Wataalam wa upasuaji, radiolojia, patholojia, tiba ya mionzi na dawa wamekutana kwa lengo la kujengeana uwezo ili kuboresha huduma za upasuaji kwa wagonjwa wanaogunduliwa na saratani ya matiti mapema ili kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonyesha kuwa wanaogunduliwa na saratani ya matiti ni kati ya wanawake wenye umri wa miaka 40 hadi 80.
Hayo yamesemwa na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi wakati akiwasilisha mada kuhusu hali ya ugonjwa wa saratani ya matiti nchini katika mafunzo ya wiki moja iliyoandaliwa na Hospitali ya Muhimbili kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Roche ya nchini Kenya.
“Saratani ya shingo ya kizazi ni ya kwanza ikifuatiwa na saratani ya matiti ambayo ni ya pili kwa sasa, mwaka 2007 saratani ya ngozi (Kaposi Sarcoma) ilikuwa ya pili na hivi sasa ni ya tatu kati ya magonjwa ya saratani yanayowapata wanawake” amesema Dkt. Magandi.
Mtaalam wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Caspar Haule ameelezea mafanikio walioyapata kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu walipofanya mafunzo Aprili, 2019 kuwa ni pamoja na kuweza kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye titi bila kuliondoa au kuharibu muonekano wake (Breast conserving surgery) kwa wanawake 20.
“Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja toka Aprili 2019 tulipofanya uchunguzi kwa njia ya kisasa kwa wanawake 162 na kuwafanyia upasuaji 152 ambapo kati ya hao 20 waliondolewa vivimbe bila kuondoa titi lote” amesema Dkt. Haule.
“Timu ya Madaktari Bingwa 12 kutoka hospitali mbalimbali nchini pamoja na madaktari wanafunzi 10 tumeanza kufanya upasuaji mwingine kwa wanawake 8 ambao kati yao sita watafanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe bila kuharibu muonekano wa titi (Breast conserving surgery) na wengine wawili watafanyiwa upasuaji wa kuondoa titi ambapo tunatarajia baada ya upasuaji kufanyika wagonjwa hawa watapona ndani ya kipindi cha kuanzia siku 10 hadi 14” ameeleza Dkt. Haule.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Tiba Radiolojia wa (MNH), Dkt. Flora Lwakatare ametaja kuwa pamoja na mafanikio yaliyofikiwa bado kuna changamoto mbalimbali zinazopelekea madaktari kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi nchini kama vile upungufu wa vifaa tiba na mashine za kisasa zinazoweza kupima titi kabla ya kufanyiwa upasuaji, upungufu wa wataalam bobezi na ukosefu wa warsha zinazohusu uchunguzi wa matiti.
Mafunzo hayo imehusisha wataalam takribani 40 kutoka MNH-Upanga na Mloganzila, Kenya, Bugando, KCMC, Mbeya, Ocean Road na Besta.
 Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akiwasilisha mada kuhusu hali ya saratani nchini katika mafunzo ya wiki moja yaliyoandaliwa na Hospitali ya Muhimbili kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Roche ya nchini Kenya.
 Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Matiti kutoka nchini Kenya, Dkt. Peter Bird pamoja na timu ya wataalam bingwa wakishirikiana kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye titi bila kuharibu muonekano wa titi (Breast conserving surgery).
Baadhi ya wataalam kutoka hospitali mbalimbali nchini wakifuatilia mada zilikuwa zinawasilishwa katika mafunzo hayo ya wiki moja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...