Mkutano wa Maafisa Waandamizi ambao ni mkutano wa awali wa maandalizi ya Baraza la Mawaziri la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajia kufanyika tarehe 18 Machi 2020 umefunguliwa rasmi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Akifungua mkutano huu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafisa Waandamizi wa SADC, Balozi Kanali Wilbert Ibuge amewashukuru wajumbe wote kutoka nchi wanachama pamoja na wataalamu wa TEHAMA kwa jitihata walizoonesha kuhakikisha mkutano huu kwa mara ya kwanza unafanyika kwa mfumo wa Video.
“ Hii ni uthibitisho siyo tu wa namna ambavyo Teknolojia ya Habari na Mawasilisno imebadilisha na itaendelea kutubadilisha namna tunavyowasiliana bali pia ambavyo matishio ya majanga ya kidunia kama ugonjwa wa Virusi vya CORONA (COVID 19) yanavyotulazimisha kutafuta mbinu mbadala za kufanya mambo yetu kikanda na kidunia pamoja na kuendelea kuimarisha ushirikiano bila kuonana ana kwa ana” alisema Balozi Ibuge
Mkutano huu unahudhuriwa na Maafisa Waandamizi kutoka nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana ya masuala ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha, Uchumi, Mipango pamoja na Viwanda na Biashara.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharikia na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafisa Waandamizi wa SADC, Balozi Kanali Wilbert Ibuge ambaye ameambatana na maafisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wizara ya Viwanda na Biashara Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Maafisa wengine waandamizi walioshiriki ni pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Ndani. Vilevile mkutano huu umehudhuriwa na baadhi ya Mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha katika nchi za SADC ambao ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Mkutano huu utajadili ajenda chache za muhimu kwa wakati huu ambazo ni: Taarifa ya Maandalizi ya Dira ya SADC ya 2050; Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC 2020-2030; Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980; Utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita; Hali ya michango na kifedha kwa ujumla ya SADC; na Kupokea taarifa ya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za Sekretarieti SADC.
Awali mkutano katika ngazi ya Maafisa Waandamizi ulipangwa kufanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi 2020 na kufuatiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri tarehe 17 na 18 Machi 2020.
Hata hivyo, kufuatia ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na Mawaziri wa Afya kutoka Nchi Wanachama wa SADC walipokutana kwa dharura tarehe 9 Machi, 2020. Mkutano huo ulijadili na kupendekeza kwa Nchi Wanachama namna ya kuzuia maambukizi ya mlipuko wa ugonjwa hatari wa virusi vya Corona (COVID 19) unaosambaa kwa kasi na kuleta athari kubwa duniani tangu kubainika kwakwe mwezi Desemba.
![]() |
Maafisa Waandamizi wa nchi za SADC wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano kutokea nchini Tanzania kupitia mfumo wa video |
![]() |
Mkutano ukiendelea.
|
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...