Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed akizungumza na Waandishi wa
habari kuhusu Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya
masuala ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama Jumuiya ya
MaendeIeo Kusini mwa Afrika, tarehe 16 Februari, 2020, Ukumbi wa Shirika
la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni
ya Kukabiliana na Maafa, Zanzibar, Makame Khatibu Makame akitoa
Ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa
kuhusu Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya
menejimenti ya Maafa kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrikatarehe 16 Februari, 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji
Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.


Baadhi ya waandishi wa Habari
wakifuatilia Mkutano wa Waandishi wa Habari na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed (hayupo pichani)
wakati wa akifafanua kuhusu Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri
wenye dhamana ya masuala ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama
Jumuiya ya MaendeIeo Kusini mwa Afrika, tarehe 16 Februari 2020, Ukumbi
wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.
……………………………………………………………………………………..
Ndugu Wananchi,
Kama tunavyoeelewa kuwa kufuatia
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC), uliofanyika mwezi Agosti 2019 ambapo, Mhe. Dkt. John Joseph
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokea rasmi
uenyekiti wa jumuiya hiyo, hali hiyo imepelekea mkutano mbalimbali
ya Kisekta kufanyika hapa Tanzania.
Ndugu Wananchi,
Mkutano huu unafanyika kutokana na
umuhimu mkubwa wa Mawaziri wa nchi wanachama wa SADC wanaohusika na
masuala ya maafa kukutana kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya
pamoja ya namna bora ya kukabiliana na matukio ya maafa yanayoukabili
ukanda huu yakiwemo vimbunga, mafuriko, ukame, na hata ajali za baharini
ambayo yamekuwa yakisababisha athari kubwa kwa maisha ya watu na mali.
Sote ni mashuhuda athari za
Kimbunga Idai na Keneth vilivyotokea katika nchi za Madagascar, Malawi,
Msumbiji na Zimbabwe vilipelekea vifo vya maelefu ya watu na wengine
kutoonekana kabisa na kupelekea mahitaji ya kiasi cha dola bilioni 10
za Kimarekani kwa ajili ya kurejesha hali.
Ndugu Wananchi,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika
na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika utakaofanyika katika hoteli ya Madinat Al Bahri
Mbweni, tarehe 18 – 21 Februari, 2020, hapa Zanzibar. ambapo Kaulimbiu
ya Mkutano huu: “Ushiriki wa Kisekta kwenye Kupunguza madhara ya
maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika” (SADC)
Ndugu Wananchi,
Mkutano huu unakuja kipindi
ambacho nchi nyingi wanachama katika ukanda huu zimekuwa zikiathiriwa na
majanga ya asili mara kwa mara na kusababisha madhara makubwa. Hali
iliyoonesha wazi umuhimu wa mashirikiano ya kikanda katika kukabiliana
na maafa ili kupunguza athari za maafa, kukuza uwezo wa kujiandaa na
kukabiliana kwani mara nyingi athari zinazotokana na majanga ya
kimaumbile yakiwemo ukame, mafuriko, maradhi ya mlipuko na mengineyo,
hupelekea vifo kuharibu miundombinu muhimu ikiwemo barabara na hudumaza
msingi za jamii kama vile afya na elimu na kupelekea gharama
kubwa katika kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Ndugu Wananchi,
Katika hatua ya kujenga mataifa
yenye uhimili katika kukabiliana na maafa, SADC imefanikiwa katika
kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema inayoendana na majanga ya Hali
ya hewa, kuandaa vikao vya mwaka kwa nchi wananchama kwa ajili ya
kujikinga, kujiandaa na kukabiliana na maafa pamoja na kuandaa mipango
ya dharura na kutoa mafunzo ya utafutaji na uokozi kwa majanga ya
baharini kwa nchi wananchama.
Ndugu Wananchi,
SADC imetekeleza program ufanyaji
wa tathmini na uchambuzi wa usalama wa chakula kwa nchi wananchama 14
zilizoathiriwa na majanga yanayoendana na hali ya hewa yakiwemo ukame,
imeandaa mpango na mkakati wa pamoja kwa ajili ya kujikinga na kukabili
maafa. Mikakati yote hiyo ni kwa ajili ya kupunguza athari za maafa
katika kanda hii. Mnamo mwaka 2017-2018 takribani watu wapatao milioni 7
waliathiriwa na maafa idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na watu
milioni 17 walioathirika katika miaka ya 2015-2016.
Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, imekamilisha kuandaa nyaraka zote muhimu katika masuala ya
kukabiliana na maafa ikiwemo sheria ya Usimamizi wa Maafa ya Kitaifa Na.
7 ya 2015, Sheria ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar No. 1 ya mwaka 2015,
Sera za Kukabiliana na Maafa, Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na
Maafa na Mkakati wa Mawasiliano Wakati wa Maafa na rasimu ya Mkakati wa
Kukabiliana na Maafa pamoja kuanzisha vituo vya mawasiliano na
operesheni za dharura na vituo vya uokozi hasa kwa majanga ya baharini.
Mkutano huu wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika unalenga katika kushajihisha juhudi zilizopo
katika kukabiliana na maafa kwa kuziwezesha nchi wanachama kuandaa
mikakati ya uhimili kutokana na athari za maafa, kuandaa mkakati wa
kujiandaa na kukabiliana na maafa. Aidha, mikakati hii itaisaidia sana
juhudi za ukanda huu katika kupunguza athari za maafa na kuimarisha
uwezo wa nchi husika katika kukabiliana na maafa pamoja na kurejesha
hali baada ya maafa kutokea.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuwakaribisha
waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kufuatilia juu ya Mkutano huu
ambao utakuwa ni fursa tosha ya kutangaza utalii wetu na kukuza uchumi
wan chi pamoja na kupunguza athari za maafa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...