NA TIGANYA VINCENT
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasi na Utalii
wameitaka Serikali kutoa tuzo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey
Mwanri kwa jitihada zake za upandaji miti katika eneo hilo.
Walisema kuwa ushiriki wake moja kwa moja na uhamasishaji wake katika
jamii kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu umesaidia kujenga uelewa
wa umuhimu wa upandaji na utunzaji miti katika eneo hilo.
Mjumbe Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua Magdalena
Sakaya alisema juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora zimesaidia
kuwaelimisha wanafunzi kutoka Shule za Msingi kujifunza umuhimu wa
upandaji wa miti katika mazingira.
Alisema hatua hiyo imesaidia miti kuanza kuenea katika maeneo
mbalimbali na kuondoa uwezekano wa Mkoa huo kugeuka jangwa.
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay alisema viongozi
wengine ni vema wakaiga mfano huo ili waweze kuinusuru Tanzania
kugeuka jangwa.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Chambani Yusuph Hussein alisema
tafiti zinaonyesha kuwa kila mwaka kuna haribifu wa hekta 500,000 za
miti na ambazo zinapandwa ni hekta 200,000 na zinazopona ni hekta 100.
Alisema ni vema viongozi mbalimbali wakaongeza juhudi katika upandaji
miti na kulinda visiki vya miti iliyokatwa vising’olewe ili kurejesha
uoto wa asili.
Hussein alisema jitihada za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha miti
mingi inapanwa na kuitunza na kudhibiti uharibifu wa mistu ili
kuinusuru Tanzania isigeuke kuwa jangwa katika kipindi cha miaka
michache ijayo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kemerembe Lwota alisema wajumbe kwa
kuridhika na juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika suala zima la
usimamiaji wa mazingira na upandaji miti wanaishauri Serikali kumpa
tuzo.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuwahamasisha na viongozi wengine
kuongeza juhudi katika suala zima la kulinda miti asili na kupanda
mipya.
Lwota alisema kama Serikali itashindwa kutoa tuzo hizo wao watampatia
tuzo kwa kutambua mchango wake aliounyesha wa upandaji miti mkoani
Tabora.
Akijibu hoja za Wabunge, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis
Kigwangalla alisema kwa kutambua juhudi za Mkuu huyo wa Mkoa
wanakusudia kumpa tuzo wakati wa maadhimisho ya wiki ya asili ambayo
yatafanyika Kitaifa Mkoani humo mwezi Mei mwaka huu.
Alisema serikali itaendelea kuthamini na kutambua juhudi za wadau
mbalimbali ambao wanashiriki katika uhifadhi wa mazingira na upandaji
miti kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho
Waziri wa Maliasi na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla akitoa ufafanuzi juzi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakipokuwa na ziara ya kikazi mkoani Tabora kukagua shughuli mbalimbali katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki(BTI).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalli Kemirembe Lwota( wa pili kutoka kushoto) akiongozana na wajumbe wa Kamati yake na Viongozi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora(BTI) kukagua shughuli mbalimbali wakati wa ziara yao ya kikazi juzi mkoani Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa taarifa kwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasi na Utalii kuhusu uhifadhi wa maliasi
na upandaji wa miti katika Wilaya mbalimbali mkoani humo juzi wakati
wajumbe hao walipokuwa na ziara ya kikazi
Picha na Tiganya Vincent
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...