KAMATI YA YAAGIZA ULINZI WA MIUNDOMBINU
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kuhakikisha inaweka ulinzi madhubuti katika miundombinu ya mradi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam ili idumu kwa kipindi kirefu.
Mradi huo wenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katika njia za barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 229 na huku Serikali ikichangia fedha za fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa mradi.
Ameyasema hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso wakati wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea ujenzi wa mradi huo na wajumbe hao kuridhika na hatua ya kazi zilizofikiwa kwa sasa ambao walimtaka mkandarasi kutimiza malengo kwa kadiri mkataba walivyousaini.
"Tunaipongeza Serikali, Wizara na TANROADS kwa kazi nzuri na usimamizi kwani tumefarijika kuona miundombinu ambayo imejengwa ni mizuri na kazi iliyofikiwa ni nzuri sana hivyo tunamategemeo kwamba miundombinu hii itawanufaisha watanzania", amesema Kakoso.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameihakikishia kamati hiyo kuwa watasimamia utekelezaji wa miundombinu bora ya Barbara kwa kila fedha inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
"Dhamira ya Serikali ni kuongeza ubora wa huduma za miundombinu ikiwemo ya barabara na pia kupunguza msongamano katika majiji na hasa jiji la Dar es Salaam na sisi Wizara tuwahakikishie kuwa tutaendelea kutekeleza miradi kama hii ya ubungo na maeneo mbalimbali", amefafanua Naibu Waziri huyo.
Amesema kuwa watanzania wanaopita katika barabara zetu wakipoteza muda mwingi katika foleni Serikali inapata hasara kubwa kwani uzalishaji unapungua hivyo miundombinu hii itakuwa ni mkombozi kwa Taifa kwa ujumla.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, ameieleza kamati hiyo kuwa ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kudumu miaka 120 ijayo na kupunguza msongamano wa magari kwa zaidi ya miaka 50 ijayo ndo hali hiyo ijirudie tena.
Aidha amewaeleza kuwa mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mapema mwishoni mwa mwezi wa Julai, 2020.
"Niwatoe hofu wajumbe kuwa mradi utakamilika mapema zaidi, mkandarasi yupo mbele ya muda na changamoto ya msongamano wa magari katika makutano haya utakuwa historia", Mhandisi Mfugale.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mheshimiwa Munde Abdallah, amesema wamefurahi kuona mradi kama huo wa kihistoria unatekelezwa katika nchi yetu na ni sifa kwa watanzania na Serikali yetu ya Awamu ya Tano.
"Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu na ndio kazi ya fedha za Serikali ya Awamu hii chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli yenye dhamira ya dhati ya kuhakikisha maendeleo ya Tanzania yanapatikana hivyo miundombinu hii mizuri ni kivutio kwa jiji la Dar es Salaam", amesema Mheshimiwa Munde.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, baada ya Kamati hiyo kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam
Mkandarasi kutoka Kampuni ya China Civil Engineering Construction Company Corporation (CCECC), Mhandisi Yuang, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, namna nguzo za zege zinavyotengenezwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Mkandarasi kutoka Kampuni ya China Civil Engineering Construction Company Corporation (CCECC), Mhandisi Yuang, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, namna nguzo za zege zinavyotengenezwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakikagua ngazi ya pili ya barabara ya juu iliyokamilika kujengwa katika makutano ya Ubungo. Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa ngazi zote unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Julai, 2020.
Muonekano wa ngazi ya pili iliyokamilika kujengwa katika barabara ya juu kwenye makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa barabara hizo za juu (Interchange) umefikia asilimia 70.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Wizara na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wakati kamati hiyo ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...