Na Mdau wa Soka Arusha

Hatua hii itakuwa siyo ya kujenga bali ni kubomoa soka letu. Kiuhalisia kwa sasa ni timu 3 zenye uwezo wa kusajili wachezaji 10 wa kigeni; Simba, Yanga na Azam.


Usajili  kwa sasa unaruhusu kila timu ya TPL kusajili wachezaji mpaka 30 kwa msimu.Kwa mahesabu hayo jumla ya namba ya wachezaji wanaosajiliwa na timu 20 za ligi kuu ni 600(30 x20). 

Chukulia mfano timu 3 kubwa zimesajili wachezaji 10 wa kigeni kila moja ukijumlisha unapata wachezaji 30.



Chukulia pia mfano timu 17 zilizobaki zimesajili uwiano wa wachezaji 5 wa kigeni kila timu utapata jumla ya wachezaji 85 wa kigeni ingawa kiuhalisia  hawafikii namba hiyo kwa sasa.



Hivyo, ukijumlisha 30 wa timu kubwa 3 na makadirio ya 85 wa timu 17 zilizobaki
unapata jumla ya wachezaji 115 wa kigeni kati ya wachezaji wote 600 wanaosajiliwa ligi kuu kwa msimu.



Kimahesabu inamaanisha wachezaji wa kigeni kimakadirio ni asilimia 19 tu ya wachezaji wote wanaosajiliwa ligi kuu ingawa kiuhalisia hiyo asilimia ipo chini zaidi ya hapo.



Ligi ya Uingereza (EPL) ambayo ni maarufu zaidi duniani ina zaidi ya 60% ya wachezaji wa kigeni na inakaribia mpaka 80% kwa baadhi ya timu kubwa za ligi hiyo. Ligi hiyo inaruhusu kila timu kusajili  wachezaji hadi 17  wa kigeni kati ya jumla ya 25 lakini bado timu ya taifa ya Uingereza inashikilia nafasi ya nne kwa ubora duniani licha ya kwamba  kwenye kikosi chao cha sasa ni wachezaji wao wawili tu ndo wanacheza ligi za nje, mmoja Spain(Trippier) na mwingine Ujerumani(Sancho).



Tujiulize, hivi kweli asilimia 19 tu inaweza kuathiri  ukuaji wa vipaji vya wachezaji soka wa kitanzania?



Ushahidi uliopo unaonyesha hali halisi ni kinyume na huo mtazamo maana inaonekana tayari kuwa kiwango cha wachezaji wa kitanzania hasa kwenye timu ndogo kwenye ligi kinaendelea kukua, ushindani unaongezeka, tactical discipline inaboreka kidogo kidogo na hii kwa kiasi  inachangiwa pia  na uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni.



Kwa upande mwingine, tunashuhudia idadi ya wachezaji wa kitanzania wanaocheza nje ikizidi kuongezeka, timu zetu za Taifa zimeanza kidogo kupata mafanikio endelevu  mfano mfululizo kufuzu AFCON,  CHAN na hatua ya makundi kombe la dunia na hii inatokana pia na mikakati endelevu ya TFF kukuza soka la vijana, ushiriki wa mashindano ya kimataifa katika ngazi zote za umri na kutengeneza utaratibu mzuri wa kuendesha ligi za madaraja ya chini.



Katika kipindi hiki ambacho timu zetu  zinafanya uwekezaji mkubwa wa kusajili wachezaji bora wa viwango vya kimataifa  na kuboresha miundombinu yao kwa lengo la kuchukua mataji makubwa Afrika  wazo hili la kupunguza idadi wachezaji wa kigeni litakwamisha juhudi hizo na kudumaza kiwango cha soka letu kwa miaka mingi ijayo.



Soka ni mchezo na burdani namba moja kwa asilimia kubwa ya watanzania hivyo ni vyema busara ikatumika kwa kutoa nafasi ya mjadala mpana utakaoshirikisha wadau na wapenzi wa soka  kabla ya kuchukua maamuzi mazito kama haya ambayo siku za baadaye yanaweza kuonekana yalifanywa kwa kukurupuka.



.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...