Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya Dkt. Zainab
Chaula akiwa kwenye jengo la mpaka wa nchi ya Uganda ikiwa ni ziara yake
ya kikazi ya kuangalia utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula
akiongea na watumishi wa idara mbalimbali wa mpaka wa mtukula nje ya
jengo la kituo cha pamoja nchini Tanzania.

Dkt. Chaula akiangalia ofisi ya
maofisa afya wa mpaka wa mtukula nchini Tanzania na kujionea jinsi
wanavyotoa huduma ikiwemo ya kudhibiti magonjwa ya milipuko na utoaji wa
chanjo ya homa ya manjano(Yellow Fever)
………………………………………………………………
Na. Catherine Sungura-Kagera
Maofisa afya wanaofanya kazi kwenye mipaka nchini wametakiwa kuongeza umakini wa kufanya ukaguzi katika mipaka.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara kuu Afya Dkt. Zainab Chaula wakati alipotembelea mpaka wa Mutukula nchina Tanzania na Uganda ikiwa ni moja ya ziara yake ya kuangalia utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko ambayo inafanywa na wizara ya afya kwa kushirikiana na TAMISEMI.
“Umakini mkubwa unatakiwa katika kufanya ukaguzi kwa wasafiri wanaopita kwenye.mpaka huu ingawa kuna mwiingiliano mkubwa baina ya nchi hizi mbili ili kuweza kuzuia magonjwa ya mlipuka kama Ebola usiingie nchini.
“Kujilinda ni jambo moja na kuzuia ni jambo lingine,nimetembelea mpaka huu, nimejionea na maofisa wetu wa Tanzania wa afya, forodha, uhamiaji wamenieleza changamoto iliyopo hapa ni mwingiliano mkubwa, watu wanatoka upande mmoja kwenda mwingine kwa wingi, wanashirikiana kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi,hivyo lazima muangalie tunatoka vipi kwenye hili.
Hata hivyo Dkt. Chaula aliwapongeza watumishi wote wa idara zote kwa ushirikiano na kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kudhibiti magonjwa ya milipuko hayajaingia nchini.
“Lakini pamoja na hayo, bado inahitajika muwe imara zaidi, ndiyo maana tumeleta vifaa tiba vya kisasa vya ukaguzi wa joto la afya ya mwili, nawasihi msimamie hili kwa umakini zaidi,” alisema.
Aidha, Dk. Chaula alisisitiza maofisa afya hao kuongeza elimu.ya afya kwa umma kwa wananchi wote wanaopita mpakani hapo ili kuwajengea uelewa jinsi ya kujikinga na dalili za magonjwa hayo“Wataalamu wa afya wa Mkoa na viongozi wote pamoja hakikisheni elimu ya afya kwa umma inafika hadi kule vijijini, watu wetu waelewe jinsi ya kujikinga,” alisema Dk. Chaula.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...