Kikundi cha Wanawake na Mabadiliko Manispaa ya Shinyanga (Women For Change - WFC) kimekabidhi bweni walilokarabati kwenye kituo cha kulea watoto wenye ulemavu mbalimbali cha Buhangija Jumuishi, wakiwamo na watoto wenye ualbino kwa ajili ya kuwaweka katika mazingira mazuri. Zoezi la kukabidhi bweni ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, limefanyika leo Alhamis Machi 5, 2020 ambapo mgeni Rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, huku hafla hiyo fupi ikihudhuriwa pia na maofisa elimu, pamoja na wajumbe wa kamati ya shule ya msingi Buhangija.
Akizungumza wakati wa kukabidhi bweni hilo, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, amekipongeza Kikundi hicho cha Wanawake na Mabadiliko Manispaa ya Shinyanga kwa moyo wa kujitolea kulifanyia ukarabati bweni moja la wavulana ambalo lilikuwa limechakaa miundombinu yake, na hatimaye watoto hao wataishi kwenye mazingira mazuri.
Amesema jukumu la kulea watoto hao wakiwamo wenye ualbino ni la kila mtu na siyo kuiachia Serikali peke yake kuwatunza, ambapo jamii pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani ya mkoa wa Shinyanga na nje, wanapaswa kuwa hudumia ili kutatua changamoto zinazowakabili. “Serikali inakipongeza chama hiki cha Wanawake na Mabadiliko kwa kujitolea kufanya ukarabati wa bweni hili moja la wavulana kwenye kituo cha buhangija cha kulea watoto wenye ulemavu mbalimbali wakiwamo wenye ualbino, ili waishi katika mazingira mazuri,”amesema Mboneko.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto hawa, ikiwamo upungufu wa walimu maalumu, ukarabati wa miundombinu, pamoja na ujenzi wa uzio kwenye majengo mapya ili kuimarisha ulinzi,”ameongeza.
Naye katibu wa Kikundi cha Wanawake na Mabadiliko Manispaa ya Shinyanga (Women For Change - WFC), Lucy Mwita, amesema katika kuelekea kwenye kongamano lao la siku ya wanawake duniani, ambalo watalifanya siku ya Jumamosi,Machi 7,2020 wameona kabla ya tukio hilo ni vyema wafanye kitu kama wanawake, na kuamua kukarabati bweni hilo.
Mwita ametoa wito kwa uongozi wa kituo hicho kulitunza bweni hilo ambalo limegharimu kiasi cha Shilingi 2,450,000/= ili lidumu kwa muda mrefu na kutunza watoto hao katika mazingira mazuri, huku wakigawa zawadi ya juisi, na biskuti.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Buhangija na mlezi mkuu wa kituo hicho cha watoto wenye ulemavu mbalimbali wakiwamo wenye ualbino Seleman Kipanya, ameshukuru chama hicho kwa kukarabati bweni hilo, huku akiomba wadau wengine wajitokeze kufanya ukarabati mabweni yaliyosalia ili kuwaweka watoto hao katika mazingira mazuri ya kuishi.
Kikundi cha Wanawake na Mabadiliko Manispaa ya Shinyanga (Women For Change - WFC), kinajihusisha na Ununuzi wa Hisa ili kuinuana kiuchumi na chenye mfuko wa kusaidia jamii na watoto walioko kwenye mazingira magumu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...