Wajumbe wa Kamati ya Michezo ya
mashindano ya Mei Mosi wakiwa kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya
michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano
wa Chuo cha Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo
ya mashindano ya Mei Mosi, Moshi Makuka (aliyenyoosha mikono)
akisisitiza jambo kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo
kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro.

Wajumbe wa mkutano wa maandalizi
wa michezo ya mashindano ya Mei Mosi (pichani) wakiwa kwenye kikao cha
maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye
ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani
Morogoro
………………………………………………………………………………………………..
Na Bahati Mollel, Morogoro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa nchini Tanzania (Takukuru) mkoa wa Mwanza itashirikishwa kwenye
michezo ya mashindano ya Mei Mosi inayotarajiwa kuanza Aprili 16-29,
2020 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, endapo kutakuwa na timu
za Wizara, taasisi za Umma na Binafsi zitawatumia wachezaji wasiokuwa
watumishi wao halali.
Katibu wa Kamati ya michezo
hiyo, Moshi Makuka, alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha
kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, ambapo
suala hilo limewekwa kwenye kanuni namba 13 kati ya 15 zilizopitishwa na
wajumbe wote walioshiriki kwenye kikao hicho.
Makuka alisema mbali na
Takukuru kushirikishwa kubaini uhalali wa mchezaji aliyesajiliwa na timu
iliyomchezesha, pia viongozi wote walioshiriki kumsajili mchezaji huyo
wataripotiwa kwenye taasisi hiyo, ili sheria za nchi zichukue mkondo
wake.
“Haya mashindano yanajumuisha
watumishi halali wa taasisi na wizara hivyo hairuhusiwi kuwachezesha
wachezaji ambao sio watumishi halali, kwa lengo la kujipatia ushindi,
hili ni katazo na kanuni yetu ipo wazi kabisa, hivyo timu zisithubutu
kuja na wachezaji hao kabisa,” alisisitiza Makuka.
Alizitaja adhabu ambazo timu
itakayobainika kumtumia mamluki ni pamoja na viongozi wake watafungiwa
kushiriki michezo hiyo kwa muda wa miaka miwili na nakala ya barua
itawasilishwa kwa Mwajiri wake; timu itatozwa faini ya Tshs. 500,000;
timu husika itapokonywa ushindi endapo itakuwa imeshinda; timu
itaondolewa kwenye mashindano.
Kamati imesema mamluki
wanadhibitiwa kwa wanamichezo kuwa na vitambulisho halisi vya kazi, Kadi
ya Bima ya Afya, Kadi ya Mfuko wa Jamii na hati ya Malipo ya mshahara
za miezi miwili ‘salary slip’.
Hatahivyo, Makuka alisema
tyimu zote shiriki zinatakiwa kuwahi mkoani Mwanza tarehe 14 Aprili,
2020 ambapo ndipo sherehe za Sikukuu za wafanyakazi zitafanyika Kitaifa
kama ilivyotangazwa awali, ambapo timu itakayochelewa hadi tarehe 20
Aprili, 2020 itakuwa imejiondoa kwenye mashindano hayo.
“Timu ikichelewa inawapa shida
na kuwaumiza wachezaji kwa kuwa watacheza mfululizo ili kwenda na
ratiba, hadi kufikia michezo yao iliyosalia, hivyo hii hatutaki kwani
michezo itakuwa haina ushindani kwa kuwa wachezaji wa timu moja watakuwa
wamechoka kwa kucheza mfululizo wa mechi mbili au tatu kwa siku, hivi
huu ni mwezi wa pili muanze kufuatilia ruhusa za wachezaji wenu,”
alisema Makuka.
Kamati inategemea ushiriki wa
timu zaidi ya 25, kwa kuwa zinaongezeka kila mwaka ambapo mwaka jana
zilishiriki timu 23. Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na soka,
netiboli, kuvuta kamba, baiskeli, riadha, karata, bao na draft.
Pia Makuka amesisitiza timu
shiriki kulipa ada ya ushiriki kwa wakati, ili fedha hizo zitumike
katika ulipaji wa gharama mbalimbali za uendeshaji wa mashindano hayo.
Ada ya ushiriki ni Tshs.
1,000,000 ambapo kila timu inatakiwa kulipa mapema kabla ya tarehe 6
Aprili, 2020, ili timu ziweze kupewa kadi za ushiriki zitakazofanikisha
usajili wao.
Halikadhalika Makuka amesema
timu zote zilizotwaa vikombe kwa kuwa washindi wa Kwanza hadi wa tatu
wanatakiwa kurejesha vikombe walivyoshinda kabla yatarehe 29 Machi, 2020
na timu itakayochelewa utatozwa faini ya Tshs. 200,000.
Wakati huo huo, Makuka amesema
timu zinaruhusiwa kushiriki kwenye michezo ya mashirikisho mbalimbali
yakiwemo ya Shimiwi, Shimmuta na Mei Mosi, na sio kusubiri michezo ya
shirikisho moja, ambayo kwa wakati huo inakuwa haijafanyika kwa sababu
mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...