Na Abdullatif Yunus wa Michuzi TV.

Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa inajipanga kujenga Soko la Mazao na  Mnada wa Mifugo katika Kata ya Murongo Wilayani Kyerwa  lenye thamani ya Shilingi 114, 549,996 lengo likiwa ni kudhibiti biashara ya magendo ya usafirishaji na uuzaji wa mazao na mifugo kwa njia zisizokuwa halali.

Mpango huo ni miongoni  mwa vipaumbele ambavyo vimebainishwa katika Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020-2021, uliowasilishwa katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, wakati ambapo Baraza hilo limeketi katika Kikao maalum cha kujadili makadirio ya mpango na Bajeti mnamo 17. Feb, 2020.

Awali akifungua Kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ndg. Kashunju Runyogote amesema miongoni mwa vipaumbele ambavyo vinapendekezwa katika Bajeti hiyo ni pamoja na ujenzi wa Soko kubwa la Mnada wa mazao na mifugo ambalo litasaidia kudhibiti biashara ya uvushaji mifugo na mazao kwenda nje ya Nchi kwa njia za magendo, hivyo Soko hilo litasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri.

Aidha Mwenyekiti Kashunju amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa Stendi ya magari katika Miji ya Nkwenda na Murongo, Ununuzi wa Boti kwa ajili ya udhibiti uvuvi haramu, kuimarisha sekta ya Afya  kwa kuongeza vifaa tiba na madawa, kuimarisha sekta ya Elimu kwa kuboresha miundo mbinu na mengine.

Akisoma muundo wa bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyerwa, Afisa mipango Wilaya ya Kyerwa Ndg. John Mayunga Msafiri ametaja kiasi kinachoombwa na halmashauri hiyo kuwa ni jumla ya Shilingi 28,107,595,004.34 ambapo ruzuku ya matumizi ya kawaida ni Shilingi 974,320,000.00, shilingi 18,707,379,000.00 ni mishahara, shilingi 3,577,664,009.34 ni miradi ya maendeleo toka Serikali Kuu, Shilingi 1,981,699,360.00 ni makusanyo ya ndani, Shilingi 1,569,032,635.00 ni mchango kutoka kwa  wadau wa maendeleo.

Tayari Baraza hilo limepitisha Bajeti hiyo baada ya kukamilika Kwa Kikao hicho kilichoketi siku mbili, huku hoja mbalimbali zikijadiliwa ikwemo masuala ya Vitambulisho vya Taifa, miundombinu ya Barabara, Huduma za Afya na Maji, Umeme, masuala ya Utawala bora,  Elimu, Kilimo hususani bei ya Kahawa na mengine mengi.
 Pichani ni baadhi ya Madiwani wa Kata 24 zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa wakiendelea na Kikao, wakati wa kujadili Bajeti ya Mwaka wa fedha 2020/2021.
Pichani ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Ndg. Kashunju Runyogote akitoa Maelezo machache wakati wa ufunguzi wa Kikao cha kujadili rasimu ya Bajeti ya Halmashauri hiyo.

 Pichani ni Afisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya Kyerwa Ndg. John Mayunga Msafiri akiwasilisha umbile la Bajeti ya Halmashauri ya Kyerwa mbele ya wajumbe wa Kikao cha Baraza la madiwani, tayari kwa kujadiliwa.

 Pichani ni Mkuu wa Wilaya Kyerwa Mhe. Rashid Mwaimu akitoa ufafanuzi na maelekezo ya Serikali katika hoja zilizoulizwa na Madiwani, wakati wa kujadili Bajeti ya Halmashauri hiyo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...