndio maana tunataka kuliangalia jambo hili kwa busara na bora ya kuhakikisha usalama wa vijana hao. Ni matarajio yetu kuona kila mmoja anakuwa salama na hatutaki kupeleka ugonjwa nyumbani, wenzetu wa China wana fedha nyingi, wana madaktari wengi na ndani ya wiki mmoja wamejenga hospitali kubwa , kwetu sisi hatuna uwezo huo.Hivyo nchi za Afrika inayo kila sababu ya kuchukua hata ili ugonjwa usifike katika nchi zetu,"amesema.
Balozi Kairuki amesema kuwa pale ambapo watapata uhakika wa kutosha wa kufanya katika kusaidia vijana hao basi watachukua hatua huku akiwaomba wanafunzi hao kuwa na subira."Nawaomba mchukue tahadhari, na kikubwa zaidi tuendelee kuwasiliana.Serikali ya China imehakikisha inatuma maski za kutosha na wataendelea kutuma kila aina ya kifaa ili kukabiliana na ugonjwa huo,"
Hata hivyo amesema kuwa tayari wamezungumza na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na wamewahakikishiwa wanafunzi hao kuwa salama."Nitoe ombi kwa Watanzania endeleeni kutuombea kwani tunapita katika kipindi kigumu sana."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...