Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
JESHI
la Magereza limeeleza kusikitishwa na kitendo cha viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kushindwa kutii sheria bila
shuruti na kuhatarisha usalama wa wafungwa, askari na mali za Jeshi la
Magereza na hiyo ni baada ya watu wanaoaminika kuwa ni wafuasi na
viongozi wa chama hicho wakiwa katika msururu ya magari binafsi na gari
za kubeba abiria kufika katika eneo la gereza la Segerea na kutaka
kuingia bila utaratibu.
Taarifa
iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Magereza SSP Amina Kavirondo
imeeleza kuwa Jana Machi 13, 2020 viongozi wa CHADEMA wakiwa na wafuasi
wao walifika eneo la Magereza wakiwa na makundi ya watu na msururu wa
magari binafsi na magari ya kubeba abiria na walipofika geti kuu
walitaka kuingia ndani na magari yao jambo ambalo ni kinyume na taratibu
za kiusalama katika eneo hilo ambalo limezuiliwa.
Taarifa
hiyo imeeleza kuwa Askari wa Jeshi la Magereza waliokuwa zamu
walijaribu kuwasihi watu wao na kuwaeleza kuwa ni mtu mmoja tuu
anayetakiwa kuingia ndani na kukamilisha utaratibu wa kumtoa mfungwa
aliyelipiwa faini lakini jitihada hizo za kufafanua utaratibu
hazikusaidia na watu hao walikaidi na kuendelea kuweka msongamano katika
eneo hilo la kiusalama na kutoa maneno ya kashfa, matusi, vitisho na
kumshambulia askari aliyekuwepo zamu na kumchania sare za Jeshi la
Magereza.
Imeelezwa kuwa
utaratibu wa kusimamia usalama wa eneo la Magereza na itifaki za
kiusalama magerezani zilifuatwa na watu hao kuondolewa kwa nguvu ya
wastani hadi nje ya eneo la Magereza.
Pia
taarifa hiyo imeeleza umma wa watanzania kuwa utaratibu unaotumika
kufika na kutembelea maeneo ya Magereza ikiwa ni kwa lengo la kuona
wafungwa au kuwatoa wafungwa waliomaliza adhabu yao utaratibu huanzia
mahakamani kwa kulipa faini na mahakama kutoa hati ya uthibitisho wa
kupokea malipo hayo hatimaye hati hiyo kukabidhiwa kwa mkuu wa gereza
ambaye hufuata taratibu na itifaki ya gereza na kumtoa mfungwa
aliyemaliza Kifungo.
Pia
imeelezwa kuwa wananchi lazima wafuate kanuni na Sheria za maeneo hayo
nyeti ya kiusalama yaliyozuiliwa kwa kutofanya mambo yaliyozuiliwa
ikiwemo kutoingia na simu au kamera, kupiga picha, kupiga kelele na
kuweka mikusanyiko.
Jeshi
hilo limetoa Rai na onyo kali na kueleza kuwa halitovumilia vitendo vya
mtu au kundi lolote litakalokaidi Sheria, kanuni na miongozo ya
utendaji kazi wa jeshi na limetoa pongezi kwa wananchi wote wanaotii
sheria bila shuruti na kuwakaribisha kuendelea na kupata huduma ambazo
jeshi la Magereza linatoa.
Msemaji wa Jeshi la Magereza SSP Amina Kavirondo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...