Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kulia) akizungumza
na Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira
walipotembelea eneo la Kaole, Wilaya ya Bagamoyo.

Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kulia) akiteta jambo na
Waziri wa Kazi, Usalama wa Zambia Mhe. Joyce Simukoko walipokuwa
wakiangalia eneo la Makaburi ya Wapendanao yaliyopo eneo la Kaole Wilaya
ya Bagamoyo Machi 6, 2020.

Sehemu ya
Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na
Ajira wakiangalia eneo la kaburi la Imamu aliyekuwa na uwezo wa kutabiri
mambo mbalimbali lililopo katika eneo la Kaole wilaya ya Bagamoyo.

Baadhi ya
Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na
Ajira (waliokaa) wakiangalia kikundi cha Ngoma Asilia cha Kaole
walipotembela Magofu ya Kaole yaliyopo eneo la Kaole wilaya ya Bagamoyo.

Waziri wa Kazi,
Uzalishaji na Ukuzaji Ujuzi wa Botswana Mhe. Mpho Balopi (wa tatu kutoka
kushoto) akipiga ngoma pamoja na wanakikundi cha ngoma asilia cha
Kaole. Wa pili kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.
Jenista Mhagama na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Kawawa.

Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akieleza
jambo kuhusu Programu ya Ukuzaji Ujuzi kwa Vijana kwa Mawaziri na Wadau
wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira.

Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akikata keki pamoja na Mawaziri wa
SADC sekta ya Kazi na Ajira walipotembelea Chuo cha Don Bosco kujionea
utekelezaji wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi. Kulia ni Waziri wa Kazi,
Usalama wa Zambia Mhe. Joyce Simukoko na Waziri wa Kazi na Ajira Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Ilunga Nkulu Nene (wenye miwani).

Baadhi ya Vijana
wa fani ya umakenika waliopo katika chuo cha Don Bosco wakitengeneza
vipuri vya magari wakati walipotembelewa na Mawaziri na Wadau wa Utatu
wa SADC sekta ya Kazi na Ajira.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
*********************************
Na: Mwandishi Wetu
Mawaziri na Wadau
wa Utatu wa Nchi Wananchama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) sekta ya kazi na ajira waipongeza Serikali ya Tanzania kwa
mikakati iliyojiwekea katika kuwajengea uwezo vijana kupitia Programu ya
Taifa ya Kukuza Ujuzi.
Pongezi hizo
zimetolewa na Mawaziri na Wadau wa utatu wa Jumuiya hiyo ikiwemo Jukwaa
la Vyama vya Waajiri Kusini mwa Afrika (SPSF), Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Kusini mwa Afrika (SATUCC), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na
Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji kanda ya
Kusini mwa Afrika (IOM).
Akizungumza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) na waandishi
wa habari wakati wa ziara yake aliyoambatana na Mawaziri na Wadau wa
Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipotembelea Chuo cha Don Bosco
Network kilichopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam na Maeneo ya Vivutio
vya Utalii Bagamoyo alieleza kuwa Serikali iliamua kuanzisha programu
hiyo lengo ikiwa ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana
kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuajiriwa au
kujiajiri.
“Mawaziri na Wadu
wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira wamefurahia kuona namna
Serikali inavyotekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuza kwa Vijana
ambayo kwa kiasi kikubwa itawawezesha vijana kupata uwezo na ujuzi
unaohitajika katika soko la ajira kwa nchi hizo wanachama,” alisema
Waziri Mhagama.
“Zipo nchi
wananachama wameomba kukutana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inatekeleza
programu hiyo kwa lengo la kuweza kupata uelewa wa taratibu na namna ya
kutekeleza programu hiyo, nchi ya Eswatini tayari imeonyesha nia ya
kukutana na ofisi yangu ili nao waweze kuanzisha programu hiyo nchini
kwao,” alieleza Mhagama
Alieleza kuwa
wakati wa uzinduzi rasmi wa Mkutano huo wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa
SADC sekta ya Kazi na Ajira uliozinduliwa Machi 5, 2020 na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
Serikali iliona umuhimu wa kuzindua Programu mmoja wapo ambayo ni
Programu ya Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi (Internship) ili kuelezea
nchi wanachama mikakati ambayo Serikali imejiwekea katika kutatua
changamoto ya ajira inayowakabili vijana kwa kuwawezesha vijana kuwa na
uzoefu katika utendaji kazi.
Aidha aliongeza
kuwa katika mkutano huo uliowakutanisha waliweza kujadili masuala
mbalimbali yanayohusu sekta ya Kazi na Ajira ambazo ni masuala ya
Hifadhi ya Jamii, Uhamishaji wa nguvu kazi, mapitio ya sera na miongozo
iliyotungwa na nchi wanachama kuhusu masuala ya kazi na ajira, haki na
wajibu wa wafanyakazi, mapitio ya mikataba ya kimataifa na mikataba ya
Shirika la Kazi Duniani (ILO) inayoongoza masuala ya ajira pamoja na
kuwajengea uwezo vijana.
Kwa upande wake
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony
Mavunde wakati akielezea kuhusu programu ya ukuzaji ujuzi kwa Mawaziri
na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira alieleza kuwa Programu
hiyo ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inafadhiliwa na Serikali kwa lengo la
kuwawezesha vijana ambao kwa asilimia kubwa ndio nguvukazi ya taifa
wanapata ujuzi na uzoefu ambao utawafanya waweze kujitegemea.
“Hii ni habari
njema kwa sisi Watanzania kutembelewa na Mawaziri na Wadau wa Utatu
ambao wamekuja kujionea namna serikali yetu inavyowajali vijana na jinsi
inavyowatumikia katika kuwawezesha kupata ujuzi ambao utawasaidia pindi
vijana hao wanapomaliza mafunzo waweze kujiajiri ama kuajiriwa,”
alisema Mavunde
Alifafanua kuwa
Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu Programu ya Ukuzaji Ujuzi ikiwemo Mafunzo
kwa Njia ya Uanagenzi, Mafunzo ya Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje
ya Mfumo Rasmi, Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi kwa Wahitimu na
Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa walio Makazini na Mpango huo wa
Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior
Learning).
Katika ziara hiyo
Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipata
fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria yaliyopo Bagamoyo ikwemo Ngome
Kongwe, Soko la zamani la Watumwa, Bandari iliyokuwa inatumika
kuwasafirisha watumwa, eneo la Msalabani ambapo Ukristo ulianzia
kuenezwa hapo na wakoloni, Magofu ya Kaole lengo la ziara hiyo ilikuwa
kutangaza maeneo ya vivutio vya kihistoria vilivyopo hapa nchini.
Waziri wa Kazi na
Ajira Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Ilunga Nkulu Nene alieleza
kuwa wamevutiwa sana na maeneo ya kihistoria yaliyopo Tanzania na ni
nchi ya kuigwa.
“Nchi ya Kongo
ina maeneo mengi ya kitalii lakini hatuyatangazi kama Tanzania
inavyofanya, kama kiongozi nimejifunza jambo katika ziara ya leo na
hivyo nitakaporudi Kongo nitahamasisha utangazaji wa maeneo ya
kihistoria yaliyopo kwa lengo la kuvutia watalii,” alisema Nene
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...