WAZIRI MKUU Kassim Mjaliwa amesema wanafunzi wanaosoma katika vyuo
vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kutokana na mlipuko wa homa
ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona wote wanaendelea na
masomo yao kwa njia ya mtandao.
“Tehama sasa imefikia katika hatua nzuri kwa sababu Mhadhili mmoja
anaweza kuwafundisha wanafunzi wake wote popote walipo kwa njia ya
mtandao. Tehama imewezesha wanafunzi waliozuiwa kurudi nchini China
kuendelea na masomo wakiwa nyumbani kwao.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 12, 2020) katika
mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja
wa Ilulu mjini Lindi. Amesema baada ya virusi vya corona kuikumba
China vyuo vilifungwa na sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasomo kwa
njia ya mtandao.
Pia, Waziri Mkuu amewaeleza wahitimu wa CKHT kuwa vyeti
walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha
katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe
wanaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi itakayoakisi viwango
vilivyoainishwa kwenye vyeti vyao.
“Nendeni mkaidhihirishe tuzo hii ya pili katika utendaji wenu na
maisha yenu ya kila siku, iwe ni katika sekta rasmi au sekta isiyokuwa
rasmi. Hakikisheni mnaonesha tofauti katika kutafuta majibu ya
maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania kuhusu mustakabali mzima
wa kujiletea maendeleo.”
Waziri Mkuu amesema amefuatilia kwa karibu maelezo ya Viongozi
waliotangulia kuhusu umuhimu na hata mafanikio ya chuo hicho ambapo
amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu
sana kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya
Taifa.
Amesema licha yachangamoto mbalimbali zilizopo, Serikali imeweza
kuanzisha chuo hiko na kukiona kikiendelea kutanuka hadi nje ya mipaka
ya nchi yetu. “Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia.
Tunawashukuru waasisi wa Taifa letu kwa maono haya makubwa kuhusu
Tanzania.”
Waziri Mkuu amesema Mwasisi wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, aliona mbali sana wakati akianzisha mchakato wa
kuanzisha Chuo hiki kwa kusema angependa kuona taasisi inawawezesha
watu wazima wengi waweze kuendelea na elimu ya juu pasipo kuacha kazi
zao.
Vilevile, aliongeza kwa kusema, “Kwa nchi maskini kama Tanzania,
hakuna Taasisi nyingine ya elimu ya juu inayoweza kuwa ya msaada zaidi
kwa watu wetu”.
Waziri Mkuu amesema ukweli wa kauli hiyo unaendelea kudhihirishwa siku
hadi siku kupitia mafanikio ya chuo hicho. “Tutake tusitake, elimu ya
juu inayoweza kusaidia watanzania wengi zaidi ni hii ya kupitia mfumo
wa Elimu Masafa na Huria.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa umuhimu na thamani ya Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania na vyuo vingine utakuwa na maana tu pale ambapo vitakuwa na
mchango kwenye maendeleo ya nchi.
“Kwa miaka nenda rudi, chuo kimehitimisha wataalamu lukuki, ambao
wengi wameingia kwenye sekta mbalimbali za utumishi na uzalishaji na
kutoa mchango muhimu sana kwenye maendeleo ya nchi yetu.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa uongozi wa CKHT na Tume ya
Vyuo Vikuu nchini (TVV) wahakikishe kuwa udahili wa CKHT unatanuliwa
kwa sababu hadi sasa chuo kina kozi moja tu ya maandalizi kwa ajili ya
kuwaandaa vijana kuingia kwenye Shahada.
Waziri Mkuu amesema katika kuongeza udahili kwenye elimu ya juu,
ameshauri wawe na kozi ama programu za maandalizi kwa wale wanaotaka
kusoma stashahada na kwa wale wa cheti pia.
Amesema matokeo ya programu hizo yataongeza ushiriki wa Watanzania
wengi kwenye elimu ya juu. “Wito wangu kwa TCU nchini kuhakikisha
inasimimia na kuongoza, kwa kushirikiana na CKHT katika uanzishwaji wa
programu hizi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora wa elimu ya
juu.”
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 698 walitunikiwa vyeti
wakiwemo 20 wa Shahada za Uzamivu (PhD) na wengine 185 Shahada na
Stashahada za Uzamili, wengine 344 walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 166
walitunikiwa Stashahada na Astashahada mbalimbali.
Mahafali hayo yamehudhuliwa naWaziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo
Kikuu Huria Cha Tanzania Mizengo Peter Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Lindi na
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Chuo Mkoani Lindi Godfrey W. Zambi,
Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania,
Profesa Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha
Tanzania Profesa Elifas Tozo Bisanda na wakuu wa wilaya za mkoa wa
Lindi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...