Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli
ametoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara na watu
wenye mapenzi mema kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji maalumu kwani
kwa kufanya hivyo ni kutimiza amri kuu ya upendo ya Mwenyezi Mungu
isemayo pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi.
Mama magufuli ameyasema hayo wakati akitoa misaada mbalimbali kwa
vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu vya Cheshire Home na
Nyumba ya Matumaini katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino
jijini Dodoma Alhamisi Machi 19, 2020.
Mama Magufuli amekabidhi misaada hiyo kwa wawakilishi wachache wa
watoto hao walioongozana na baadhi ya walezi wao, ikiwa ni hatua ya
utekelezaji wa agizo la serikali la kuepuka mikusanyiko ya watu isiyo
lazima kutokana na janga la ugonjwa wa mafua makali ya CORONA.
Mke wa Rais amesema hivi sasa ni kipindi cha Kwarezma ambapo ni
kumbukumbu ya mateso ya Yesu Kristo, na kwamba kwa mujibu wa Isaya
58:7 waumini wanahimizwa kufunga, kuomba na pia kujitoa kwa wenzao
wenye mahitaji mbalimbali.
"Kwa kuzingatia hilo nami leo nimewaita hapa ili kutoa kazawadi kangu
kadogo kwa wanangu hawa", alisema Mama Magufuli.
Misaada aliyotoa ni pamoja na mchele tani mbili, unga wa sembe tani
mbili, maharage kilo 830, mafuta ya kupika lita 830, sukari, vinywaji,
biskuti, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kupaka, mashuka, nguo,
viatu pamoja na vyandarua.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...