Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akimkabidhi Mkurugenzi wa
Shirika la Maendeleo la Kimarekani, USAID, Andy Karas Mpango mkakati wa THBUB
wa miaka mitano (2018/ 2023) alipotembelea ofisi za THBUB zilizopo jijini
Dodoma na kukutana na viongozi wa juu wa taasisi hiyo leo (Februari 20, 2020).
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la
Kimarekani, USAID, Andy Karas akiongea katika kikao kifupi kilichofanyika baina
yake na viongozi wa tume alipotembelea ofisi hizo za THBUB zilizopo jijini Dodoma leo (Februari 20, 2020).
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la
Kimarekani, USAID, Andy Karas akiteta jambo na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji
Mstaafu Mathew Mwaimu muda mfupi baada
ya kumaliza kikao kilichofanyika baina yake na viongozi wa tume alipotembelea
ofisi hizo za THBUB zilizopo jijini
Dodoma leo (Februari 20, 2020).
Na Mbaraka Kambona.
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la
Kimarekani nchini Tanzania, USAID, Andy Karas ameipongeza Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa jitihada zake za kujenga jamii
inayoheshimu na kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora, na
kusema kuwa jitihada hizo ni muhimu katika kusaidia nchi kufikia malengo yake
ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikiapo 2025.
Karas alisema hayo alipotembelea ofisi
za THBUB zilizopo jijini Dodoma na kukutana na viongozi wa juu wa taasisi hiyo
leo (Februari 20, 2020).
Alisema kuwa jukumu la THBUB la kuhamasisha
ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala
bora ni muhimu sana na kuahidi kuwa USAID ipo tayari kushirikiana katika
kutimiza jukumu hilo kikamilifu.
“Jukumu la tume ni muhimu mno, jitihada
zenu ni nzuri, ni wazi kuwa mahala popote ambapo hakuna haki maendeleo ni ngumu
kuyafikia, milango yetu ipo wazi kwa mashauriano na tunawahakikishia kuwa tupo
tayari kushirikiana nanyi”, alisema Karas.
Karas alisema kuwa USAID ipo mstari wa
mbele katika uwekezaji kwenye sekta
mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na Utawala Bora
na kusema kuwa wamekuwa wanawekeza Dola za Kimarekani milioni mia tatu hamsini
(350) kwa mwaka kutekeleza miradi katika maeneo hayo.
Aliendelea kusema kuwa uwekezaji
unaofanywa na USAID unaenda sambamba na mipango mikakati ya Tanzania ili
kusaidia nchi kutimiza ndoto yake ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Hivyo tupo hapa leo, kubadilishana
uzoefu na kujadiliana maeneo tunayofikiri tunaweza kuunganisha nguvu zetu kwa
lengo la kuboresha uhamasishaji wa haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi
ya utawala bora nchini”, aliongeza Kalas.
Aidha, alisistiza kuwa USAID ni mwenyekiti
wa wadau wa maendeleo katika eneo la utawala bora hivyo tume isisite kuwasiliana
nao pindi wanapokuwa na jambo lolote linalohitaji msaada au ushauri.
Akiongea mapema, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji
Mstaafu Mathew Mwaimu alimueleza kwa
ufupi Mkurugenzi huyo wa USAID kuwa tume imepewa majukumu mawili kwa pamoja
nayo ni kusimamia haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
Jaji Mwaimu alitaja vipaumbele vya THBUB
mwaka huu kuwa ni kupokea malalamiko ya uvunjifu wa haki za binadamu na misingi
ya utawala bora, kukuza uelewa wa wananchi kuhusu haki za binadamu, kuimarisha
ushirikiano na wadau mbalimbali, kujenga uwezo wa watumishi na kufanya
ufuatiliaji wa uchaguzi mkuu.
“Tunajipanga kutoa elimu ya kuhamasisha
haki ya kupiga kura wakati, huohuo tunapanga kuwa na mikutano na wadau
mbalimbali wa uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi ili kujadiliana na kukumbushana
umuhimu wa kuwa na uchaguzi mzuri na wa amani”, alisema Mwaimu.
“Hivi
karibuni maafisa wetu walikuwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kufanya
ufuatiliaji wa zoezi la uandikishaji wananchi katika Daftari la Mpiga kura japo
lengo letu ni kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi nchi nzima”, alisisitiza
Mwaimu.
Katika kikao hicho, Karas aliahidi kuwatuma
maafisa wa kitengo cha utawala bora kutoka USAID kwenda kukaa na maafisa wa
THBUB kwa lengo la kujadiliana na kuangalia maeneo ambayo wanaweza
kushirikiana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...