Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipeana mkono na
Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini
Tanzania, Bw. Jens Reinke, aliefika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango
Jijini Dodoma kujitambulisha.


Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBC), Dkt. Albina Chuwa (kulia) akieleza jambo wakati wa
Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb) (kushoto) na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tatu kushoto)
akieleza kuhusu agenda ya Serikali ya kujenga uchumi Jumuishi, wakati wa
Mkutano kati yake na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke (wa tatu kulia), katika
ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.

Mwakilishi Mkazi
mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens
Reinke, akieleza nia yake ya kushirikiana kwa dhati na Tanzania kwa
kuisemea Serikali katika Shirika lake kuhusu vipaumbele vya Taifa,
wakati alipofika katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini
Dodoma kujitambulisha.

Mtakwimu Mkuu wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBC), Dkt. Albina Chuwa (kushoto) akiwa na
Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini
Tanzania, Bw. Jens Reinke, baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya
Mwakilishi huyo wa IMF na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani).

Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tano kulia) na
Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini
Tanzania, Bw. Jens Reinke (wa tano kushoto), wakiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya wajumbe waliohudhulia Mkutano kati ya Dkt. Mpango na
mwakilishi huyo wa IMF nchini, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango jijini Dodoma.(Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)
****************************
Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali ya
Tanzania inatarijia kukutana na Timu ya wataalamu kutoka Shirika la
Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kujadili Programu mpya ya Ushauri wa
Kisera (PSI) yenye dhima ya kusimamia sera za kiuchumi kwa lengo la
kutatua changamoto zitakazoonekana pamoja na namna ya kutumia fursa
mbalimbali zilizopo nchini.
Haya yameelezwa
na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, alipokutana na
kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi mpya wa IMF nchini, Bw. Jens
Renke, aliyekuja kujitambulisha rasmi kwa Waziri huyo jijini Dodoma
baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hapa nchini.
Dkt. Mpango
alisema kuwa pamoja na kufanya majadiliano na wataalamu hao, Serikali
inatarajia kuwa wataafikiana nao ili kuanzisha programu hiyo ya Serikali
ambayo Shirika hilo limekuwa likishauri.
“Tumekuwa
tukishirikiana na IMF kwa muda mrefu na imekuwa ikitushauri mambo
mbalimbali ya kusimamia Sera za Kiuchumi katika kuondoa changamato ya
umasikini na kuwa na maendeleo endelevu kwa usimamizi wa Sera za Uchumi
“, alieleza Dkt. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango
alimueleza Mwakilishi huyo kuwa vipaumbele vya Serikali na juhudi mbali
mbali zilizofanyika katika kukabiliana na tatizo la umaskini ni pamoja
na kujenga uchumi jumuishi, kusimamia fedha za umma vizuri, kuhakikisha
kwamba nchi inaendelea kuwekeza katika kilimo pamoja na ujenzi wa
miundombinu ya kisasa.
Waziri Mpango
alibainisha kuwa vipaumbele vingine ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa
na kukusanya mapato ya ndani ipasavyo ili kuweza kutumia rasilimali
zote za nchi vizuri na kuboresha huduma muhimu za wananchi kama elimu na
afya.
Aidha, alimueleza mgeni huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana nae katika kuleta maendeleo nchini.Naye Mwakilishi
Mkazi mpya wa IMF nchini, Bw. Jens Renke, aliahidi kuwa balozi mzuri wa
Tanzania katika Shirika hilo na kuiomba Serikali ushirikiano katika kazi
zake.
Aliiomba Serikali
imtumie katika kutatua matatizo mbalimbali na yuko tayari kutoa ushauri
wa kisera na kichumi, na kubainisha kuwa atafanya kazi kama sehemu ya
Serikali katika kutatua matatizo na kuleta maendeleo nchini.
Bw. Renke alisema
anapenda kujifunza mengi nchini na atatembelea katika mikoa, Serikali
za Mitaa pamoja na vyuo mbalimbali ili kuona mambo ambayo Serikali
imeyafanya katika kujikwamua kiuchumi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...