Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Plan International, kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 400 mkoani Mwanza kupitia mradi wa Vijana na Ubunifu katika Kazi (VUKA).

Akizungumza wakati wa tukio la utiaji saini makubaliano hayo leo tarehe 21 Februari, 2020 katika ofisi za VETA Makao Makuu Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Tanzania Dkt. Mona Girgis amesema kuwa makubaliano hayo yanalenga hasa kutoa mafunzo ya ufundi stadi yatayowezesha vijana wanaotoka katika mazingira magumu mkoani Mwanza kupata ujuzi utakaowawezesha kujipatia ajira.

Dkt. Girgis amesema kuwa mradi wa VUKA utatekelezwa katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza na utamalizika mwaka 2021 ukifadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) na shirika la Plan International la nchini Ubelgiji.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa VETA imekuwa ikishirikiana na Plan International katika kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na hivyo kuwekwa rasmi kwa ushirikiano huo ni jambo muhimu.

Dkt. Bujulu amesema kuwa VETA kupitia chuo cha VETA Mwanza itakuwa na jukumu la kudahili na kutoa mafunzo kwa vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu, kutoa ushauri wa kitaaluma na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali ikiwemo makongamano ya vijana.

Mdhibiti wa Fedha kutoka shirika la Plan International la nchini Ubelgiji, Sibylle Gilbert amesema shirika lake linaona fahari kufadhili mradi huo na anaamini kuwa ushirikiano kati ya VETA na Plan International utaleta manufaa makubwa kwa vijana hapa nchini.
 Wafanyakazi wa VETA na Plan International Tanzania katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu na Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Tanzania, Dkt. Mona Girgis, mara baada ya kutia saini makubaliano ya Mradi wa VUKA.
 Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu (kulia) na Mkurugenzi  Mkazi wa Plan International Tanzania, Dkt. Mona Girgis (kushoto), wakitia saini Makubaliano ya Ushirikiano kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa VUKA, leo tarehe 21 Februari 2020 katika ofisi za VETA Makao Makuu, Dar  es Salaam.

 Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, akipeana mkono na Mkurugenzi  Mkazi wa Plan International Tanzania, Dkt. Mona Girgis, mara baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kutoa mafunzo kwa vijana 400 kupitia mradi wa VUKA. Kulia ni Afisa Mwanasheria Mwandamizi wa VETA, Rujama Chisumo na kushoto ni Mkurugenzi wa Miradi wa Plan International Tanzania, Peter Mwakabwale.
 Wajumbe wa Menejimenti ya VETA wakiwa katika majadiliano na Watendaji na Maafisa wa Plan International Tanzania wakati wa tukio la utiaji saini makubaliano ya Mradi wa VUKA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...