Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

SERIKALI ya China kupitia ubalozi wake nchini utafadhili vifaa vya kupambana na virusi vya Corona (Covid 19) ikiwemo kutoa vifaa vya kupima virusi hivyo pamoja na kutoa vitakasa mikono (sanitizers) ambazo zitatolewa kwa wananchi wa hali ya chini ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya virusi hivyo vinavyosambaa katika maeneo mbalimbali duniani.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea kiwanda cha uzalishaji bidhaa binafsi ikiwemo vitakasa mikono (saniters) cha Traidea, Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda amesema kuwa tangu shirika la afya duniani (WHO)  litangaze kuzuka kwa ugonjwa huo Mkoa huo wenye wakazi milioni 6 ni watu watatu pekee wamegundulika kuwa na virusi hivyo.

"Nimetembelea kiwanda hiki na nimewaomba waongeze kasi ya uzalishaji wa vitakasa mikono licha ya kuwa na  changamoto za rasilimali za kutosha za kuwawezesha katika uharakishaji wa rasilimali hizo ili bidhaa ziwe za kutosha kutokana na mahitaji ya jamii" ameeleza.

Amesema kuwa taarifa zote kuhusiana na janga hilo la kidunia zinatolewa na Wizara ya Afya ambayo ina mamlaka;" Sio kila anayepelekwa hospitali ana Corona, kuzuka kwa Corona hakujasimamisha magonjwa mengine hivyo tusiwe wasemaji wa mambo tusiyoyajua, mitandao ya kijamii itumike vizuri" ameeleza Rc Makonda.

Pia Makonda ameiomba Wizara ya Fedha kupunguza Kodi za rasilimali za vitakasa mikono kwa kuwa kupanda kwa bei kwa rasilimali hizo na kufungwa kwa viwanda kwa baadhi ya nchi kumepelekea kupanda kwa bei ya bidhaa hizo sokoni.

Vilevile amewataka wananchi kufuata taratibu za afya zinazoelekezwa kila siku na hiyo ni pamoja na kutowanyanyapaa au kuwaficha waliopatwa na virusi hivyo, kutokusanyika sehemu ambazo sio muhimu ili kujikinga zaidi na virusi hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho Payal Kotecha amesema kuwa kiwanda hicho kimewekeza ndani ya miaka minne katika harakati za kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa viwanda nchini na kimekuwa kikitoa ajira kwa wazawa.

Amesema kuwa kupanda bei kwa vitakasa mikono kumetokana na kukosekana na viungo na malighafi na wameiomba Serikali kusimamia hilo ili malighafi hizo ziingie nchini kwa uharaka zaidi.

Payal amewashauri wananchi kufuata kanuni na taratibu zinazotolewa na Wizara ya Afya kila siku na kueleza kuwa ushirikiano utafanikisha kutokomeza kuenea kwa virusi hivyo ambavyo vimesambaa duniani kote.
 .Mkurugenzi wa kiwanda cha uzalishaji bidhaa binafsi ikiwemo vitakasa mikono Payal Kotecha (kushoto) akitoa maelekezo ya kiwanda hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (katikati) kulia ni Mkurugenzi wa uendeshaji wa kiwanda hicho  Kishan Gokani, leo jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (katikati) akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa binafsi ikiwemo vitakasa mikono cha Tradea ambapo amesema kuwa wananchi wafuate taratibu za afya zinazotolewa kila siku pamoja na kutokuwa wasemaji wa mambo wasiyoyafahamu, leo jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa binafsi ikiwemo vitakasa mikono Payal Kotecha (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutembelea kiwanda hicho ambapo ameiomba Serikali kusimamia malighafi ili ziingie nchini, leo jijini Dar es Salaam.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...