Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akieleza
umuhimu wa Serikali kushiriki kikamilifu katika uchambuzi wa mazingira
ya Sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi, wakati wa Mkutano na Meneja wa
Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za
Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (kulia), jijini Dodoma.

Meneja wa Shirika
la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika
Mashariki, Somalia na Malawi (kulia), akieleza fursa zilizopo katika
Shirika lake ikiwemo mikopo, wakati wa mkutano na Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), katika
ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akipeana mkono
na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses,
anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (kulia),
baada ya kumalizika kwa Mkutano ulioangazia Sekta Binafsi, jijini
Dodoma.

Wajumbe wa
Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb) na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses,
anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (hawapo
pichani), wakifuatilia kwa makini maelezo ya fursa zilizopo katika
Shirika la IFC, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini
Dodoma.

Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kushoto),
akipeana mkono na Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel
Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Somalia na Malawi (wa
tatu kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi wa wajumbe wa
mkutano huo kutoka Tanzania na Shirika la IFC.
*****************************
Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali ya
Tanzania imeiomba Benki ya Dunia kupitia Shirika lake la Fedha
(IFC), kufanya kazi ya uchambuzi wa kitaalamu wa mazingira ya Sekta
Binafsi nchini kwa kushirikiana na Serikali ili kuweza kufanyia kazi
kikamilifu taarifa za uchambuzi huo kwa manufaa ya Taifa.
Hayo
yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip
Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Meneja wa Shirika la
Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, anaeziwakilisha nchi za Afrika
Mashariki, Somalia na Malawi.
Dkt. Mpango
alisema kuwa msimamo wa Serikali ni kuwa kazi ya uchambuzi wa changamoto
za mazingira ya Sekta Binafsi ifanyike kwa ushirikiano kati ya Serikali
na IFC ili taarifa ya matokeo ya uchambuzi huo iweze kufanyiwa kazi
kikamilifu badala ya taarifa hiyo kuachwa bila kufanyiwa kazi kutokana
na ushirikishwaji hafifu kutoka katika taasisi hiyo.
“Tunataka
kufanyia kazi taarifa ambayo tumeshiriki kuiandaa na tutakuwa
tunatekeleza jambo letu sisi wenyewe”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango
amelitaka Shirika hilo lijielekeze katika misaada ya kitaalam na fedha
ili kukuza Sekta Binafsi kwa kuendana na vipaumbele vya Serikali ya
Awamu ya Tano hususan upande wa kilimo bila kuiacha nyuma Sekta ya
viwanda kwa kuangalia namna wadau wa Sekta Binafsi wanavyoweza kupata
utaalam kutoka IFC.
Aidha alibainisha
kuwa Tanzania imewahi kufanya kazi za uchambuzi na Serikali ya Marekani
mwaka 2011 wakati wa kupitia utekelezaji wa dira ya maendeleo na
kuandaa mipango ya nchi, pia kuna mpango wa kuangalia mazingira ya
biashara pamoja na jarida lenye hatua mbalimbali ambazo zilikubaliwa na
Sekta Binafsi katika kukuza sekta hiyo na kutoa ajira kwa wananchi.
“Kazi yoyote
lazima izingatie mipango ya Serikali katika kuendelea kuboresha
mazingira ya kukua kwa Sekta Binafsi, kufanya biashara na kuwekeza”,
aliongeza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango
alisema kuwa wamejadili pia kuhusu uwezekano wa IFC kutoa hati fungani
ambayo kwa sasa inalipwa kwa dola iweze kutolewa kwa Shilingi ya
Tanzania. Hata hivyo alibainisha kuwa bado jambo hilo linahitaji
uchambuzi wa kitaalamu kwa kuwa hati fungani haiwezi kutolewa bila nchi
kufanya tathmini huru na makampuni ya kimataifa kuhusu nguvu yake ya
kuweza kukopa kwenye masoko kama hayo.
Alisema kuwa hadi
mwishoni mwa mwezi huu majibu yatatatolewa baada ya wataalamu kuchakata
na kupata majibu ya kuendelea na jambo hilo au kulisitisha.
Kwa upande
mwingine Serikali ya Tanzania imeiomba Benki ya Dunia
kupitia Shirika hilo la IFC, kufuata Sheria za nchi inapotoa misaada
ikiwemo ya Sekta Binafsi ili kujiridhisha iwapo misaada hiyo inamanufaa
kwa taifa.
Aliyasema hayo
baada ya kuwepo kwa misaada iliyotolewa kwa Sekta Binafsi na Shirika
hilo ambayo haikufuata utaratibu wa utoaji misaada unaotumika nchini kwa
mujibu wa sheria zilizowekwa.
Dkt. Mpango
alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria za nchi maombi yote ya misaada nchini
ni lazima yapite kwenye kamati ya kitaalamu ya kuishauri Serikali kuhusu
madeni na baadae kamati ya kitaifa ambayo itatoa ushauri kwa Waziri wa
Fedha ili aweze kusema sawa, iwapo msaada huo unamanufaa kwa maendeleo
ya taifa.
Kwa upande
wake Meneja wa Shirika la Kimataifa la IFC, Bw. Manuel Moses, alikubali
kufanyia kazi ushauri wa Dkt. Mpango na pia alisema kuwa wamefanya
mazungumzo na Serikali ili kusaidia kuboresha zaidi mazingira ya Sekta
Binafsi ili iweze kuajiri watu wengi zaidi na kulipa kodi katika juhudi
za kukuza uchumi wa nchi husika.
Shirika la IFC
lipo chini ya Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea
kama Tanzania kuendeleza Sekta Binafsi pamoja na kutoa mikopo na misaada
mbalimbali ambapo kwa sasa wameelekeza mikopo mingi kwenye Sekta ya
Benki ambayo hutoa mikopo kwa kampuni ndogo na kubwa hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...