*Ni baada ya Makonda kudai mzee Mkapa alimpa fedha za TASAF
 
Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

RAIS Dk.John Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kurudisha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) huku akifafanua huenda kuwa Makonda ni kati ya wanakaya ambao si masikini lakini wamepata fedha hizo.

Ametoa kauli hiyo leo Februari 17 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam wakati akizindua awamu ya tatu ya TASAF ikiwa ni mkakati wa mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia mfuko huo.Sababu za Rais kumtaka Makonda kurudisha fedha hizo ni baada ya Mkuu huyo wa Mkoa kueleza mbele yake kuwa mwaka 2012 wakati anakwenda Dodoma kubombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM alipewa nauli na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

"Naomba niwapongeze marais wastaafu mliopo hapa kwenye uzinduzi wa TASAF, nitumie nafasi hii kukupongeza Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwani katika awamu yako ndio ulianzisha mfuko huu, na moyo wako wa upendo haukuishia kwenye TASAF tu kwani huenda hata ile nauli ambayo ulinipa kwenda Dodoma itakuwa ni sehemu ya fedha za TASAF.Na leo hii niko hapa naendelea kuwatumikia wanananchi,"amesema Makonda.

Baada ya kauli hiyo ya Makonda ambayo aliitoa wakati anatambulisha viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Magufuli wakati anatoa hotuba yake ametumia nafasi hiyo kumeleza Makonda kama ni kweli alipewa fedha za TASAF anatakiwa kuzirudisha mara moja."Fedha ambazo umechukua kama ni za TASAF kweli, rudisha haraka.Moja ya changamoto ambayo imebainika ni kuwepo kwa kaya hewa ambazo zimefuja hizi fedha, na katika kaya hizo kuna kaya 22034 zilithibitika kuwa wanakaya wake si masikini,huenda kati ya kaya hizo yumo na Makonda."

Kuhusu TASAF, Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu mzee Benjamin Mkapa kwa kuungana nao kwenye tukio hilo na kwmaba kama wanavyofahamu mpango huo wa TASAF ulianza kutekelezwa mwaka 2000 wakati huo mzee Mkapa alikuwa Rais wa nchi yetu."Hii ina maana kwamba yey ndiye alibuni wazo la kuanzisha mpango huu.

"Namshukuru mzee Jakaya Kikwete , Rais mstaafu wa Awamu ya Nne aliyehakikisha mpango huu wa TASAF unaendelea katika kipndi chake.Aidha namshukuru Rais wa Zanzibar Dk.All Mohamed Shein aliyesimamia vizuri mpango huu wa TASAF visiwani Zanzibar,"amesema.

.Rais Magufuli pia amesema tatizo la umasikini hususani wa mahitaji ya msingi/kipato na chakula ni moja ya changamoto kubwa inayozikabili nchi nyingi duniani lakini zaidi kwenye Bara la Afrika.Kwa mujibu wa Benki ya Dunia mwaka 2015 takribani watu milioni 736 walikuwa wakiishi kwenye umasikini uliokithiri duniani, ambapo kipato au matumizi yao yalikuwa chini ya mstari wa umasikini , yaani chini ya dola za Marekani 1.90 ."Chakusikitisha zaidi ni kwamba zaidi ya nusu (asilimia 55) ya masikini wote duniani wanaishi barani Afrika ambapo mwaka 2015 idadi yao ilikuwa milioni 413.

"Hii inamaanisha kwamba kwenye kila watu watatu waishio kwenye Bara la Afrika mmoja ni masikini, na kwa mujibu wa Benki ya Dunia, endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa ikifika mwaka 2030 asilimia 90 ya masikini wote duniani watakuwa kwenye Bara la Afrika,"amesema Rais.

Amefafanua Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kukabiliwa na tatizo la umasikini na kwamba itakumbukwa kuwa mara tu baada ya nchi yetu kupata Uhuru ,Baba wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliutaja umasikini kuwa miongoni mwa maadui wakubwa watatu wa Taifa letu."Maadui wengine ni ujinga na maradhi na tangu wakati huo awamu zote za uongozi wa nchi yetu zimekuwa zikibuni na kutekeleza sera, mipango , mikakati , programu na miradi mbalimbali ya kupambana na umasikini.

"Na kutokana na jitihada hizo, hali ya umasikini imekuwa ikipingua.Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kiwango cha umasikini wa matumizi ya msingi nchini kimepungua kutoka asilimia 39.0 mwaka 1990/1990 ambapo utafiti wa kwanza wa kisayansi ulifanyika, hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2017/2018.Aidha umasikini wa chakula nao umepungua kutoka asilimia 18.7 mwaka 2000/2001 hadi kufikia asilimia 9.5 mwaka 2017/2018,"amesema Rais Magufuli.

Ameongeza takwimu hizo zinathibitishwa na taarifa ya watafiti wa Benki ya Dunia iliyotolewa Seotemba mwaka 2019 ambayo imeitaja Tanzania kuongoza kwa kasi ya kupambana na umasikini kwenye nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
 
Hivyo ametumia fursa hiyo kuzipongeza awamu zote za uongozi wa nchi yetu kwa jitihada kubwa ilizofanya kupambana na tatizo la umasikini nchini."Sio siri kuwa Tanzania ya sasa sio ile ya mwaka 1964."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...