Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji (TBC) Ayub Rioba akizungumza katika mhadhara wa nguli wa utangazaji lililofanyika leo katika shule kuu ya uandishi wa habari na Mawasiliano kwa Umma na kueleza kuwa wanahabari lazima wawekeze fikra katika masuala ambayo yanahitaji uchambuzi wa kina, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji (TBC) Ayub Rioba akionesha kitabu hicho katika mhadhara wa nguli wa utangazaji lililofanyika leo katika shule kuu ya uandishi wa habari na Mawasiliano kwa Umma na kueleza kuwa maarifa yaliyopo kwenye andiko hilo ni tunu kwa kizazi cha sasa, leo jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa kitabu cha "Nguli wa Utangazaji Tanzania" Teonas Aswile akizungumza mara baada ya warsha hiyo ambapo amesema kuwa kitabu hicho kitatoa mchango katika tasnia na jamii kwa ujumla, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Ayub Rioba (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Nguli wa Utangazaji Tanzania (walioketi) Edda Sanga (kushoto) na Masoud Manju wa Muziki (kulia) pamoja na wanafunzi wa shule kuu ya uandishi wa habari na Mawasiliano kwa Umma, leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MKURUGENZI wa Shirika la Utangazaji (TBC) Dkt. Ayub Rioba amesema kuwa uthubutu aliouchukuwa mwandishi wa habari Teonas Aswile wa kuandika kitabu kilichobeba jina la "Nguli wa Utangazaji Tanzania" ni mfano bora wa kuigwa kwa tasnia hiyo kwa kuwa kuandika kunaacha alama nzuri hali kadharika maarifa mengi hupatikana kwenye vitabu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mhadhara uliokwenda kwa jina la Nguli wa Utangazaji uliofanyika katika shule kuu ya uandishi wa habari na Mawasiliano kwa Umma Dkt. Rioba amesema kuwa kitabu hicho ni muhimu kwa kuwa kinaeleza historia yetu ya wapi tumetoka na tunapoelekea.
"Ni faraja kubwa kwa kijana Aswile kuandika kitabu cha namna hii ambacho maudhui yake yatanufaisha kizazi Cha sasa na hii ni kwa kuwa kinaeleza ni wapi tumetoka katika tasnia hii, na vijana wafuate nyayo za Aswile ili kuendelea kuiboresha tasnia hii" ameeleza.
Pia amewashauri waandishi wa habari kuiga mfano huo pamoja na kuwa na fikra tunduizi katika kuchambua masuala mbalimbali kwa kina;
"Ni wajibu wetu kutunza historia yetu kwa kueleza ni wapi tumetoka na hiyo ni bila kuhadaika na vibaraka ambao wanaliandama bara la Afrika kwa kupewa vijifedha" ameongeza.
Aidha amesema kuwa uongozi wa awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Joseph Magufuli umekuwa makini katika Kuhakikisha taifa linabaki salama na kutokana na umuhimu wa vyombo vya habari wanahabari hawana budi kuwekeza fikra zao katika masuala yanayohitaji uchambuzi wa kina bila kuyumbishwa na nguvu kutoka nje.
Katika warsha hiyo jumla ya nakala 560 zimetolewa kwa wanafunzi wa Shule kuu ya uandishi wa habari na Mawasiliano kwa Umma ili viweze kuwajenga kifikra na kuwaongezea maarifa zaidi.
Kwa upande wake mwandishi wa kitabu hicho Teonas Aswile kitabu hicho kimesheheni maudhui ambayo kwa namna moja au nyingine yatatoa mchango kwenye tasnia ya habari.
"Nawashukuru wote walioshiriki katika kufanikisha katika kazi hii, nina imani kitabu hiki kitakuwa na mchango katika tasnia ya habari pamoja na kueleza historia ya wapi tumetoka" amesema.
Vilevile amesema kuwa kitabu hicho kimeeleza namna bora ya matumizi ya lugha Kiswahili ambayo yanachagiza kukuza lugha na kueneza utamaduni wa mtanzania.
Kitabu hicho kimesheheni nguli wa utangazaji nchini pamoja na kazi zao ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya habari, na nguli hao ni pamoja na Edda Sanga, Mosoud Masoud Manju wa Muziki na Tido Mhando.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...