NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata Wahamiaji haramu 51 walioingia nchini kupitia bandari bubu ya ya Makurunge Tarafa ya Yombo Wilayani Bagamoyo Mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo alisema wahamiaji hao walikamatwa majira ya saa 11 alfajiri Mach 19.
Wankyo alisema, watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa vyombo vingine vya dola kwa taratibu za kisheria waweze kuchukuliwa hatua.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa alisema, wahamiaji hao wamekutwa katika pori wakiwa katika harakati za kutafuta usafiri kuelekea Mikoa ya Nyanda za juu Kusini ili waweze kuendelea na safari yao hadi Afrika Kusini.
Kawawa lisema, Wahamiaji hao walikuwa wanaotokea nchini Ethiopia, ambao katika mahojiano ya awali walikiri kuingia Nchini kwa kupitia Pwani ya Bagamoyo, wakitumia majahazi.
Alisema, Wahamiaji hao walichukuliwa hadi katika kituo cha Afya Matimbwa (Bagamoyo) ili kupimwa kama Wana maambukizi ya Virusi vya Corona.
Kituo hicho kilichotengwa na Halmashauri kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa Corona wanaoweza kujitokeza siku za usoni, .
Wahamiaji hao, wamefikishwa katika kituo hicho ili kufanyiwa vipimo vya awali kujiridhisha kama hawana maambukizi ya ugonjwa wa Corona, kabla ya kupelekwa katika gereza la Kigongoni Wilayani Bagamoyo wakisubiri kusomewa mashtaka yao ya kuingia Nchini bila kibali
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji na kufukia mwili wa marehemu..
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa alisema, watuhumiwa hao walikamatwa Machi 19 huko Kibindu Wilaya ya Bagamoyo wakituhumiwa kuua na kuzika mwili wa marehemu (jina linahifadhiwa)katika shamba la mahindi.
Wankyo alisema, Machi 3, majira ya saa nane mchana huko Kibindu mtuhumiwa Chacha Machangu (27) alimfumania mke wake akiwa na mwanaume mwingine .
Kamanda alisema, Machangu alimshambulia mke wake kwa kumkata na panga maeneo mbalimbali ya mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo.
Wankyo alisema, Machangu kwa kushirikiana na ndugu zake Emmanuel Machangu (19) na Hamis Machangu (22 walichimba shimo kwenye shamba la mahindi na kufukia mwili wa marehemu.
Kamanda alibainisha kuwa, Machi 19 Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambapo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu ambao walionyesha shimo lilipo na lilipofukuliwa mwili wa marehemu ulipatikana.
Alisema, mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari na kufanyiwa mazishi kwa kufuata taratibu.
Jeshi hilo limesema, bado linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaodaiwa kushiriki katika tukio hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...