Charles James, Michuzi TV
Serikali imesitisha mashindano ya michezo kwa wanafunzi katika ngazi ya Shule ya Msingi na Sekondari (Umiseta, Umitashumta) yaliyokua yafanyike hivi karibuni kutokana na tishio la maambukizi ya ugonjwa wa Corona hadi hapo itakapotangazwa baadae.
Akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amesema pamoja na kusitisha mashindano hayo pia shule zitakazofanya mahafali ya kidato cha sita hazitoruhusiwa kualika wageni kutoka nje ya shule.
Waziri Jafo amesema pamoja na Wizara ya Afya kupitia kwa Waziri Ummy Mwalimu kuthibitisha kutokuepo kwa mgonjwa wa Corona bado tahadhari zinapaswa kuchukuliwa za kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.
" Nikiwa kama Waziri wa TAMISEMI ambaye nasimamia elimu ya Msingi na Sekondari tunasitisha mashindano haya kwa mwaka huu lakini pia hata mahafali ya kidato cha Sita kama shule zitaona umuhimu wa kuyafanya basi yahusishe wanafunzi na watumishi wa shule husika na siyo wageni, wazazi ambao wamekua na Kawaida ya kuhudhuria, hii yote ni katika kuchukua hatua za ugonjwa huu wa Corona," Amesema Mhe Jafo.
Amesema licha ya mashindano ya Umiseta na Umitashumta kupata mafanikio makubwa chini ya serikali ya awamu ya tano ya kuibua vipaji vya watoto wengi lakini bado wameona kuna haja kubwa ya kusimamisha mashindano hayo kwani mazingira hayajawahi rafiki kutokana na hofu ya Corona.
Hivyo amewataka wanafunzi wote wanaohusika na michezo hiyo kuanzia Shule za Msingi na Sekondari kubakia kwenye shule zao na kuendelea na masomo kama kawaida.
" Kuhusu mahafali ya kidato cha sita, hatujakataza kufanyika tunachosema kama kuna haja ya kufanya mahafali hayo basi shule zinazofanya zisihusishe wageni kutoka nje ya shule badala yake wafanye walimu, wanafunzi na watumishi wa shule husika," Amesema Mhe Jafo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumza na wandishi wa habari leo ofisini kwake kuhusu kusimamisha mashindano ya michezo kwa Shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...