Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kutoka
kushoto) akionyesha mwongozo wa matibabu ya saratani nchini Tanzania
mara baada ya kuuzindua katika siku ya Saratani Duniani iliyofanyika
katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizindua mwongozo wa
matibabu ya saratani, upande wa kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba
kutoka Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe, aliye kushoto ni Mkurugenzi
Mtendaji Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo kwa wadau
wa Sekta ya Afya (hawapo pichani) katika siku ya Saratani Duniani
iliyofanyika katiaka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi mwongozo wa
matibabu ya saratani kwa Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Mifupa MOI Dkt.
Respicious Boniface.
******************************
Na Mwandishi Wetu – Dar Es Salaam
Dar es Salaam. Serikali ya
Tanzania imezindua mwongozo wa kitaifa wa tiba ya magonjwa ya saratani
utakaoziwezesha hospitali za serikali na binafsi katika kutoa matibabu
kwa usawa na kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na
wataalamu wengine.
Kuzinduliwa kwa mwongozo huo
kumefuatia baada ya hospitali za kanda kuanza kutoa tiba za saratani,
kuongezeka kwa hospitali binafsi na za umma zinazotibu ugonjwa huo kwa
sasa nchini, huku kwa kipindi kirefu hospitali nyingi zikitumia miongozo
tofauti na ile ya nje ya nchi.
Akizindua mwongozo huo, Waziri wa
Afya Ummy Mwalimu amesema huduma za saratani zinasambaa katika hospitali
mbalimbali nchini kwa sasa hivyo utoaji wa huduma lazima uangaliwe ili
zitoke kwa kiwango kinachopaswa.
Amesema kuwepo kwa miongozo
tofauti ilisababisha kutokuwepo kwa usawa katika tiba za wagonjwa lakini
pia kulikuwa na changamoto ya mgonjwa kuendelea na tiba sahihi pindi
akipewa rufaa kwenda hospitali nyingine.
“Kuwepo kwa mwongozo huu
kutawezesha kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na
wataalamu wengine wa matibabu ya saratani kote nchini,
“Kurahisisha uandaaji wa maoteo na
ununuzi wa dawa na vitendanishi vinavyotumika katika matibabu ya
saratani, mwongozo huu pia umetoa orodha ya dawa na vifaa tiba kwa ajili
ya matibabu ya saratani ambayo itatumika kama mwongozo kwa ajili ya
manunuzi na matumizi nchini,” amesema Ummy Mwalimu.
Amesema mwongozo huo pia
itawezesha wananchi kupata huduma bora na za viwango vya juu katika
vituo vyote vya matibabu kwa kuwa tiba zote zitapangwa kwa kufuata
mwongozo huo.
Waziri Ummy amesema pia utawezesha
kutoa mwongozo kwa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF kuhusu dawa na
vipimo mbalimbali stahiki kwa wagonjwa wa saratani.
“Mfuko wa Taifa NHIF uhakikishe
unatumia mwongozo huu katika kuweka vitita vya huduma za saratani hapa
nchini kwani katika ile standard treatment guideline kuna baadhi ya dawa
za kutibu saratani hazikuorodheshwa, na niwaambie mmeweka masharti
magumu sana katika vipimo hivi CT Scan na MRI nani anapima mara kwa mara
tuondoe baadhi ya vikwazo na hili NHIF mkalitekeleze,” ameagiza.
Ameagiza mwongozo huo utumike na vituo vyote vinavyotoa tiba za saratani nchini;
“Ninafahamu hospitali zote zilishiriki kuuandaa hivyo sitegemei
kusikia kuna hospitali inafanya tiba nje ya mwongozo huu, ninaagiza pia
wizara kufanya mapitio ili kuhakikisha dawa zote zinazotibu saratani
zinakumuishwa katika mwongozo huu.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Julius Mwaiselage amesema, “Matumizi ya
mwongozo huu yamefanyiwa majaribio kwa kipindi cha miezi sita katika
taasisi hii kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha St Francisco.”



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...