Na Ramadhani Ali - Maelezo Zanzibar
Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeanza ukaguzi wa wauza maziwa wasiofuata utaratibu unaokubaliwa ikiwemo sehemu zisizo rasmi ili kulinda afya za wananchi.

Mkurugenzi Idara ya Udhibiti Usalama wa Chakula wa ZFDA Dk. Khamis Ali Omar alisema ukaguzi umefanyika baada ya kutoa elimu na matangazo kwa wauza maziwa kuacha kutumia chupa na madumu ya plastiki na katika maeneo yasiyo rasmi. 

Alisema chupa na madumu ya plastiki baada ya kutolewa maziwa hayawezi kusafika na hubakisha chembe chembe za maziwa wakati wa kukosha ambazo baada ya muda huoza.

Dk. Khamis alisema zoezi hilo litakuwa endelevu na amewataka wauzaji wa maziwa kufuta maelekezo yanayotolewa na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ili kujiepusha na gharama zisizo za lazima.

Alisema chupa na madumu ya plastiki ambayo yamekuwa yakitumiwa na wauza maziwa hayapo salama na yanaweza kusababisha maradhi ya kuambukiza ikiwemo kifuakikuu.

Aliwashauri wauzaji wa maziwa kuwa na maeneo maalumu ya kuuza bidhaa hiyo kwa kutumia chupa za vigae zilizopunguzwa mwangaza na kutumia keni za aluminiam kubebea maziwa.

 Muuza maziwa wa eneo la Amani Haroun Abdalla alikiri kuwa  ZFDA walitoa elimu kuhusu madhara ya kutumia chupa na madumu ya plastiki lakini muda waliopewa kujitaarisha kutumia chupa za vigae na keni za alluminiam ni mfupi.

Alisema bei ya keni moja ya kubebea maziwa inagharimu zaidi ya shilingi laki mbili kiwango ambacho wauzaji wadogo waliowengi wengi hawawezi kumudu kununua kwa kipindi kifupi.

Muuzaji mwengine Ali Muhamed alisema tatizo kubwa liliopo Zanzibar hakuna kiwanda kinachozalisha chupa za vigae zinazotakiwa kutumika kwa ajili ya kuuzia maziwa.

Katika ukaguzi huo wafanyakazi wa ZFDA waliharibu lita kadhaa za maziwa waliyoyakuta yakiuzwa katika sehemu zisizo rasmi na kutumia chupa na madumu ya plastiki.
 Maafisa ukaguzi kutoka Wakala wa Chakula na Vipodozi Zanzibar wakifanya ukaguzi baada ya kutoa tangazo kwa wauza maziwa kuacha kutumia madumu na chupa za plastika kuhifadhia maziwa tangazo ambalo halijatekelezwa.
 Mkuu wa ukaguzi wa chakula kutoka (ZFDA) Muhamed Shadhil Shauri akiyaharibu maziwa kwa kuyatia rangi wakati wa ugakuzi wa wafanya biashara ya maziwa waliokuwa hawafuati utaratibu katika eneo la Amani Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya wananchi wakishuhudia maafisa wa (ZFDA) wakiyaharibu maziwa yaliyokuwa kwenye madumu na chupa za plastiki eneo la Amani Mjni Zanzibar.
Mkuu wa ukaguzi wa chakula kutoka Wakala wa Chakula na Vipodozi Zanziba (ZFDA) Muhamed Shadhil Shauri akiyapima maziwa yaliyotiwa katika sehemu salama kuona kama hayajatiwa maji katika ukaguzi uliofanywa maeneo mbali mbali ya Mkoa Mjini Magharibi.

Picha na Makame Mshenga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...