Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia
maswala ya Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima akiwa katika moja ya chumba kilicho
andaliwa kwa ajili ya kutolea kuhuduma kwa wagonjwa wa COVID-19 (CORONA)
katika halmashauri ya Ikungi mkoani Singida.

Baadhi ya Watumishi kutoka Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakikagua dawa
zilizoandaliwa katika kituo cha Ilongero cha kuhudumia wa wagonjwa wa
COVID-19 (CORONA) katika halmashauri ya Singida mkoani Singida.
……………………………………………………………………………………….
Na. Majid Abdulkarim, Singida
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia
maswala ya Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na
Halmashauri watoke ofisini kukagua utayari wa vituo vya kutolea huduma
za Afya katika kukabiliana na virusi vya COVID-19(CORONA) na kuhakikisha
vituo vilivyotengwa katika kila Halmashauri nchini vinakidhi vigezo vya
kutoa matibabu ya COVID-19(CORONA).
Dkt.Gwajima amesema kuwa taarifa
ya zoezi hilo itumwe kila baada ya masaa 24 Ofisi ya Raisi, TAMISEMI
kukiri kuwa viongozi hao walifika kituo gani na yatakonayo na ziara hiyo
ni yepi katika kituo husika.
Dkt.Gwajima ameagiza hayo leo
akiendelea na ziara yake ya kukagua matayarisho ya vituo kwa ajili ya
kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 (CORONA) katika halmashauri za Singida,
Ikungi na Manyoni mkoani Singida.
Aidha Dkt.Gwajima amesisitiza kuwa
kila mjumbe wa Kamati ya Afya Halmashauri apewe vituo vya kuvifuatilia
kila siku kwani ni sehemu ya moja wapo ya majukumu yao na hususan
kipindi hiki ambapo nchi inapambana na maradhi haya.
“kila Mkuu wa Kituo ahakikishe
amewashirikisha watumishi wote, Kamati ya Afya ya Kituo na Wahudumu wa
Afya Ngazi ya jamii katika kupanga na kutekeleza mikakati ya kupambana
na Covid-19(CORONA)”,ameeleza Dkt.Gwajima.
Pia Dkt.Gwajima ameongeza kuwa
Kamati za Afya ya Msingi ngazi ya mkoa na halmashauri zihakikishe kila
mjumbe anao mpangokazi wake wa ufuatiliaji na uhamasishaji juu ya
ugonjwa huu ili kuleta uelewa kwa jamii mfano, Afisa Biashara anatakiwa
kuhakikisha wafanya biashara wote wanaelewa vizuri dhana nzima ya
kujikinga ili biashara zao zisiwe chanzo cha kuchochea maambukizi.
Katika ziara hii, Dkt Gwajima
ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Manyoni kwa jinsi ambavyo
wamezingatia maelekezo na kuyafanyia kazi ikiwemo matayarisho ya vituo
kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 (CORONA) kwa ushirikiano na
viongozi wa jamii ngazi zote wakiwemo Mhe Diwani Kata ya Chikuyu,
Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji cha Mwiboo na Mwenyekiti wa Kijiji
hicho.
Naye Diwani wa Kata ya Chikuyu
wilayani Manyoni Bw.Benjamini Kamwoga amesema kuwa, wananchi wa Chikuyu
wako bega kwa bega na serikali yao katika kupambana dhidi ya ugonjwa
huu.
“Ili kuonyesha kuwa janga hili ni
letu sote kesho wananchi watakuja kwa awamu ili kusafisha mazingira ya
kituo hiki ikiwa ni sehemu moja wapo ya kuaanda mazingira rafiki ya
kupambana na ugonjwa huu” amesema Bw.Kamwaga.
Kwa kuhitimisha Dkt Gwajima
amewapongeza watumishi wote wa sekta ya afya, wananchi na wadau wote
kwa ujumla kwa jinsi wanavyojitoa katika vita dhidi ya Covid-19.
Amewataka wataalamu kuendelea kushirikiana na wadau wote ngazi zote za
jamii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...