Veronica Simba – Dar es Salaam
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesisitiza msimamo wa serikali kutoruhusu uagizwaji nje ya nchi, vifaa vya umeme hususan mashine umba (transfoma) na nyaya na kwamba atakayebainika kukaidi agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria zinazohusiana na uhujumu uchumi.
Alitoa msimamo huo jijini Dar es Salaam, Machi 12 mwaka huu, baada ya kutembelea kiwanda cha Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL), kinachozalisha vifaa hivyo na kujiridhisha kuwa uwezo wake unatosheleza mahitaji ya sasa nchini.
Akiwa ameambatana na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Waziri alitoa tamko rasmi la serikali kuwa msimamo wake unabaki palepale.
Alisema, miradi mingi ya umeme imekuwa ikichelewa huku wakandarasi husika wakilalamika kuwa wanakwamishwa na ukosefu wa vifaa, jambo ambalo serikali imejiridhisha kuwa siyo kweli.Akitoa mfano wa uwezo wa uzalishaji kwa kiwanda hicho alichotembelea, Dkt Kalemani alibainisha kuwa kinazalisha zaidi ya mashine umba 75,000 kwa mwaka wakati mahitaji ya nchi ni 21,000 pekee.
“Sasa, hawa tu peke yake wanazalisha zaidi ya mahitaji yetu ukiachilia mbali viwanda vingine tulivyonavyo nchini ambavyo ni pamoja na TANALEC, AFRI-CABLE na wengineo,” alibainisha.
Aidha, aliongeza kuwa, kwa upande wa nyaya, baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakilalamika kwamba hazitoshelezi mahitaji jambo ambalo alisema siyo kweli kwani baada ya kukagua amejiridhisha kuwa kiwanda hicho pekee kina shehena ya kutosha.
Kuhusu malalamiko ya uhaba wa mashine umba za KVA 11, Waziri alibainisha kuwa amejiridhisha zipo nyingi zinazotosheleza mahitaji na alitoa maagizo kwa watendaji wa REA kuanza mara moja kuchukua oda yao waliyokuwa wameagiza kiwandani hapo ili miradi ya umeme vijijini iendelee kutekelezwa kwa kasi kutokana na uhitaji walionao wananchi kwa nishati hiyo muhimu.
Katika hatua nyingine, Waziri aliwapongeza wamiliki wa kiwanda hicho ambao pia kampuni yao (State Grid Electrical & Technical Works Ltd) ni moja ya zilizopewa dhamana na serikali kutekeleza miradi ya umeme vijijini, huku akiwaasa wakandarasi wengine nchini kuiga mfano wao kwa kuanzisha viwanda vyao wenyewe vyenye kuzalisha vifaa watakavyotumia katika kutekeleza miradi hiyo pamoja na kuwauzia wengine.
Hata hivyo, aliiagiza kampuni hiyo kuhakikisha inakamilisha kazi yake katika mikoa iliyopewa kimkataba ya Lindi na Morogoro kufikia mwezi ujao (Aprili) kwani hakuna sababu ya kutotekeleza kwa wakati ilhali vifaa wanavyo.
Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakitoa salamu za ukaribisho kwa Waziri, wamiliki wa kiwanda, Aloyce Ngowi na Charles Mlawa pamoja na Meneja Mkuu Pamela Irengo, waliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, wakisema ndiyo iliyowatia chachu ya kuanzisha kiwanda hicho.
“Tulipata hamasa kutoka kwa Rais John Magufuli kutokana na msisitizo wake katika kujenga uchumi wa viwanda, hivyo nasi tukaitumia fursa hii ipasavyo.”
Aidha, walimpongeza Waziri Kalemani na watendaji wote wa Wizara kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiwapatia katika utendaji kazi wao.
Kampuni hiyo inayomilikiwa na wazawa kwa asilimia 100 imeajiri wafanyakazi 300 ambao wote ni watanzania na imeanza mchakato wa kupanua kiwanda husika kitakachojengwa eneo la Kisemvule wilayani Temeke ili kukidhi kwa ufanisi zaidi mahitaji ya wateja wake.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani-katikati), akisikiliza maelezo kuhusu uzalishaji nyaya za umeme kutoka kwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL), Charles Mlawa, alipotembelea kiwanda hicho kinachozalisha mashine umba (transfoma) na nyaya za umeme, Machi 12, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akisikiliza maelezo kuhusu kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme na mashine umba (transfoma) kinachomilikiwa na kampuni ya Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL) kutoka kwa Meneja Mkuu, Pamela Irengo (kulia kwa Waziri), alipotembelea kiwanda hicho Machi 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Waziri ni Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga.
Mmoja wa waajiriwa wa kiwanda cha kutengeneza mashine umba (transfoma) na nyaya za umeme, kinachomilikiwa na kampuni ya Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL), Farida Karim akiwa kazini. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) kiwandani hapo, eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, Machi 12 mwaka huu.
Sehemu ya shehena ya mashine umba (transfoma) zinazozalishwa na kampuni ya Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL) iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) kiwandani hapo, Machi 12 mwaka huu.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua sehemu mbalimbali za kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme na mashine umba (transfoma) kinachomilikiwa na kampuni ya Europe Inc. Industries LTD (TROPICAL) iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam, akiwa katika ziara ya kazi, Machi 12 mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...