Charles James, Globu ya Jamii
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma limekabidhi magari matatu kwa Idara ya Mipango Miji kwa ajili ya kurahisisha shughuli za wataalamu wake katika kudhibiti ujenzi holela kwenye jiji hilo.
Hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa la kusimamia utekelezaji wa mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema magari hayo yamegharimu kiasi cha Sh Milioni 345 kwa idara ya mipango miji ambapo yatatumiwa na ofisi ya udhibiti ujenzi holela, mkuu wa upimaji na mkuu wa idara ya mipango miji.
Kunambi amesema halmashauri ya jiji inaamini ili kutekeleza agizo la MWaziri Mkuu ni lazima wawe na vitendea kazi ambavyo vitarahisisha ufanyaji kazi wa watalaamu wao.
" Mhe Mkuu wa Mkoa tunakushukuru kwa kuja kwenye tukio letu hili, haya ni mafanikio makubwa kwetu katika kuondoa changamoto ya vitendea kazi kwa wataalamu wetu ambao wanakua field muda wote kuhakikisha wanaondoa tatizo la ujenzi holela kwenye jiji letu.
Fedha hizi Milioni 345 ni fedha zetu za mapato ya ndani, Jiji la Dodoma hatuombi fedha serikali kuu kama halmashauri zingine. Sasa tunaamini hakuna nyumba yoyote ambayo itawekea X kwa sababu kabla hata ya kujenga wataalamu wetu watakua wameshatoa elimu kwa wananchi juu ya maeneo gani ya kujenga na ya yapi hayafai kujenga," Amesema Kunambi.
Ameongeza kuwa Jiji la Dodoma linapiga hatua kutokana na ushirikiano uliopo baina ya Ofisi yake, Mkuu wa Wilaya pamoja na Baraza la Madiwani linaloongozwa na Mstahiki Meya, Prof Davis Mwamfupe.
" Mhe RC hakuna Jiji lingine ambalo limepangwa vizuri kwa asilimia 100 zaidi ya Jiji letu la Dodoma, lakini pia Jiji letu limepimwa kwa asilimia 60 hatutaki kabisa kuharibu madhari ya Jiji letu na tunakuhakikishia mpango kabambe tuliokabidhiwa na Mhe Waziri Mkuu tutautekeleza kwa asilimia 100," Amesema Kunambi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amelipongeza jiji hilo kwa kupiga hatua ya kuwanunulia watalaamu wake magari ambayo pia yatakua msaada kwa wananchi waliokua wanasafiri umbali mrefu kufika ofisi za Jiji.
" Sitegemei kuwaona watalaamu ofisini, hizi gari tunazowakabidhi leo zitumieni vizuri kwa kwenda field walipo wananchi, muwape elimu nzuri ili kuepusha changamoto za baadae za ujenzi holela.
Hatutaki tena kuona ujenzi holela, wala kuona alama za X maana zikiendelea kuwepo zinatoa picha kwamba nyie watalaamu wetu hamfanyi kazi ipasavyo licha ya kukabidhiwa magari mazuri yanayorahisisha utendaji kazi wenu," Amesema Dk Mahenge.
RC Mahenge amelitaka Jiji la Dodoma kuhakikisha linaondoa pia changamoto ya wananchi kujenga kwenye maeneo ya wazi, milima pamoja na maeneo ya hifadhi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge akizungumza na wandishi wa habari baada ya kutoka kukabidhi magari matatu kwa idara ya mipango miji ya Jiji la Dodoma ili kusaidia kuongeza ufanisi wao wa kazi. Kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge akimkabidhi ufunguo wa gari Mkuu wa Idara ya Mipango Miji ya Jiji la Dodoma, Pius Mafuru katika hafla iliyofanyika leo.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi akizungumza na wandishi wa habari baada ya halmashauri ya Jiji lake kukabidhi magari kwa watalaamu wake wa mipango miji ili yaweze kusaidia katika kazi zao za kudhibiti ujenzi holela.
Mojawapo ya gari tatu ambazo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imezikabidhi kwa Idara yake ya Mipango Miji leo ili kusaidia kuboresha ufanisi kazi wao katika kudhibiti ujenzi holela wa Jiji hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...